Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgambo wa Makonda walipwa nusu ya faini za Serikali

16769 Pic+mgambo TanzaniaWeb

Tue, 11 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kiasi cha Sh346 milioni zimekusanywa ndani ya mwezi mmoja kutokana na faini walizotozwa wananchi waliokutwa na makosa kwenye operesheni ya usafi inayosimamiwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda huku nusu ya mapato hayo wakilipwa mgambo wanaoisimamia.

Kiasi hicho cha fedha kimepatikana kwenye kampeni hiyo ambayo watu 11,669 walikamatwa huku 6,667 kati yao wakipigwa faini iliyowezesha kupatikana kwa kiasi hicho cha fedha.

Akizungumza kwenye mkutano na wadau wa afya na mazingira jana, Makonda alisema lengo la kampeni hiyo halikuwa kujipatia fedha, bali kuhakikisha jiji linakuwa safi na wananchi wanatekeleza jukumu hilo bila shuruti.

“Lengo siyo kujipatia kipato wala kumshtaki mtu, bali kuwataka watu wawe wasafi. Ninawapongeza mgambo kwa kufanya kazi nzuri licha ya baadhi ya changamoto zilizojitokeza,” alisema Makonda.

Alisema nusu ya fedha zilizokusanywa katika Sh346 milioni, zimetumika kuwalipa mgambo walioshiriki kutekeleza kampeni hiyo wakishirikiana na wenyeviti, watendaji wa mitaa na kata.

“Nina imani mgambo hawa watafurahi watu waendelee kuwa wachafu kwa sababu wanajipatia ajira. Lakini siyo lengo letu Serikali, tunataka kuona jiji linakuwa safi wakati wote.”

Kati ya watu waliokamatwa kwenye kampeni hiyo, Makonda alisema 4,043 waliachiwa huru wakati 376 walidhaminiwa, sita walifikishwa mahakamani na 2,213 walipewa adhabu ya kufanya usafi.

Mgambo wanaopiga wananchi

Kuhusu mgambo wanaopiga wananchi, Makonda alisema analaani vitendo hivyo na siyo malengo ya kampeni hiyo, bali kusimamia usafi wa mkoa ili ufanane na miji mingine mikubwa duniani.

Alisema mgambo hawana mamlaka ya kumpiga raia badala yake wanatakiwa kumfikisha kwenye ofisi za serikali za mitaa.

Aliongeza kuwa watendaji wa mitaa na kata wana wajibu wa kumchukulia hatua za kisheria mgambo anayekiuka utaratibu wa kazi yake.

“Tulipopata taarifa kwamba mgambo wamewapiga wananchi kule Bunju, polisi waliwachukua wahusika na wakawafikisha mahakamani. Hawakupata dhamana, sasa wapo Segerea,” alisema mkuu huyo wa mkoa.

Wadau waibua changamoto

Katika mkutano huo, wadau nao waliibua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika kuhakikisha kwamba wanahifadhi mazingira na kurahisisha shughuli ya usafi kwa wananchi mitaani.

Khalid Singano kutoka kampuni ya usafi ya Kamoa, alisema wakandarasi wamekuwa wakicheleweshewa malipo jambo linalowafanya washindwe kutoa huduma kwa ufanisi na kulipa mishahara ya wafanyakazi kwa wakati.

“Inachukua muda mrefu mpaka kulipwa, tunakaa miezi sita mpaka mwaka bila kulipwa. Sasa nitawezaje kutoa huduma na nitalipaje mishahara ya wafanyakazi?” alihoji Singano na kuzitaka halmashauri kuwalipa wakandarasi kwa wakati.

Mwanaisha Mrutu alisema baadhi ya wenyeviti wa mitaa wanahujumu jitihada za wakandarasi kukusanya taka kwa sababu wamejitengenezea mfumo wa kujipatia fedha kutokana na ukusanyaji taka usio rasmi.

Alisema wenyeviti hao wamekuwa hawatoi ushirikiano kwa wakandarasi wakisubiri ashindwe kutoa huduma ili waendelee na miradi yao. Aliitaka Serikali kusimamia jambo hilo ili mkakati wa usafi uwe na mafanikio.

Mashine za kielektroniki (EFD)

Akielezea changamoto zilizojitokeza, Makonda alisema baadhi ya maeneo mgambo hawakuwa na mashine za kielektroniki (EFD) za kutosha hivyo kuwaagiza kila wanapotoka kwenye ofisi za watendaji wa mitaa au kata kuwa nazo ili watoe risiti papohapo kila wanapotoza faini.

