Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgodi wapewa siku 14 kudhibiti maji taka

637c24326eb3a725bc6c31f37f628d6d.jpeg Mgodi wapewa siku 14 kudhibiti maji taka

Wed, 14 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imesema uwekezaji wowote ni lazima uzingatie Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 na Kanuni zake ikiwa ni pamoja kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) kwa kuwa ni takwa la kisheria.

Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Hassan Chande ametoa kauli hiyo jana mjini hapa baada ya ziara ya kukagua migodi ya uchimbaji wa makaa ya mawe ya Tancoal Ltd na Ruvuma Coal.

Naibu Waziri ametoa siku 14 kwa Mgodi wa Tancoal kudhibiti maji taka katika mabwawa yao pamoja na kudhibiti vumbi ambalo limekuwa kero kwa wakazi wa maeneo ya jirani.

“Mazingira ndio uhai wetu, tuyatunze na tuyalinde kwa gharama yoyote ile,” alisisitiza Chande.

Naibu Waziri alishuhudia ukataji wa miti kwa kiwango kikubwa katika migodi hiyo na kuwaagiza migodi yote miwili kuandaa mpango wa muda mfupi wa upandaji miti ili kurejesha uoto wa asili.

Aidha, ameagiza migodi hiyo ya makaa ya mawe kuhakikisha wanaandaa na kutekeleza mpango madhubuti wa kurejesha ardhi katika hali ya awali baada ya shughuli za uchimbaji kukamiika ikiwamo kupanda miti kwa wingi.

“Upandaji miti uwe ni utamaduni wetu, hapa mgodini miti mingi imekatwa, wekeni mkakati wa kuirejesha kipindi cha mvua,” aliagiza.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri amemuagiza Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kusini, Jamal Baruti kufanya kaguzi za mara kwa mara ili kuhakikisha masuala ya uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira yanakuwa endelevu.

Akiwasilisha taarifa ya wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Aziza Mangosongo alisema jitihada na mikakati imechukuliwa kudhibiti vitendo vya uchafuzi na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za uchimbaji wa madini kwa kufanya ufuatiliaji na usimamizi wa mara kwa mara kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.

Uchimbaji, uchakataji na uuzaji wa madini ya makaa ya mawe wilayani Mbinga zilianza mwaka 2012 kupitia Kampuni ya TanCoal Energy Ltd na siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la kampuni zinazojikita katika utafiti na uwekezaji kwenye sekta ya madini.

Chanzo: www.habarileo.co.tz