Mchungaji Francisco Barajah (39), wa nchini Msumbiji aliyefariki baada ya kujaribu kuiga mafanikio ya kibiblia ya Yesu Kristo ya kufunga kwa siku 40 mfululizo bila kula chakula na maji anadaiwa kuwa alikataa ushauri wa wasaidizi.
Barajah, ambaye ni mwanzilishi wa Kanisa la Kiinjili la Santa Trindade na mwalimu wa Kifaransa katika mji wa Messica unaopakana na nchi ya Zimbabwe, alikuwa amefunga kwa siku 25 kabla ya kukimbizwa hospitalini na wafuasi wake kutokana na afya yake kuzorota.
Muhudumu wa afya ambaye alitoa ripoti ya Barajah alisema iligundulika kuwa ana upungufu wa damu na viungo vyake kushindwa kufanya kazi na pia alikuwa amepungua uzito kiasi kwamba hakuweza kusimama.
Wasaidizi wake wamedai kuwa, mara kadhaa walimshauri kutumia maji japo kidogo kutokana na uhalisia wa maisha ya sasa na mtindo wa vyakula lakini alikataa na jaribio ya kumtundikia maji kwa seramu na lishe ya kioevu hayakufaulu, kwani aliaga dunia saa chache baada ya kulazwa.
Wamesema, ilikuwa ni kawaida kwa Mchungaji huyo kufunga lakini si kwa muda mrefu kama huo huku kaka wa marehemu Marques Manuel Barajah, akisema mdogo wake aliaga dunia kutokana na shinikizo la chini la damu.