Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgeni rasmi afariki kwa kuugua ghafla kwenye mahafali akigawa vyeti

JENEZA MK Mgeni rasmi afariki kwa kuugua ghafla kwenye mahafali akigawa vyeti

Tue, 18 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mvumi Mission, Wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma, Lucas Kaira ameelezea dakika za mwisho za Mwandishi wa habari, Frank Mbunda aliyefariki dunia baada ya kuugua ghafla akiwa katika mahafali ya kidato cha nne ya shule hiyo.

Mbunda alifariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Jumatatu ya Oktoba 17, 2022, wakati akipatiwa matibabu baada ya kuishiwa nguvu ghafla katika mahafali ya shule hiyo.

Akizungumza leo Jumanne, Oktoba 18, 2022 katika ibada ya kumuaga iliyofanyika katika Kanisa la Anglikana Parishi ya Makole, Dodoma, Kaira amesema Oktoba 15, 2022, Mbunda alikwenda kwenye mahafali hayo kama mgeni rasmi.

“Alifika kwa kuchelewa kidogo, alisema ameuheshimu mwaliko wetu ndio maana amefika lakini anachangamoto kidogo ya afya akaona ni vyema aungane nasi ili asituangushe,” amesema Kaira huku akilia hivyo kulazimika kukatisha kuzungumza mara kwa mara.

Kaira amesema aliifanya kazi iliyompeleka kwa asilimia 99 kabla ya kuishiwa nguvu na kupelekwa Hospitali ya Mvumi Mission ambapo alipata matibabu ya awali kisha kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

“Alipogawa vyeti kwa wanafunzi na kubakisha kama wanafunzi sita ama saba, nikashtuka mbona amechelewa kupokea cheti, nilipomwaangalia nikaona anataka kuanguka, nikatumia mkono mmoja kumdaka asianguke,” amesema.

Amesema baada ya hapo walimbeba hadi nje ambapo alipewa huduma ya kwanza na mganga mkuu wa Hospitali ya Mvumi Mission kabla ya kumpeleka hospitali.

Kaira amesema baadaye alirejea kuendelea na mahafali baada ya mganga mkuu kumhakikishia Mbunda alikuwa akiendelea vizuri.

Rafiki wa karibu wa Mbunda, Peter Chidawali amesema Mbunda alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.

Amesema Mbunda alipewa cheo cha Canon na Askofu wa Anglikani (hakumtaja) wa Ruvuma na alikuwa mlezi wa kwaya za kanisa la Angkani Parishi ya Makole jijini Dodoma.

Akihubiri katika ibada hiyo, Mwakilishi wa Askofu, Mchungaji Canon, Samwel Nyhinyinha amewataka watu kumuenzi Mbunda kwa kufanya matendo mema ili waweze kuacha alama duniani itakayowafanya kukumbukwa daima.

“Tuwe na la kujifunza maisha haya tutapita, mambo mema utakayotenda yatabaki. Katika nafasi zetu tulizonazo tusiache kutenda mema, kumuheshimu Mungu na wengine,” amesema.

Mwili wa Mbunda umeagwa leo jioni na kusafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika Alhamisi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live