Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgodi wa North Mara watozwa faini Sh1 bilioni

Mgodipiic Data Mgodi wa North Mara watozwa faini Sh1 bilioni

Sun, 24 Apr 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameutoza faini ya Sh1 bilioni mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara baada ya kupasuka kwa bomba katika kijiji cha Nyangoto wilayani Tarime.

Pia, amemuondoa katika nafasi yake ofisa mgodi mkazi, Hamad Kallaye kwa madai ya kushindwa kutimiza wajibu wake.

Akizungumza baada ya kufika katika eneo hilo leo Jumapili Aprili 24, 2022, Biteko amesema kuwa faini hiyo inatakiwa ilipwe ndani ya siku 14 kuanzia leo.

" Maji yamevuja kwa zaidi ya saa nne bila kuchukua hatua zozote wakati hapa mtu akiingia na kuiba atapatikana ndani ya nusu saa tu hivi kama haya maji yangekuwa na sumu leo tungekuwa tunaongea lugha gani" amesema Biteko

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesema bomba hilo lililopasuka linatoa maji katika bwawa linalokusanya maji kutoka kwenye miamba ya mashimo ya dhahabu kwenye mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara na si kwenye bwawa la sumu kama ilivyodhaniwa awali.

Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa, Jerome Kayombo amesema lipo bwawa maalum linalokusanya maji  yanayotiririka kutoka kwenye miamba kwa ajili ya kuhifadhiwa  kabla ya kusafirishwa kwa ajili ya kutibiwa na kutumika kwa matumizi ya kawaida.

" Lipo bwawa maalum linalokusanya maji kutoka kwenye miamba ambayo kwa asili yana tindikali kwahiyo yakishajaa kwenye bwawa yanasafirishwa kwenye mfumo kwa ajili ya kutibiwa ili kuingia kwenye mfumo wa matumizi ya kawaida," amesema

Amesema kuwa mara baada ya tukio hilo kutokea,  juzi wataalam kutoka NEMC  walifika katika eneo hilo na tayari wamechukua sampuli za maji kutoka katika maeneo tofauti ikiwemo kwenye mto Tigite  ili kupima ubora wa maji hayo.

Naye Meneja wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Ziwa, Musa Kazimila amesema vipimo vya awali vinaonyesha  maji katika eneo hilo ni salama, ingawa uchunguzi wa kina unaendelea na majibu yanatarajiwa kutoka Jumatano Aprili 27, 2022.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally lly Hapi amesema Serikali ya mkoa itaweka utaratibu maalum wa kulinda maeneo ambayo ni hatarishi ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

Kwa upande wake Meneja wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko amesema baada ya kupata taarifa za kupasuka kwa bomba hilo walifika eneo la tukio kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi ili kuzuia hali hiyo.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz