Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfahamu Lea, mwanamke kondakta kwa miaka 30

Lea Pic Mfahamu Lea, mwanamke kondakta kwa miaka 30

Mon, 21 Aug 2023 Chanzo: mwanachidigital

“Wee bibi, nenda kalee wajukuu.” Hayo ndiyo maneno anayokutana Lea Ntunda akiwa kwenye kazi yake ya utingo wa daladala inayofanya safari Mwananyamala-Buza jijini Dar es Salaam.

Ukimtazama ni mama wa makamo, ambaye huwezi ukadhani anaweza kudandia na kushuka kwa kuruka kwenye gari kama wafanyavyo utingo vijana wakiwa katika kazi hiyo.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Lea anasema alianza kazi ya utingo tangu nauli ya daladala ikiwa Sh5, jijini Dar es Salaam kwenye gari zilizojulikana kama chai maharage.

Anasema alipata kazi hiyo baada ya kuchoka kukaa kwa dada yake bila kazi kwa muda mrefu.

Lea anasema dada yake huyo alimchukua kutoka kijijini kwao Singida kwa lengo la kumsaidia malezi ya watoto wake.

“Nakumbuka nilikuja Dar es Salaam nikiwa bado msichana kabisa, ziwa kwenzi na nilikuwa nimeishia darasa la nne.

“Baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kazi nikaona kwa nini nami nisitafutie kazi itakayoniingizia chochote kitu, ndipo hapo nikaingia kwenye kazi hii ya daladala nikiwa wakati huo nina miaka 20 na mpaka leo bado naifanya kazi hii ambayo nauli ni Sh500,” anasema Lea.

Anasema katika kipindi chote hicho ameshafanya kazi katika njia zote za daladala katika jiji hilo na kubainisha kuwa licha ya kuwa ni kazi aliyokuwa anajitafutia kipato, lakini pia aliipenda kutoka moyoni.

Lea anakiri kwamba umri wake sasa ulipofika anahitaji kustaafu kazi hiyo kwa kuwa amekuwa akichoka sana ikilinganishwa na enzi za ujana wake.

“Wakati nikiwa bado nina nguvu zangu nilikuwa nikitoa gari saa kumi alfajiri na kulirudisha saa nne usiku, lakini kwa sasa natoa gari saa moja asubuhi nalirudisha saa tatu,” anasema Lea.

Hata hivyo, anasema ameweza kusimama kiafya katika kazi hiyo hadi leo kwa kuwa pia anazingatia sana suala la kula yake kwa kuzingatia mlo ulio kamili.

Leo, mwenye mtoto wa darasa la sita, anasema wakati mwingine huwa anazunguka na mtoto wake kwenye daladala siku za mapumziko akiwa haendi shule.

Hata hivyo, anasema kitu ambacho hawezi kusahau ni kipindi alichokusanya pesa yake ya kununua kiwanja na mwisho wa siku mumewe alimwibia ambaye wameachana kwa sasa.

Changamoto

Moja ya changamoto anayokutana nayo Lea katika kazi yake hiyo ni watu kumuita bibi na wengine kumtaka aache kazi hiyo na kwenda kulea wajukuu.

“Kauli hizi za kuniita bibi, sipendi na hata nikiwakataza bado baadhi wanaendelea kuniita, ningependa zaidi waniite kwa jina langu,” anasema.

“Lakini jingine ni jamii kuona kuwa mwanamke akiwa katika umri wangu hapaswi kuifanya kazi hii, wakati kuna wanaume wana umri mkubwa kuliko mimi wapo huku kwenye magari, mbona siwasikii wakiwaambia wee babu nenda kalee wajukuu, waache mfume dume na dhana potofu juu ya mwanamke.”

Akielezea changamoto nyingine katika kazi yake hiyo, Lea anasema ni pamoja na kuyaoga matusi kutoka kwa abiria kwa kuwa baadhi yao wakiwa wameudhiwa nyumbani hasira wanazishushia kwao, hasa nyakati za asubuhi watu wanapoelekea katika maeneo yao ya kutafuta riziki.

Changamoto nyingine anasema ni kutolipwa nauli mwisho wa safari ya abiria, jambo linalowafanya kuwa na mabishano kati yao na wakati mwingine kuamua kusamehe ili kuepuka kupoteza muda.

Wakati matukio ya kuibiwa kwenye daladala yakidhaniwa ni kwa abiria tu, Lea anasema hata utingo wanakumbana na matukio hayo.

“Kama ushawahi kuwachunguza utingo wengi utakuta wamevaa hata suruali tatu hadi nne, hii yote ni katika kujilinda na vibaka ambao wamekuwa wakituibia,” anasema Lea.

“Hawa hupanda kwenye daladala kama abiria na nauli wanakulipa, ila wakishafanikisha lao wanashuka kituo chochote, hivyo abiria nao waelewe pia hata sisi huwa tunapigwa.”

Utingo kuwajua vibaka

Kuhusu madai kuwa utingo huwa wakiwajua vibaka wanaopanda kuwaibia abiri na kugawana nao hela au watakachofanikiwa kuiba, Lea anakiri kuwa hilo lipo kwa baadhi yao.

Anasema kuna wengine hawapendi kuyaona hayo, wakijaribu kuwasema huwa wanawatisha kwa silaha za ncha kali wanazokuwa wamezibeba, ikiwamo kisu na bisibisi.

Hata hivyo, Lea anasema kwa upande wake akishawagundua huwa anamuamuru dereva kusimamisha gari na kumshusha, kwa kuwa anajua uchungu wa kuibiwa, hivyo hayuko tayari kuona abiria wake wakiwa wamepanda gari kwa amani na kushuka kwa huzuni kutokana na vitendo hivyo.

