Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfungwa aliyegeukia utunzi wa vitabu akiwa gerezani

Vitabu Jela.png Mfungwa aliyegeukia utunzi wa vitabu akiwa gerezani

Tue, 26 Sep 2023 Chanzo: mwanachidigital

“Nikiwa gerezani mwaka 2014 nilipokea ujumbe kutoka kwa mtoto wangu ulionisukuma kuanza utunzi wa vitabu kama njia ya kuingiza kipato kumsaidia,’’

Hiyo ni sehemu ya simulizi ya Majid Gao (46), mtunzi wa vitabu na mashairi.

Anasema akiwa gerezani kutumikia kifungo cha miaka 30 baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la ubakaji, siku moja alitembelewa na mmoja wa marafiki zake aliyempelekea ujumbe kutoka kwa mtoto wake (jina linahifadhiwa kumlinda), ambao siyo tu ulimsononesha, bali ulimpa mwanga wa kuanza kujishughulisha na kazi itakayomwingizia kipato cha kuisaidia familia yake.

‘’Mtoto wangu alinitumia salamu kupitia kwa mtu mmoja aliyekuwa anakuja gerezani kunitembelea…ile salaam ilikuwa na ujumbe ulioniumiza sana lakini namshukuru Mungu kwamba leo ule ujumbe umeniwezesha kuwa miongoni mwa watunzi wa vitabu na mashahiri,’’ anasema.

Anasema katika ujumbe huo, mtoto wake alimweleza hamu ya kumtembelea gerezani, lakini anashindwa kufanya hivyo kwa sababu hana nauli.

‘’Mwambie baba kuwa natamani kumtembelea lakini sina nauli ya kunifikisha huko alipo….pia mwambie ajitahidi kutafuta namna ya kunisaidia nifahamu asili yangu, ndugu zangu na eneo walipo,’’ anasema Gao akinukuu moja ya ujumbe kutoka kwa mwanaye uliomfanya aanza utunzi wa vitabu

Chanzo cha kufungwa

“Mwaka 2003 nilirudi nyumbani Rorya kwa ajili ya kwenda kulima, nilianza kulima bustani kisha nikapanda miwa heka sita, lakini nikashtakiwa kwa uvamizi wa ardhi,” anasimulia Gao.

Anasema baada ya shauri hilo kumalizika, wahusika hawakuacha kumfuatafuta ndipo siku moja alijikuta akitiwa mbaroni na kufunguliwa mashtaka ya kujeruhi ambayo baadaye yalibadilishwa kuwa ya ubakaji.

‘’Kesi ile iliisha kwa mimi kutiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela katika Gereza la Butimba jijini Mwanza,’’ anasema Gao.

Anasema wakati anafungwa alimuacha mke na mtoto mwenye umri wa miaka tisa, ambaye ilibidi akalelewe na bibi yake baada ya mama yake kuolewa na mwanaume mwingine.

Anasema baada ya muda mfupi, bibi aliyekuwa akiwalea watoto wake alifariki dunia na hivyo jukumu la malezi ya familia likasalia mikononi mwa mtoto wake mwenye umri wa miaka tisa, ambaye alimtumia ujumbe uliomfanya kugeukia utunzi wa vitabu kama njia ya kuingiza kipato cha kuisaidia familia yake akiwa gerezani.

Wazo la utunzi

“Baada ya kufikiria kwa muda namna ya kuisaidia familia yangu, niliijiwa na wazo la kuandika mashairi na vitabu. Nilikwenda kumpa wazo hilo ofisa mapokezi. Kwanza alinishangaa na kunihoji iwapo kweli naweza.

Anasema baada ya kueleza kwa kina nia na uwezo wake wa kuandika, ofisa huyo alimkubalia kwa sharti kwamba kila anachokiandika lazima kikaguliwe na kisainiwe na uongozi wa gereza kabla ya kukabidhiwa kwa mtu atakayemsaidia kwenda kukichapisha.

‘’Yule ofisa aliniruhusu pia machapisho yangu yasomwe na wafungwa wenzangu na jamii nzima ya gereza kabla ya kuchapishwa ili niweze kufanya masahihisho. Hii ilinisaidia sana katika utunzi wangu,’’ anasema Gao.

