Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfanyakazi wa TSN afariki dunia

6d2c970edeb8d5659a57e07ce4c93bfe Mfanyakazi wa TSN afariki dunia

Wed, 3 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MFANYAKAZI wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) Idara ya Habari Kitengo cha Msanifu Kurasa, Anneth Solomon Urio (52), amefariki dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Tumbi wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Kwa mujibu wa Ofisa Rasilimali Watu Mkuu wa TSN, Joyce Macha, Anneth alikumbwa na mauti akiwa amelazwa katika hospitali hiyo kwa matibabu.

“Maandalizi ya shughuli yote ya msiba yanafanyika leo (jana) jioni Mwenge lakini tayari familia yake imesema wanatarajia kusafirisha mwili kwenda Moshi eneo la Mwika Jumatatu au Jumanne kwa ajili ya mazishi,” alisema Macha na kuongeza kuwa taratibu za ndugu, jamaa na marafiki kuuaga mwili jijini Dar es Salaam zitatolewa leo.

Macha alieleza kuwa Anneth alijiunga na TSN inayochapisha magazeti ya Daily News, HabariLEO na SpotiLeo mwaka 2007 akiwa kama Msanifu Kurasa wa gazeti la HabariLEO hadi mauti yanakumta.

Anneth alizaliwa Aprili 25, 1969 katika Kijiji cha Mwika mkoani Kilimanjaro, alisoma Shule ya Msingi Kifungilo kuanzia mwaka 1960 hadi 1982 na kujiunga na Shule ya Sekondari Kifungilo Girls kuanzia mwaka 1983 hadi 1986.

Aidha, mwaka 1987 alijiunga kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Jangwani jijini Dar es Salaam hadi mwaka 1989 na kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kambi ya Maramba mkoani Tanga mwaka 1989 hadi 1990.

Lakini pia katika uhai wake alifanya kazi katika Kampuni ya Printpak Tanzania Limited akiwa Msanifu Kurasa wa magazeti, vitabu, majarida na vipeperushi. Pia alifanya kazi katika Kampuni ya Guardian Limited akiwa Msanifu Kurasa wa magazeti ya Guardian, Nipashe na Alasiri.

Aidha, kabla ya kujiunga na TSN, Anneth aliajiriwa na kufanya kazi katika Kampuni ya Habari Corporation Limited akisanifu kurasa za magazeti ya Mtanzania, Rai, Bingwa na Dimba.

Anneth alijaliwa kupata watoto wawili wa kiume, Oscar na Obrien Kigeso.

Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amen.

Chanzo: habarileo.co.tz