Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Meya Mwanza adai uzazi wa mpango utapunguza watoto wa mataani

651d2e96c244b826ff775b243fd255dd Meya Mwanza adai uzazi wa mpango utapunguza watoto wa mataani

Thu, 28 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MSTAHIKI Meya wa Jiji la Mwanza, Constantine Sima ametoa wito kwa jamii kuendelea kuzingatia ushauri wa wataalamu juu ya elimu ya uzazi na uzazi wa mpango ili kusaidia kupunguza mimba zisizotarajiwa zinazopelekea ongezeko la watoto wa mitaani kwa kiasi kikubwa.

Sima alitoa wito huo wiki iliyopita alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika mahojiano maalumu kuelezea mikakati iliyowekwa na ofisi yake kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani jiini Mwanza.

Alisema kupitia idara za afya ngazi ya kata na halmashauri jijini hapa zimekuwepo semina na warsha mbalimbali zinazotolewa mitaani ambapo wataalamu wa afya wamekuwa wakipita kutoa elimu ya uzazi wa pango ili kukabiliana na mimba zisizotarajiwa ambazo zinachangia ongezeko la watoto wa mitaani.

"Imefika muda sasa kwa kila mmoja wetu ndani ya jamii, kuanza kutilia mkazo elimu ya uzazi inayotolewa hususani ngazi ya mtaa ambako ndiyo chimbuko la watoto na wananchi wengi, na tunajua mipango hii imekuwa ikihamasishwa kwa muda sasa, lakini inabidi twende kwenye awamu nyingine ya kampeni hii kufikia malengo.

"Suala la ongezeko la watoto wa mitaani ni suala lenye taswira tofauti ndani ya jamii, kupitia kamati za maendeleo za kata maafisa jamii wa maeneo yetu wamekiri kushuhudua sababu ya malezi duni ya wazazi ikiwa chanzo kikubwa kwani siyo wote walio mtaani hawana wazazi,"

"Na pia tumebaini siyo wote hawana makwao, kwa maana ya sehemu za kuishi bali yamekuwepo malezi duni hususani ya wazazi kutumia muda mwingi kwenye kazi na kutotenga muda wa kukaa na watoto na kupelekea unyanyasaji wa watoto na kusababisha baadhi ya watoto kukimbilia mtaani," alisema Sima.

Alisema kama kiongozi wa jiji la Mwanza anatarajia kuona elimu inayotolewa mtaani inaongeza mwamko wa wazazi kukabili mimba za utotoni, mimba zisizotarajiwa na wazazi kujali malezi ya watoto wao ili kufikia adhima ya kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani.

Aidha meya aliiomba jamiii kushiriki utoaji taarifa za watuhumiwa wanaowapa mimba wanafunzi kwenye ofisi za waratibu wa kata ili kupiga vita mimba za utotoni hususani kwa wanafunzi ambazo zimeendelea kuwepo siku hadi siku hasa maeneo ya mijini.

Chanzo: habarileo.co.tz