Dar es Salaam. Serikali imesema baada ya kufanya maboresho katika sekta ya afya, imeanza kutekeleza mchakato wa kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na bima ya afya.
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi, Mfuko wa Bima ya Afya na wadau mbalimbali wa afya, makatibu tawala na wabunge, leo Februari 12 wamekutana kujadili suala hilo, wakilenga huduma za afya kwa wote bila vikwazo vya kiuchumi, yaani Universal Health Coverage (UHC).
Mkurugenzi wa huduma za kinga wizara ya Afya, Dk Leonard Subi amesema lengo la mkutano huo ni kubadilishana uzoefu lakini pia kupata maoni na mawazo kutoka kwa wadau mbalimbali ili kupata ufanisi katika hatua hiyo muhimu kwa taifa.
Amesema mjadala huo uliowakutanisha wadau kutoka ndani na nje ya nchi, umejikita zaidi kuangalia namna watakavyowafikishia bima ya afya watu wasio katika sekta rasmi.
“Leo asubuhi tumeanza kujadili mada mbalimbali kwanza kuangalia mwelekeo wa kisera ukoje, lakini pia utekelezaji mfuko wa afya ya jamii iliyoboreshwa yaani CHF unaendaje, lengo la Serikali tunataka kila Mtanzania aweze kupata huduma bora za afya mahala popote bila kikwazo chochote kikiwamo cha fedha,” amesema Dk Subi.
Mkurugenzi msaidizi wa huduma za afya -Tamisemi, Dk Anna Nswilla amesema kwa mfuko wa afya ulioboreshwa walianza na asilimia 7 ya wanachama lakini kwa sasa wamefikia asilimia 25, lakini bado waliopo katika mfumo wa bima ni wachache.
“Ni asilimia 33 pekee ya Watanzania waliopo katika mfumo wa bima ya afya, lengo la mchakato huu ni kuhakikisha tunawafikia asilimia 67 waliosalia katika mpango maalum,” amesema.
Katika majadiliano hayo, imepangwa angalau kufikia Juni mwaka huu, Serikali ihakikishe imeifikia mikoa yote kwa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa bima ya afya.