Upatikanaji wa mapato

Jingine anasema upatikanaji wa hela sasa hivi kwenye daladala umekuwa mgumu ukilinganisha na kipindi cha nyuma, huku akibainisha kuwa imechangiwa na ujio wa aina nyingine za usafiri, ikiwamo bajaji na bodaboda kwa kuwa abiria anaamua apande usafiri upi.

“Enzi usafiri huu mwingine haujaja (bajaji na bodaboda), ilikuwa mtu unaweza kulaza chini Sh60,000 (kipato cha siku) hapo ushampa bosi wako hela yake, lakini sasa hivi umepata sana Sh30,000 kwa siku,” anasema Lea.

Pia, anawataja wapiga debe kuwa kero, na kueleza kuwa wengine wanachangiwa uwepo wao na utingo na madereva wenyewe, lakini kwake kutokana na msimamo wa kutowatumia huwa hawasogelei gari lake.

Anasema wapiga debe ni miongoni mwa wanaowafanya wasitimize hesabu za mabosi zao, kwa kuwa unaweza kujikuta unatumia sio chini ya Sh5,000 kwa siku kwa ajili yao, lakini baadhi wamekuwa wakiwaibia abiria.

Katika hili anashauri Serikali pia kuwasimamia, kwa kuwa hawajawa tisho kwao tu, bali na kwa abiria na kama wanaona kuna ulazima wa kuwepo basi wawatambue rasmi kwa kuwa na sare na vitambulisho maalumu.

Leo anasema hilo linasaidia kutakapotokea jambo lolote baya iwe rahisi kuwatambua.

Vipi kuhusu mafanikio?

Lea ambaye watoto wake wawili walitangulia mbele ya haki, anasema licha ya kufanya kazi kwa muda mrefu hajapata mafanikio makubwa zaidi ya pesa ya kumsomesha mwanaye, kulipa kodi na kujikimu na hali ngumu ya maisha.

Tofauti ya utingo wa zamani, sasa

Akielezea kwa namna anavyowaona utingo wa sasa hivi ukilinganisha na wa enzi zao, Lea anasema wa sasa wengi sio waaminifu, wamekuwa wakikimbia na fedha.

Anasema unakuta unamchukua mtu unakaa naye siku tatu, baada ya hapo anaingia mitini na hesabu zote za siku na mwingine anaweza akudanganye naenda kula, basi ndio kimoja (harudi).

“Pia, wamekuwa hawawaheshimu abiria na mabosi wanaowapa magari, hivyo kujikuta wanaingia katika migogoro na mwisho wa siku kufukuzwa kazi,” anasema Leo.

Anasema hilo kwake na dereva wake ni tofauti kwa kuwa amefanya kazi kwa bosi mmoja tangu ameanza kazi, jambo linalozidi kumjengea uaminifu kwake hata siku akikosa hela anamuelewa.

Dereva anayefanya naye kazi afunguka

Dereva aliyejitambulisha kwa jina la Iddi Rajab, anayefaya kazi na Lea, anasema amefanya kazi na utingo huyo muda mrefu. Jambo analolifurahia kwa mama huyo wa mtoto mmoja, anasema wanasikilizana kwa kuwa utingo wengine hata pale unapowaelekeza wanakuona kama unaongea sana.

Pia, anasema anapenda namna Lea anavyojiamini, kwa kuwa wapo waliomzushia kuwa anatoka naye kimapenzi, lakini anapotezea, na ilifika mahali hata mke wake alishakwenda kumfanyia vurugu lakini kamwe hilo halijamrudisha nyuma.

Rajab anasema mbali ya kuwa utingo, pia ni dereva mzuri, sema tu kazi hiyo hajaitilia maanani, ikiwamo kwenda kusomea na kupata leseni. “Katika ushauri wangu tuwaamini wanawake, kwa kuwa kadiri siku zinavyozidi kwenda wamekuwa wakifanya kazi nyingi tulizodhani ni za wanaume tu,” anasema Rajab.

“Hivyo tuwape moyo badala ya kuwakatisha tamaa, kwa kuwa hata abiria huwa wananiuliza kuwa huyu ni mke wako, bila kusahau hata kwenye ofisi nyingine wanafanya kazi watu mchanganyiko.”

Abiria, majirani wamzungumzia

Baadhi ya abiria wakimzungumzia Lea, wanasema mama huyo amekuwa kivutio kila wanapomuona, hasa anapofanya kazi zake kama ni kijana vile wa miaka 25.

Monica James anasema kupitia Lea, wanawake wengine wa umri wao wanatakiwa kujifunza, ikiwamo kuona umri mkubwa ndio mwisho wa kujishughulisha hadi wengine kwenda kuomba kwenye maduka ya wafanyabiashara mjini.

Nurdin Lubaya, anasema bosi wake anatakiwa amfanyie jambo mama huyo, ikiwamo hata kumkabidhi gari ili iwe motisha kwa wafanyakazi wake wengine kufanya kazi katika uaminifu kama alivyo Lea na kwa muda mrefu.

Bertha Urio ambaye ni jirani wa Lea anasema wamekuwa wakiishi na mama huyo vizuri; kutokana na kazi zake za kutoka na kurudi usiku, wamekuwa pia wakimwangalizia mtoto wake.

“Kikubwa anachofanya ni kuacha hela, kwa kuwa ni mtoto anayeweza kujifanyia kila kitu mwenyewe na sisi tumekuwa tukimsaidia kumwangalizia mpaka muda anaorudi,”anasema Bertha.

Chanzo: mwanachidigital