Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mchakato kuufuta mji mpya Kigamboni waanza

46464 Pic+kigamboni Mchakato kuufuta mji mpya Kigamboni waanza

Wed, 13 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Manispaa ya wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam ipo kwenye jitihada za kuufuta mpango wa mji mpya wa Kigamboni kisheria.

Mpango unaotakiwa kufutwa ni ule uliotangazwa na Serikali mwaka 2008 ambao ulikwama kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo kuandaliwa kwa kuzingatia hali halisi ya jiji la Dar es Salaam ya wakati huo na haukukidhi mahitaji ya uendeshaji na usimamiaji wa manispaa hiyo.

Akizungumza kwenye mkutano wa kukusanya maoni kwa wananchi ulioandaliwa na manispaa hiyo kwa kushirikiana na taasisi ya maendeleo jumuishi (I4ID) jana Jumanne Machi 12, 2019, mkuu wa wilaya hiyo, Sarah Msafiri alisema katika mapitio ya mpango mpya, ule wa zamani utafutwa kisheria.

Alisema kwa sasa yanakusanywa maoni ya wananchi ikiwamo kuhusisha kamati ya uwakilishi wa wananchi wa Kigamboni kuangalia wanataka nini kiwemo na kipi kisiwemo kwenye mpango mpya.

Alisema kwa kuwa mpango kabambe wa jiji la Dar es Salaam wa mwaka 1979 unafanyiwa mapitio na bado mpango wa awali uliokuwa ukijulikana kama mpango wa mji mpya wa Kigamboni upo hai kisheria, hivyo Manispaa kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, itafuta tangazo la Serikali namba 229 (GN.Na.229) la mwaka 2008 ili kutoa tangazo jipya litakaloupa mpango mpya uhalali wa kisheria.

"Lazima tuhakikishe shughuli zote za maandalizi ya mipango hii kufutwa wa mwanzo na kuupa mpya uhalali wa kisheria zinafanyika kwa njia ya ushirikishwaji wa wadau wote wa ardhi, wanawake na watu kwenye mahitaji maalumu," alisema Msafiri.

Alifafanua mpango wa matumizi ya ardhi ndani ya manispaa hiyo umegawanyika  maeneo makuu matatu ikiwamo mpango wa muda mfupi ambao ni miezi sita hadi miaka mitano, wa muda wa kati ambao utachukua miaka sita hadi 15 na wa muda mrefu utakaokuwa wa miaka 16 hadi 30.

Alisema wakati wa utekelezaji mpango huo, kutakuwa na mipango chochezi ya maendeleo ya muda mfupi ili kufungua fursa za kiuchumi.

Alisema wataalamu wamekamilisha hatua za awali za uandaaji wa wasifu wa manispaa hiyo unaoonyesha hali ya matumizi ya ardhi na shughuli za maendeleo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati inayowakilisha wananchi wanaomiliki ardhi Kigamboni, Kassim Abdallah amesema kwenye mpango kabambe wa matumizi ya ardhi wamebaini kuna mapungufu kadhaa yakiwamo ya kisheria, kitakwimu, kiusalama na kitaalamu.

"Tumeshatoa ushauri na tayari tumeyawasilisha kwa wataalamu ambao wanayafanyia kazi ili tusije kurudi kwenye mpango ulioshindwa ambao haukuwa na takwimu sahihi na ulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa kisheria," alisema Abdallah.

Alisema wameukubali mpango huu mpya kwa sababu unawashirikisha wananchi na unazingatia kila kasoro, maoni yanayotolewa katika hatua za awali za utekelezaji wake na kuyafanyia marekebisho.

"Ule wa awali hatukushirikishwa na tuliupinga kwa nguvu zote, huu wa sasa unatoa nafasi sawa kisheria," amesema Abdallah.

Naye Agnes Kipande mkazi wa Kimbiji alisema licha ya Kigamboni kuzungukwa na fukwe za bahari bado hawajanufaika nazo.

"Kwenye huo mpango mpya watuwekee soko la kisasa la samaki ili kusisimua uchumi wa wakazi wa huku ambao wengi kipato chao ni cha chini na wanafanya kazi kwenye sekta isiyo rasmi," alisema Kipande.

Alisema baada ya kila asubuhi kuondoka kwenda kutafuta riziki na fursa nje ya manispaa yao, wawe na sababu za kubaki zitakazotokana na kukua kwa shughuli za uzalishaji mali na uchumi kwa ujumla.



Chanzo: mwananchi.co.tz