Aliongeza kuwa upungufu wa watendaji wa usafi katika mitaa na kata ni changamoto kiasi cha mgambo kukosa wa kuongozana nao. Alisisitiza kuwa hakuna mgambo anayeruhusiwa kwenda kwenye nyumba ya mtu bila kuongozana na viongozi wa mtaa husika.

Wadau waja na maswali

Licha ya umuhimu wa operesheni hiyo kwa jiji la Dar es Salaam na wananchi wake, baadhi ya wadau wanaona kuna mambo kadhaa hayaendi sawa katika utekelezaji.

Katika matumizi ya fedha zilizokusanywa kutokana na faini walizotozwa waliokutwa na hatia, utaratibu unalitaka baraza la madiwani kuidhinisha matumizi ya fedha za halmashauri ikiwamo mishahara na posho za vibarua.

Kuhusu ukubwa wa malipo yaliyotolewa kwa mgambo kama ilivyobainishwa na mkuu huyo wa mkoa, meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob alisema kiwango hicho kinakiuka utaratibu wa usimamizi na uendeshaji wa halmashauri.

“Yeyote anayefanikisha kukamatwa kwa mtu anayechafua mazingira, kanuni zinasema atalipwa asilimia 20 ya faini aliyotozwa. Hii asilimia 50 sijui imetoka wapi lakini siwezi kuingilia masilahi ya watu,” alisema Jacob.

Hata mafanikio yaliyopatikana, meya huyo alisema si ya kujivunia kwa sababu wengi waliotozwa faini hizo ni wafanyabiashara wadogo wakiwamo mamalishe, wamachinga pamoja na wananchi wanaoishi Uswahilini.

“Hizi hela zimekusanywa zaidi Temeke, Manzese, Tandale na maeneo mengine ya Uswahilini ambako hakuna miundombinu ya usafi. Huwezi kupeleka mgambo Masaki au Oysterbay. Nilishawazuia mgambo mara kadhaa kwenye Halmashauri ya Ubungo,” alisema.

Mkurugenzi wa jiji

Mkurugenzi wa jiji hilo, Spora Liana alisema operesheni hiyo ilikuwa ni ubunifu wa mkuu wa mkoa mwenyewe ambaye ndiye anayeisimamia ingawa matumizi ya fedha zitokanazo na faini pamoja na vyanzo vingine vya mapato hupangwa na halmashauri.

“Wakati anaanzisha alisema mgambo watalipwa kutokana na fedha zitakazopatikana. Sifahamu kulikuwa na utaratibu gani wa kuidhinisha malipo hayo, watafute wakurugenzi wa halmashauri huenda watakuwa wanajua,” alisema Liana.

Ukiacha changamoto chache zilizojitokeza, wapo wanaopongeza ubunifu ulioonyeshwa na Makonda.

Mwanasiasa na mtafiti, Julius Mtatiro alisema Serikali ielekeze nguvu kubwa kutoa elimu kwa sababu Dar es Salaam ni mkoa unaokutanisha watu wenye tamaduni na ustaarabu tofauti.

Alisema kila mwananchi akipewa elimu ya usafi atafahamu athari za uchafuzi wa mazingira na kutambua wajibu wake kuhakikisha unakuwa na mazingira safi.

“Usimamizi lazimishi ninauunga mkono, nimependa wazo la kutumia mgambo kusimamia usafi. Jambo hili linapaswa kuendelea lakini mgambo waelimishwe kwamba hawatakiwi kupiga watu,” alisema Mtatiro.

Tofauti na Mtatiro, mwanasheria mkongwe na mtetezi wa haki za binadamu, Dk Hellen Kijo Bisimba alisema matumizi ya fedha zilizotokana na faini hizo yanatia shaka.

Alisema kama kila mtumishi wa umma angekuwa analipwa nusu ya mapato ya Serikali anayokusanya, askari wa usalama barabarani na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wangekuwa matajiri wa kutupwa.

“Upo utaratibu wa kuwalipa mgambo kwa kazi yoyote wanayoifanya. Siamini kama fedha zote hizo zimetumika kuwalipa askari hao,” alisema Dk Bisimba.

Usimamizi wa operesheni hiyo alisema haukupaswa kuwahusisha mgambo kwa kuwa kila kila kata na wilaya zina maofisa afya wenye jukumu hili.

“Lakini sishangai kila kitu kinachofanywa Dar hasa na Makonda kimepinda. Yeye anapaswa kusimamia sheria za usimamizi na uendeshaji wa halmashauri, lakini anazikiuka. Upo utaratibu wa kutumia fedha za Serikali siyo kiholelaholela tu.”

Chanzo: mwananchi.co.tz