Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mchungaji Msigwa aingia katika ‘vita’ na RC, DC Iringa

20747 Msigwa+pic TanzaniaWeb

Thu, 4 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa. Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa ameingia katika mvutano mkali baina yake na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela.

Mvutano huo umeibuka baada ya Hapi kufanya ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wana Iringa aliyoipa jina la ‘Iringa Mpya’ iliyosababisha kuwekwa ndani saa 48 kwa Diwani wa Viti Maalumu (Chadema), Silestina Jonso.

Jumamosi iliyopita, Hapi aliagiza polisi kumweka ndani diwani huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kihesa kwa kile kilichoelezwa kuwa alisababisha kuvunjwa kwa nyumba ya mkazi mmoja wa mkoa huo.

Mchungaji Msigwa akizungumza na waandishi wa habari juzi mkoani humo alisema kitendo alichokifanya Hapi hakikubaliki na “Tumejipanga vizuri, tunamfungulia kesi mahakamani kwa sababu anatumia madaraka yake vibaya. Tutakutana naye mahakamani kwa sababu anatumia madaraka vibaya.”

Hata hivyo, jana Kasesela akizungumza na wana habari alimjia juu Msigwa kubeza ziara ya Iringa Mpya na kusema, “Kinachonishtua ni mheshimiwa huyo kuwa mtetezi wa watumishi wabovu.”

“Msigwa ni mbunge wa wananchi, waliowalalamikia walioadhibiwa ni wananchi wapigakura wake. Inakuwaje awatetee watumishi wanaolalamikiwa na wananchi wake?” alihoji.

Alimtaka Msigwa kujiunga na vyama vya wafanyakazi kama amechoka siasa, kwani huko ndiko mahali mwafaka ambako wafanyakazi wanaweza kutetewa kutokana na makosa yao ya kiutendaji.

Wakati mkuu huyo wa wilaya akieleza hayo, Mchungaji Msigwa alisema dhana ya Iringa Mpya ina upungufu kwa kuwa haikuwa shirikishi na ililenga kumjenga na kumuongezea umaarufu mkuu wa mkoa huyo.

“Dhana ya Iringa mpya sio shirikishi na haieleweki wadau wake ni kina nani, kama ni CCM, mkuu wa mkoa mwenyewe, UVCCM, mabaraza ya madiwani au wananchi wote?” alisema Msigwa.

Katika ziara hizo, Hapi alisema dhana ya ujenzi wa Iringa Mpya inalenga kuwatoa maofisini watendaji wa Serikali, kuamsha ari yao ya utendaji na kuwapeleka kwa wananchi kusikiliza kero zao, kuzifanyia kazi na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Hata hivyo, mvutano huo unakolezwa na Meya wa Manispaa ya Iringa (Chadema), Alex Kimbe ambaye naye ameibuka na akisema zaidi ya Sh40 milioni zilitumiwa na manispaa hiyo kulipa waandishi, mafuta ya magari, matangazo na mapambo katika ziara ya siku nne iliyofanywa na mkuu wa mkoa huyo katika halmashauri hiyo.

Kimbe alisema watahitaji ufafanuzi kutoka kwa watendaji wa halmashauri hiyo kujua fedha hizo zilikotolewa na kufanyiwa matumizi hayo bila ridhaa ya vikao halali vya halmashauri.

Akijibu tuhuma hizo, Kasesela alisema hakuna ukweli wowote kwani anachojua yeye sehemu kubwa ya fedha zilizotumika zilichangwa na marafiki wa Hapi na wadau wengine walioombwa kusaidia.

Kasesela alimshutumu Mchungaji Msigwa na Kimbe kwa kutumia ofisi ya meya kufanya shughuli zao za kisiasa.

Alisema mbunge na meya huyo wanapokuwa na shughuli zao za kisiasa wanatakiwa kuzifanya nje ya ofisi hiyo inayohudumia wananchi wote bila kujali itikadi zao za kisiasa.

Chanzo: mwananchi.co.tz