Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mchungaji aomba radhi kukataza waumini ARVs

Bcc7efc9155bfb501b575334fc3133fb.jpeg Mchungaji aomba radhi kukataza waumini ARVs

Fri, 22 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MCHUNGAJI wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) wilayani Rungwe mkoa wa Mbeya, Emmanuel Mlundilwa amesema kukosa uelewa wa kutosha juu ya matumizi ya dawa za kufubaza virusi vya ukimwi (ARV’s), kulisababisha kuwakataza waumini wake kutumia dawa hizo na wakazidi kudhoofu na kupoteza maisha.

Amewaomba radhi ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao kutokana na kutofuata ushauri wa wataalamu wa afya kutokana na msimamo wake wa kuamini wataponywa kwa maombi kutoka kwake.

Mchungaji Mlundilwa alisema hayo alipokuwa akitoa ushuhuda kwenye mkutano wa kuhitimisha mradi wa mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU na kukomesha ukatili kwa vijana na watoto wa Pepfer FBO Initiative uliokuwa ukiendeshwa wilayani Rungwe na shirika lisilo la kiserikali la World Vision Tanzania.

Alisema kupitia vifungu kadhaa vilivyopo kwenye Biblia alikuwa akiwakataza waumini waliokuwa na maambukizi ya VVU wasitumie ARV’s na kuwataka wategemee maombi aliyokuwa akiwafanyia mpaka alipokutana na waratibu wa mradi wa Pepfer FBO Initiative aliosema walichukua muda mwingi kumbadilisha.

Alisema hadi anafikiwa na mradi huo alikuwa na waumini 15 waliokuwa wakiishi na maambukizi ya VVU na alikuwa amewaachisha kutumia dawa na wanne kati yao walikuwa taabani huku watatu wakiwa tayari wamefariki dunia.

Alisema kinachomuuziza zaidi ni kuona hata alipofuatwa na ndugu wa wamumini waliopoteza maisha na kumlilia kuwa amechangia vifo vya ndugu hao kwa kuwakataza dawa, aliwaaminisha kuwa ndugu zao walikufa kishujaa na wako mbinguni kutokana na kufa wakiwa na imani

moja, hatua iliyosababisha ndugu nao kuingia kwenye imani hiyo na wao kuacha matumizi ya dawa hizo.

“Nikiri wazi kuwa mimi mara kadhaa nilikusanya ARV’s na kuzitupia chooni. Na nimekwishashitakiwa na kukiri mahakamani kuwa ni kweli nilitupa dawa za waumini wangu chooni kwa kuwa nilitaka wabaki na imani moja ya kanisa pekee.”

“Niwaombe radhi mahakimu watatu waliowahi kusimamia kesi zangu nilipofikishwa mahakamani na nikawasumbua. Yupo mmoja alinitisha kunifunga jela miaka 30 hata kama hakuna kifungu cha namna hiyo, nikamwambia nipeleke nako kutakuwa na watu waanaodanganywa nitakwenda kuwafundisha waache dawa, akaniangalia baadaye akanambia nenda nitakufikiria,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) wilaya ya Rungwe, Shehe Hashim Maseta alisema kupitia mradi huo kumekuwa na ushirikiano wa karibu baina ya viongozi wa dini bila kujali imani zao kwe

nye kusimamia masuala ya kupinga ukatili ndani ya jamii na upimaji wa afya kwa waumini kupitia mpango wa Kibanda Afya.

Alisema kupitia elimu waliyoipata, pia unyanyapaa wa viongozi wa dini kwa waumini waliobainika kuwa na VVU na kujiweka wazi umepungua kwa kiasi kikubwa na kuwafanya wahusika kujiona sawa na waumini wengine na kujumuika nao kwenye shughuli zote bila ubaguzi kama ilivyokuwa awali.

“Awali tulijua mtu aliyepata maambukizi haya tunamhusisha moja kwa moja na uasherati, hivyo tukabaki wakati wote kumsema. Kumbe zipo njia nyingi tu mtu anaweza kuambukizwa na si waumini tu hata kiongozi wa dini anaweza kuambukizwa,” alisema.

Mratibu wa mradi huo kutoka World Vision Tanzania, Peter Chilewa alisema ulianza mwaka 2019, ambapo watu 991 wamepata huduma ya upimaji wa VVU, kati yao 705 wakiwa wanawake na 287 ni wanaume na kati ya hao 68 walikutwa na maambukizi na wengi wao kuanza kutumia dawa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz