Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mghwira ampa siku tatu mkurugenzi manispaa ya Moshi

Wed, 9 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amempa siku tatu mkurugenzi manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi kuandika maelezo kuhusu kushindwa kusimamia taratibu za uendeshaji wa masoko na usafi katika manispaa hiyo.

Akizungumza leo Jumatatu Januari 7, 2019 Mghwira amesema sifa za manispaa hiyo kwa usafi zimepotea kutokana na uzembe unaofanywa na baadhi ya watendaji wa halmashauri na wanasiasa.

Mkuu huyo wa mkoa leo amefanya ziara ya kushtukiza katika soko la Mbuyuni na kushuhudia wafanyabiashara wakiwa wamepanga vyakula chini kinyume na taratibu huku uchafu ukiwa umezagaa pembezoni mwa barabara.

Amesema kushindwa kusimamia usafi kumesababisha manispaa hiyo kushuka katika nafasi yake ya kwanza iliyokuwa ikishikilia katika usafi kitaifa, kutoka nafasi ya kwanza hadi ya tatu.

"Nataka ndani ya siku tatu mkurugenzi ajieleze kwa nini ameshindwa kusimamia usafi, kuweka utaratibu mzuri wa masoko kiasi cha wafanyabiashara kuweka bidhaa hovyo wakati tumeshatoa maagizo siku nyingi,” amesema Mghwira.

Pia, amemtaka meya wa manispaa hiyo, Raymond Mboya kuacha kuchanganya siasa na utendaji na kubainisha kuwa usafi hauna chama.

“Hali ya usafi katika masoko yetu ni mbaya mno, cha kushangaza meya wa manispaa anawaeleza wafanyabiashara  warudishe bidhaa barabarani wakati tumeshatoa maagizo bidhaa zisionekane pembezoni mwa barabara kwani zinafanya mji kuwa na mwonekano mbaya,” amesema Mghwira.

Akizungumzia uchafu, kaimu mkurugenzi wa manispaa hiyo, Danford Kamenya  amekiri kuwepo kwa mpangilio mbovu wa soko hilo, akidai lina wafanyabiashara wengi na taka zinazalishwa nyingi.

“Katika hili soko wafanyabiashara wengi wako nje ya soko, ni takribani 800. Sasa tukisema wote waingizwe ndani soko halitoshi lakini tunaendelea kuangalia namna ya kutatua tatizo hili,” amesema Kamenya.



Chanzo: mwananchi.co.tz