Upatikanaji wa vifaa

Baada ya ruhusa hiyo, Gao anasema alikumbana na kikwazo cha kukosa vifaa vya kumwezesha kufikia ndoto yake, ikabidi aanzishe utaratibu wa kupunguza kiwango cha chakula katika mgawo wake ili apate sehemu ya kugawa kwa wafungwa wenzake kwa kubadilishana kwa kipande cha sabuni au fedha.

Anasema baada ya muda mfupi alipata fedha za kununulia kalamu na madaftari ya kuandikia mashairi na kuanza kuandika kitabu cha kwanza kikiwa na kichwa cha habari kinachosema ‘Binadamu kumbe ndivyo mlivyo’ ikiwa ni simulizi ya mtoto aliyeishi kwa shida baada ya kutelekezwa na mama yake.

“Niliandika kitabu hiki nikiwa na fikra kuhusu maisha ya mtoto asiye na mtu wa kumsaidia. Kiukweli kichwani nilikuwa na picha ya jinsi mtoto wangu anavyoishi baada ya mama yake kuondoka na kwenda kuolewa na mtu mwingine,’’ anasema.

Anasema baada ya muda kupita, alihamishwa kutoka gereza la Butimba kwenda Gereza la kilimo Songea ambako ratiba ya kuamka, kazi za kutwa nzima na kulala ilimpa wakati mgumu kupata muda wa utunzi.

‘’Baada ya kuzoea mazingira, nilianza tena kazi ya kutunga vitabu kwa kutenga muda maalumu wa shughuli hiyo bila kuathiri majukumu yangu kama mfungwa,’’ anasema.

Kwa kupanga muda wake vizuri na kwa ushirikiano mkubwa alioupata kutoka kwa viongozi wa magereza yote mawili ya Butimba na Songea, Gao alifanikiwa kuandika vitabu 81, vitatu akiwa Gereza la Songea na vingine 78 akiwa Gereza la Butimba mkoani Mwanza.

Msamaha wa Rais

Anasema mwaka 2021 hatausahau maishani mwake kwa sababu alipata msamaha wa Rais na kutoka gerezani, baada ya kutumikia zaidi ya miaka 16 ya kifungo chake cha miaka 30.

“Kitendo cha kutoka gerezani kiliniongezea ari na muda zaidi wa kutunga vitabu, safari hii nikigeukia simulizi ya maisha yangu ya jela. Nimetunga vitabu viwili kimoja kikiwa na kichwa cha habari kinachosema 'kweli yamenikuta kama yaliyomkuta mbwa’' na kingine kikiwa na kichwa kinachosema 'Haki ya mnyonge maumivu’'.

Ushauri kwa wanaofanya makosa

“Gerezani kubaya, mtu usiombe kwenda, utakwenda huko utateseka ujute ili ukirudi uraiani usimulie wengine wenye tabia kama za kwako na ndio maana unapohukumiwa mahakamani wanasema iwe fundisho kwa watu wengine maana yake huko unapokwenda ukakome,”anasema.

Mtoto wake na maisha yake ya sasa

Gao baada ya kutoka gerezani alifanikiwa kuoa mwanamke mwingine na kufanikiwa kupata mtoto mwingine wa pili. “Mtoto niliyemuacha wakati naenda gerezani sasa hivi kafikisha miaka 28 na ana familia yake, nawasiliana naye kwa simu na kuonana naye mara kwa mara japo kwa sasa anafanya biashara ndogondogo mkoani Mbeya,”anasema.

Anasema licha ya kuwa na uwezo wa utunzi lakini kinachomkwamisha ni gharama za uchapishaji na kujikuta akichapisha kitabu kimoja baada ya kupata msaada kutoka kwa mmoja wa watu waliovutiwa na kazi zake.

“Ukosefu wa fedha unafanya fani na juhudi zangu ziishie ndani, nilifanikiwa kuchapa kitabu kimoja na baada ya kuuza kopi fedha niliyopata niliitumia kutokana na ugumu wa maisha.

“Ombi langu kwa mtu au taasisi yoyote ambayo inaweza kuniwezesha kifedha inisaidie kuchapisha vitabu vyangu ili niweze kutimiza ndoto yangu na kujikimu kimaisha,”anasema.

Chanzo: mwanachidigital