Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mchakamchaka waanza shuleni

Wed, 9 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Mikoani. Wakati msimu mpya wa masomo wa mwaka 2019 ukianza rasmi jana, pilikapilika za wazazi katika baadhi ya mikoa zimeshuhudiwa wakiwapeleka watoto wao shule.

Mwananchi pia liliwashuhudia wanafunzi wa darasa la kwanza ambao walikuwa wameongozana na wenzao ambao wako madarasa ya juu wakiwa katika makundi.

Jijini Dar es Salaam, gazeti hili lilifika katika shule za msingi Chamazi, Mbande, Mnazi Mmoja, Lumumba, Kisutu na Mtendeni kati ya saa 12:45 na 1:15 asubuhi na kuwakuta wanafunzi wakiwamo wa darasa la kwanza ambao wengi wao walionekana kushangaa mazingira ya shule.

Hata hivyo lilipotaka kuzungumza na walimu kuhusiana na mazingira ya ufunguaji wa shule na uandikishaji wa wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza, walikataa wakitaka kibali cha ofisa elimu.

Mjini Mwanza mambo yalikuwa tofauti baada ya kuzungumza na viongozi wenye dhamana ambao walizungumzia wanafunzi walioanza kidato cha kwanza.

Walisema mkoa huo umefanikiwa kuwapangia shule wanafunzi wote 55,330 waliofaulu darasa la saba 2018.

Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Michael Ligola alisema wametafuta mbinu mbadala ya kupambana na changamoto ya uhaba wa madarasa kwa kuwapanga wanafunzi 50 katika kila darasa.

“Kabla ya hapa tulikuwa tukiwapanga wanafunzi 40 kwa kila darasa, lakini sasa wameongezeka na vyumba bado ni tatizo, ndiyo maana tumeamua kupanga hivyo,” alisema Ligola.

Alisema kuna ongezeko la wanafunzi ikilinganishwa na vyumba vya madarasa vilivyopo.

Ligola alisema wanafunzi 64,000 walifanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka 2018 mkoani humo.

Kuhusu darasa la kwanza, awali ilielezwa kuwa Mkoa wa Mwanza unakusudia kuandikisha zaidi ya wanafunzi 175,000 mwaka huu.

Idadi hiyo kwa mujibu wa Ligola inaweza kuongezeka kutokana na mwamko wa wazazi kuwaandikisha watoto wao baada ya Serikali kuanza kutekeleza sera ya elimu bila malipo kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne.

Hata hivyo, ofisa elimu huyo alisema tabia ya baadhi ya wazazi kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine inatatiza uandikishaji wa wanafunzi wapya.

Kilimanjaro

Katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, sera hiyo inatajwa kuchochea ongezeko la wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza na awali.

Ofisa Elimu ya Msingi wa Manispaa ya Moshi, Patrick Leyana alisema wazazi wengi wamehamasika kupeleka watoto wao shule.

Alisema katika baadhi ya shule wanafunzi wanalazimika kukaa darasa moja zaidi ya 50 wakati Serikali ikiendelea na jitihada za kujenga na kukarabati miundombinu ya madarasa ambayo ni chakavu.

“Mfano hapa Shule ya Msingi Pasua wanafunzi ni wengi, mpaka sasa walioandikishwa darasa la kwanza ni karibu 100 na wanaweza kuongezeka jambo ambalo litatulazimu kuwa na mikondo minne,” alisema Leyana.

Akizungumzia hali ya uandikishaji, alisema hadi Januari 4 walikuwa wameandikishwa wanafunzi 1,784 sawa na asilimia 46.5 ya malengo.

“Tumelenga kuandikisha wanafunzi 3,874 na tunategemea idadi hiyo itafikia na kuzidi kwa kuwa katika eneo letu wazazi wengi hufika kuandikisha watoto darasa la kwanza baada ya shule kufunguliwa.” Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Jitegemee, Anna Kissenge alisema mwaka jana waliandikisha wanafunzi 196 wa darasa la kwanza na 94 wa lile la awali - idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na vyumba vya madarasa vilivyopo.

Alisema mwaka huu wameandikisha wanafunzi 99 na wanaendelea kuandikisha.

“Tunaweza kufikisha idadi ya 180 hadi 200. Mwaka 2017 tuliandikisha wanafunzi 202 ambao leo wanaingia darasa la tatu, tukiweka na wale wa 2018 ambao ni 196 ni idadi kubwa kulingana na miundombinu tuliyonayo,” alisema Kissenge.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Pasua, Lawrance Kisima alisema wameamua kugawa mikondo minne kwa kila darasa ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi.

“Wakifikia wanafunzi 180 kama ilivyokuwa mwaka jana itabidi mkondo mmoja uwe na wanafunzi 60,” alisema.

Mkoani Mbeya

Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wazazi walisema utaratibu wa uandikishaji darasa la kwanza ni mzuri kwa kuwa wanapokewa vizuri shuleni.

Gabriel Moses aliyefika kumwandikisha mtoto katika Shule ya Msingi Majengo, alisema changamoto ni ndogo ikiwamo kutakiwa kuwa na kitambulisho cha mpigakura kwa mzazi ambapo wengi wao hawakuvibeba siku ya jana.

“Lakini pia kabla ya kumuandikisha unatakiwa kutoa Sh3,000 kwa ajili ya malipo ya mlinzi na kwa wale wa darasa la awali unatakiwa kulipia Sh3,000 kwa ajili ya uji,” alisema Moses.

Amina Rajab aliyefika kumuandikisha mwanaye Shule ya Msingi Mbata alisema michango inayotakiwa ni kwa makubaliano kati ya wazazi na uongozi wa shule.

Alisema hatua ya Serikali kutoa elimu bila malipo imewapunguzia mzigo wazazi wa kusomesha watoto wao.

Imeandaliwa na Elizabeth Edward (Dar), Johari Shani na Sada Amir (Mwanza), Yonathan Kossam (Mbeya) na Florah Temba (Moshi)



Chanzo: mwananchi.co.tz