Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfungwa aliyetoka kwa msamaha wa Rais Magufuli adakwa na kuku wa wizi

90277 Wizi+pic Mfungwa aliyetoka kwa msamaha wa Rais Magufuli adakwa na kuku wa wizi

Mon, 30 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serengeti. Jasiri haachi asili ndivyo unaweza kusema kuhusiana na tukio la kukamatwa kwa Chacha Mwikwabe (26) kwa wizi wa kuku zikiwa zimepita siku 20 tangu alipoachiwa kutoka gerezani kwa msamaha wa Rais Dk John Magufuli.

Mwikwabe mkazi wa Mtaa wa MCH Mugumu, amekamatwa leo Jumapili Desemba 29, 2019 saa 12.30 asubuhi mtaa wa Kanisani Matare akiwa ameiba kuku wawili na kuuza mmoja, akidai kuwa ni kutokana na  ugumu wa maisha.

Mwikwabe ambaye anatembea na karatasi ya kuachiwa kutoka gerezani kwa makosa ya uwindaji, alihukumiwa kifungo cha miaka miwili na ametumikia mwaka mmoja na miezi mitatu. Anasema kuiba kuku aliona ndiyo njia rahisi ya kupata fedha .

“Ugumu wa maisha ndiyo umenifanya niibe, nimeiba kuku mmoja tu si wawili maana mmoja ameniponyoka, nikawa nimeuza kwa Sh12,000 ,” amekiri.

Huku akizungumza kwa sauti ya chini amesema kuku huyo amemwiba kwenye banda la Mwalimu wa Shule ya Msingi Matare, Yusuph Nyaikobe.

“Mimi nimeiba leo tu jana wale kuku wa mwalimu wa Mugumu wananisingizia tu, yote haya ni ugumu wa maisha unachangia maana nyumbani hakuna kitu,” amesema.

Akisimulia namna alivyoibiwa kuku huyo, Mwalimu Nyaikobe amesema leo asubuhi alitoka nyumbani kwake na kwenda shuleni kuangalia wizi wa mahindi mabichi shambani, ndipo akakutana na mtuhumiwa akitokea katikati ya shamba la mahindi akiwa amemshikilia kuku huyo.

“Aliniwahi kwa salamu oyaa vipi, nikasema safi, nikamuuliza mbona unaibukia shambani mwangu na kuku alfajiri hii, akasema ameuziwa na mwalimu, alikuwa na kuku wawili, alipoona namwangalia akadai ina maana huniamini, nikamwacha aende,” amesema.

Hata hivyo baada ya kumuuliza binti wa mwalimu mkuu ambaye yuko safari akakana, kuangalia akakuta jogoo hayupo wakaamua kumsaka na kumnasa akimaliza kuuza kwa Shilingi 12,000.

Mwenyekiti wa mtaa, Abeid Israel amesema mtuhumiwa anaonekana mzoefu kwa kuwa anajua muda wa kufungulia kuku na wapi wanakimbilia na yeye kuwanasa kwa urahisi.

“Anakoishi na hapa alipokutwa muda huo ni zaidi ya kilometa sita,” amesema.

Mkuu wa Wilaya, Nurdin Babu amesema kitendo hicho kinaonyesha wazi kuwa msamaha wa Rais aliotoa Desemba 9 kwa wafungwa 5,533 nchi nzima na wilayani hapo wafungwa zaidi ya 100 waliachiwa haukuwa na maana kwa mtu kama huyo na kuwataka watafute kazi nyingine kwa kuwa serikali haijalala.

Chanzo: mwananchi.co.tz