Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfanyabiashara Moshi apandishwa kortini kwa ubadhirifu wa milioni 27 za uchaguzi

11942 Pic+kortini TanzaniaWeb

Tue, 14 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Watu wawili akiwamo Mfanyabiashara wa mjini Moshi, Oscar Kigumu, wamefikishwa kortini leo Agosti 14, 2018 wilayanj Hai kwa tuhuma za ubadhirifu wa Sh27.6 milioni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Mfanyabiashara huyo anayemiliki kampuni ya Oscar Food and Beverage Catering Services, ameshitakiwa pamoja na mkuu wa kitengo cha uchaguzi wa Halmashauri ya Hai, Edward Ntakiliho.

Katika kesi hiyo, washitakiwa hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya ya Hai, Devotha Msofe, na kusomewa mashitaka yao na mwendesha mashitaka wa Takukuru, Rehema Mteta.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Takukuru mkoa Kilimanjaro, Holle Makungu jioni hii, imesema washitakiwa wote walikana mashitaka yao na kesi yao itatajwa Septemba 5, 2018 na upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

 

Mashtaka ya mfanyabiashara huyo ni mawili, moja likiwa ni la kugushi nyaraka kuonyesha kwamba kampuni yake ilipokea Sh20.3 milioni kutoka kwa Ntakiliho aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi.

Katika nyaraka hizo za kughushi, Mfanyabiashara huyo anadaiwa kudai yalikuwa ni malipo ya chakula na vinywaji kwa ajili ya mafunzo ya wasimamizi wa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2015.

Mwendesha mashitaka huyo wa Takukuru amedai katika shtaka la pili kuwa, mfanyabiashara huyo alimsaidia Mshitakiwa mwenzake kufanya ubadhirifu wa Sh1.49 milioni.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mshitakiwa Ntakiliho anashitakiwa kwa makosa manne, huku makosa matatu yakiwa ni ya kugushi nyaraka na moja la ubadhirifu wa fedha za umma alizokabidhiwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz