Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Meya Kinondoni awatoa hofu wakazi wa Mpigi

58872 Pic+meya

Wed, 22 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Meya wa Kinondoni Benjamin Sitta amewatoa hofu wakazi wa Mpigi wanaoishi mpakani mwa wilaya hiyo na Bagamoyo ambao nyumba zao zipo hatarini kubomoka kutokana na uchimbaji holela wa mchanga unaofanyika kwenye  kingo za daraja la Mpigi .

Uchimbaji huo wa mchanga kwenye kingo za mto unasababisha maji kuchepuka katika njia yake kwenda kwenye makazi ya watu hasa kipindi cha mafuriko na kusababisha madhara kwa wananchi hao.

Sitta ambaye ni diwani wa Msasani alieleza hayo juzi wakati alipofanya ziara ya kutembelea eneo hilo kisha kuzungumza na wananchi waliomweleza madhara na adha wanayoipata kutokana na uchimbaji huo wa mchanga.

Bila kumtaja mkandarasi huyo, Sitta alisema ameshapatikana atakayefanya kazi ya kurekebisha mto huo ili maji yanayotiririka yapite kwenye njia yake badala ya kuchepuka kwenda kwa wananchi na kusababisha madhara hasa wakati wa mvua.

“Niwatoe wasiwasi tukishirikiana na watu wa bonde ambao wametuhakikishia mkandarasi ameshapatikana atakayejikita kusafisha mto, kurekebisha kina na kingo za  mto huu. Mchakato huu ukikamilika tutawaokoa wananchi wetu wa pande zote mbili na lile daraja linalotenganisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Awali , wakazi wa eneo hilo walimweleza Sitta uchimbaji huo wa mchanga ndio chanzo kikubwa kwa makazi yao kuwa katika wakati mgumu na kwamba mwanzoni walikuwa mbali na mto huo lakini hivi sasa wanaukaribia kutokana na kingo hizo kuharibiwa.

Pia Soma

“Tulikuwa mbali na mto huu, nje ya mita sitini na tulikuwa sahihi  kuishi lakini sasa mto unatufuata kwenye makazi yetu. Watu karibu 50.

“Nimeishi hapa tangu mwaka 2010 kulikuwa na mto mdogo unaopitisha maji, lakini wachimba mchanga wanatutesa sana. Wanachimba kwenye kingo wanasema ndiko kuna mchanga mzuri wa plasta unaotumika kuchapia nyumba,” alisema Esther Maluku kwa niaba ya wenzake.

Alisema siku za nyuma walifanikiwa kwenda hadi ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kinondoni, kwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam (Paul Makonda), hadi ofisi ya mkuu wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo aliyewaahidi kulifuatilia suala hilo.

Katika juhudi za kwenda katika ofisi mbalimbali za umma, Maluku alisema Serikali iliamua kuweka mabango ya marufuku  ya kuchimba mchanga katika eneo hilo lakini cha ajabu yaliondolewa na wachimbaji  hao.

“Walituambia mnajifanya wajanja sana kwenda ngazi za juu, sasa tunayatoa na kuyaweka chini na mchanga tunaendelea kuchimba. Nakumbuka tulikwenda hadi kwa Mpina (Luhaga) aliyekuwa Naibu wa Waziri Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ambaye sasa hivi ni waziri wa mifugo akatuahidi kulifanyia kazi lakini hatukupata mrejesho,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz