Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mghwira amfunda DC

40131 Pic+mgwira Mghwira amfunda DC

Tue, 5 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amempa wosia mkuu mpya wa Wilaya ya Mwanga, Thomas Apson kuwa anataka kuiona Mwanga yenye nuru ya maendeleo siyo migogoro.

Mghwira alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akimwapisha mkuu huyo wa wilaya kuchukua nafasi ya Aaron Mbogho ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais John Magufuli Januari 27.

Mbogho ameondoka katika wilaya hiyo akiwa ameacha vumbi nene la kuongoza katika kuwaweka mahabusu kwa saa 24, viongozi na watumishi wenzake wakiwamo wateule wengine wa Rais.

“Tunataka kuona mwanga na nuru ya maendeleo siyo migogoro. Mwanga isiyo na migogoro inawezekana. Kila mtu achukue hatua na kushika nafasi yake ipasavyo chini ya uongozi wako,” alisema Mghwira.

Mkuu huyo wa mkoa alimweleza mkuu huyo mpya wa wilaya kuwa wilaya anayokwenda imebarikiwa kuwa na fursa mbalimbali, ikiwamo Bwawa la Nyumba ya Mungu ambalo ni moja ya vyanzo vya mapato.

“Mwanga pia ina idadi kubwa ya mifugo ya kila aina ng’ombe, mbuzi, kondoo na punda. Mifugo hii ni sehemu muhimu sana ya uchumi wa wafugaji na wilaya,” alisema.

Alitaja fursa nyingine kuwa ni kilimo kikiwamo cha umwagiliaji, madini ya aina mbalimbali na wilaya hiyo imepakana na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi hivyo ni vyema akatumia ulinzi shirikishi.

Naye katibu wa CCM mkoani Kilimanjaro, Jonathan Mabhia aliwataka wakuu wa wilaya kutambua wanaongoza kwa kufuata misingi ya utawala bora na kueleza anavyokerwa na amri za kuwaweka watu mahabusu.



Chanzo: mwananchi.co.tz