Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Meya Arusha azungumzia sintofahamu ya RC Gambo, DC Daqaro

35133 PIC+GAMBO Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na Mkuu wa wilaya ya Arusha Mjini, Gabriel Daqaro

Mon, 7 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na Mkuu wa wilaya ya Arusha Mjini, Gabriel Daqaro, wametofautiana juu ya ubora wa mabati ambayo yametumika kuezekwa kituo kipya cha afya Murieti katika Jiji la Arusha.

Kutofautiana kwa viongozi hao kumebainika baada ya kuvuja, kipande cha video ya kikao cha viongozi hao na watendaji wa Jiji la Arusha ambacho kilifanyika Desemba 2018 siku chache baada ya ziara ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais –Tamisemi, Josephat Kandege katika kituo hicho.

Katika video hiyo, mkuu huyo wa mkoa alidai kuwa mkuu wa wilaya, Daqaro aliyekuwa amekaa pembeni yake alitoa taarifa za kutilia shaka ubora wa mabati hayo na kueleza ameagiza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuchunguza.

Hata hivyo, mkuu huyo wa wilaya alipinga taarifa ya RC Gambo, kumtaja yeye kutoa taarifa na kueleza uamuzi wa kuchunguza mabati hayo ulitolewa na Naibu Waziri Kandege.

Kipande hicho cha video pia kinamwonyesha DC Daqaro akimweleza RC Gambo kueleza ukweli huku akitumia mikono kufafanua jambo lililomfanya mkuu huyo wa mkoa kunyamaza.

Wakati huo, Gambo alikuwa amesimama, Daqaro alizungumza akiwa amekaa na baadaye anaonekana mtu mmoja ambaye anakwenda hadi alipokuwa amekaa mkuu huyo wa wilaya na kuonekana kama akimtaka atulie.

Juhudi za kumpata Gambo na mkuu wa wilaya, Daqaro kuelezea tofauti hizo zilishindikana baada ya kutopokea simu zao.

Hata hivyo, Meya wa jiji la Arusha, Calist Lazaro akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Januari 6, 2019 amesema anashangazwa na mgogoro huo kwani, jiji la Arusha ndio linatuhumiwa kutumia mabati ya Gage 30 badala ya Gage 28 ambayo hutumika katika ujenzi wa majengo ya umma.

"Naibu Waziri alimwagiza DC Daqaro kuchunguza tukio hili lakini pia mkuu wa mkoa naye ameingilia kati na kuagiza TBS kuchunguza hapa kuna tatizo kwani kuna jambo ambalo linataka kufichwa," amesema.

Lazaro amesema kituo hicho cha afya kinasimamiwa na jiji ambalo ndilo lilitoa fedha kununua mabati lakini kuna tetesi juu ya ubora wa bati na madai zilizotumika zilitolewa na taasisi moja kama msaada.

"Hili jambo linahitaji uchunguzi ili kujua ukweli wa tukio hili ambalo linawagombanisha viongozi," alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz