Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfalme Zumaridi afunguka kilichomkuta gerezani, augua gonjwa zito!

Zumaridi Tyu Mfalme Zumaridi afunguka kilichomkuta gerezani, augua gonjwa zito!

Sun, 19 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mhubiri, Diana Bundala maarufu "Mfalme Zumaridi" amefunguka magumu aliyopitia akiwa gerezani kuwa ni pamoja na kuugua ugonjwa wa shinikizo la damu 'presha' ambao hakuwa nao, huku akitengwa na baadhi ya wafungwa wenzake.

Zumaridi ametoa kauli hiyo leo nyumbani kwake baada ya kumaliza kifungo chake cha mwaka mmoja katika Gereza la Butimba jijini Mwanza baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza kumtia hatiani katika shtaka la kuzuia maofisa wa serikali kutekeleza majukumu yao.

Amesema hatasahau miezi 10 ya mwanzo kati ya 11 aliyokaa ndani ya gereza hilo tangu alipokamatwa kutokana na baadhi ya wafungwa kumtenga jambo lililomnyima amani ndani ya gereza hilo.

"Maisha ya gerezani ni changamoto kwa sababu unakuwa chini ya ulinzi, sikuwa na amani yoyote. Niliishi kwa mateso mpaka nimepata presha, nilikuwa kawaida lakini baada ya kuingia gerezani nimepatwa ugonjwa huo," amesema.

"Nilitengwa na watu wote, wafungwa wenzangu na watu wangu niliyoingia nao gerezani walizuiwa kunisogelea, mule ndani ya gereza la wanawake kuna mwembe niliambiwa nikae kwenye mwembe peke yangu kwa hiyo sikuwa na sehemu ya kukimbilia," ameongeza

Mhubiri huyo amesema alianza kupata amani Oktoba mwaka jana baada ya uongozi wa gereza hilo kubadilishwa, ambapo mkuu wa gereza hilo aliletwa mpya ambaye alikuwa akisikiliza kero na maoni ya wafungwa katika gereza hilo.

Ameiomba serikali na Rais Samia Suluhu Hassan kufanya ufuatiliaji wa kina ndani ya magereza nchini ili kubaini madhaifu yaliyomo na kuepusha ukiukwaji wa haki za wafungwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live