Hai. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira ametoa saa 48 kwa msimamizi wa mashamba ya Kahawa ya Kibo na Kifaru,Trevo Giffod Wilayani Hai kujisalimisha mikononi mwa Polisi.
Mghwira ametoa agizo hilo leo Septemba 15 baada ya Giffod kukimbia kikao alichokiitisha Mkuu huyo kutokana na uwepo wa utata wa mwekezaji halali wa mashamba hayo.
Giffod anadaiwa kutoroka kikao alichoitisha Mghwira baada ya kukubaliana kukutana naye ili kujadili kuhusu utata wa uwekezaji wa shamba hilo.
Akizungumza na kamati ya ulinzi ya wilaya pamoja na wafanyakazi wa mashamba hayo Mghwira alisema kama mashamba hayo yanamilikiwa kihalali na Giffod, iweje akimbie mkutano huo?
Mmiliki halali wa mashamba hayo ni vyama vinne vya msingi vya ushirika ikiwamo Masama Roo, Masama Sawe, Sonu Ngira na Mudio (Mrososangi) ambavyo viliingia mkataba na mwekezaji Konrald Legg mwaka 1999.
Baada ya Legg kushindwa kuliendesha alimpa mwekezaji mwingine, ambaye ni Giffod, kinyume na mkataba.
Sambamba na mmiliki huyo kujisalimisha Polisi, Mghwira alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya kumpa taarifa halisi za nani mmiliki wa mashamba hayo.
"DC naomba nipate taarifa sahihi za nani mmiliki wa shamba hili mapema kwa sababu mmiliki huyu wa Sasa alikana kampuni hizi sio zake,hatukubali kuendeshwa Kama gari bovu nataka nione vyama hivi vya ushirika vinaona faida yake,"amesema Mghwira
Hata hivyo, uongozi wa ushirika unaomiliki mashamba hayo umedai kuwa wao wanamtambua mwekezaji Konrald Legg ambaye ni raia wa Ujerumani waliyeingia naye mkataba tangu mwaka 1999 hadi mwaka 2029 kwa kipindi cha miaka 30 ili kuendeleza kilimo cha kahawa wilayani humo.
Katibu wa mashamba hayo, Jubilathe Ndossi alikiri kuwa wanamtambua mwekezaji wa kwanza waliyeingia naye mkataba wa miaka 30 kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha kahawa.
Maliki Lema ambaye ni kibarua katika mashamba hayo amesema kuwa wao kama vibarua hawajui chochote kuhusiana na wamiliki wa mashamba hayo.
"Sisi hatuhitaji kuhoji uongozi wa mashamba haya,tunataka tupate stahiki zetu bila kubabaishwa pia hatuwezi kuhoji mabosi zetu," alisema Lema.