Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbwilo- Niligombana na wabunge kupinga kudharauliwa kazini

Mon, 31 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Elaston Mbwilo ni mstaafu aliyedumu kwenye ukuu wa wilaya kwa miaka 21 na ukuu wa mkoa kwa miaka mitano na kuifanya safari yake kwenye utumishi wa ngazi hizo kuwa miaka 26 hadi alipostaafu. Lakini, ana historia ya kuhamishwa kwenye vituo vya kazi mara nyingi kutokana na misimamo yake ya kusimamia haki, sheria na kutopenda kudharauliwa.

Mbwilo amerudi nyumbani kwake Veta Jijini Mbeya tangu alipostaafu rasmi Juni 2016 utumishi serikalini kwa nafasi ya ukuu wa Mkoa wa Simiyu, na sasa anajishughulisha na kilimo na usimamizi wa miradi yake.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake Block T jijini hapa, Mbwilo alifunguka mengi anayokumbuka ikiwamo siri yake ya kuhamishwa vituo vingi vya kazi kwa nafasi hizo.

Anasema amefanya kazi ya ukuu wa wilaya tofauti kwa miaka 21 na kituo cha kwanza ilikuwa Mpanda mwaka 1990 na ukuu wa mkoa kwa miaka mitano, na kote huko ni sehemu moja pekee aliyoomba kuhamishwa kwa hiari yake kutoka Wilaya ya Mpanda kwenda wilaya ya Mbeya, lakini wilaya nyingine zote alihamishwa kwa sababu za kiutawala.

“Unajua ukiwa na msimamo wa kuharibu kazi unaondolewa, lakini ukiwa na msimamo wa kusimamia mambo ya msingi na kutekeleza wajibu wako wale wanaokuletea matatizo watakuambia basi ondoka.

Nakumbuka kama mara mbili nimeitwa na kuulizwa ‘ee bwana eeh, naona hawa watu wanakupa shida kidogo kama upo tayari tukusaidie uende mahala pengine, nikasema sawa,” anasema Mbwilo.

Alisema kitu ambacho hakukubali na alikisimamia kwa wadhifa wake ni kutodharaulika, kuonekana kama mkuu wa wilaya si lolote wala chochote na kutaka kuamriwa vitu jambo lililomfanya kuhitilafiana na baadhi ya viongozi na wananchi.

Anasema: ‘Niligombana na wabunge wengine, unakuta mbunge anataka kuonesha kama mkuu wa wilaya si lolote si kitu…. Aaaah!! Mimi ndio mwenye nchi, ndio mtawala, ndio kiongozi. Ndio mkuu wa wilaya, natawala kwa hiyo siwezi kuchezewa chezewa na mtu mwingine, mbunge nitamheshimu kwa sababu ni mwakilishi wa wananchi, lakini sio kuchezewa chezewa.

Ninakumbuka mahala nilipoomba kuhamishwa ni kutoka Mpanda kuja hapa Mbeya kwa sababu nilitaka kuwa karibu na wazazi wangu pale Chimala wilayani Mbarali, lakini kutoka hapa kwenda huko kwingine nilihitilafiana na baadhi ya wananchi. Kwa mfano mimi nilipendekeza Chimala (Mbarali) pawe makao makuu ya wilaya ya Mbarali, kwa sababu kwa wakati ule Chimala kulikuwa na kila kitu muhimu kama vile Hospitali kubwa ya Misheni, barabara kuu ya Mbeya-Zambia, kituo kikuba cha Reli ya Tazara, nyumba za kuanzia zilikuwepo pale Kapunga’.

Anasema licha ya uongozi wa mkoa wa Mbeya kukubali mapendekezo hayo lakini walijitokeza watu wengine kwa kutumia nguvu yao kupinga uamuzi huo na wakafanya wanavyojua wao na kuanza kumtengenezea uhasama.

Anasema misimamo isiyoyumbishwa siku zote ndio nguvu kuu ya kiongozi bora japo huchukiwa na watu wenye tamaa binafsi na kupenda kuwakandamiza wanyonge, hivyo yeye alijitahidi kusimama katika haki na ndio sababu alichukua na kuhitilafiana na watu.

Anasema licha kutengenezewa mizengwe na wapinga maendeleo na wapenda rushwa, ufisadi na kujimilikisha mali isivyo halali lakini kwa vile alisimamia sheria na haki katika majukumu ya kuwatumikia wananchi bila ubaguzi kulimfanya kukaa miaka mingi katika utumishi wake.

“Kilichonisaidia mimi ni kufuata sheria, taratibu na kushirikisha walio chini yangu na kwamba mimi nimekaa miaka 26 Serikali, 21 ya ukuu wa wilaya na mitano ukuu wa mkoa na kuhama hama kote huko ni kwa vile hakuna mahali nilifanya kwa kuchepusha sheria na taratibu. Uadilifu, wizi wizi na udokozi kwangu ilikuwa mwiko,” anasema Mbwilo.

Anasema katika utumishi wake alizingatia mambo makuu matatu ambayo ni kutomuonea mtu, kutodhulumu na kuheshimu watu wote walio chini na walio juu yake.

Alidanganywa na watumishi

Anasema kiongozi bora ni yule asiyesubiri kupelekewa taarifa ya utekelezaji wa jambo lolote kwa njia ya maandishi ofisini kwake na kuamini maandishi hayo, bali ni kwenda eneo la tukio ili kujionea hali ya utekelezaji na kujiridhisha mwenyewe na sio kuambiwa.

Anasema kufanya hivyo ndio kuharakisha maendeleo kwa wananchi na kuifanya nchi isonge mbele zaidi.

Ndiyo maana katika utawala huu, Rais amechukua zaidi vijana wenye uwezo wa kukimbia kwani uongozi wake unataka mtu anayekimbia sio kutembea. Lakini, sio kwamba amewaacha kabisa wazee, hapana bado wapo lakini ameweka sehemu ya kukimbia sana. Kwa hiyo wakuu wa wilaya, wa mikoa na nakumbuka hata mimi nilipokuwa bado kijana nikiwa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, sikumbuki kama siku 60 zilifika niliwahi kulala kwa mwaka mzima.

Siku zote mimi nilishinda na kulala vijijini na unapotembea zaidi vijijini ndipo unapojua zaidi matatizo ya wananchi vijijini, kwani kiongozi yoyote asipotembelea eneo fulani unaweza kusema hakuna matatizo lakini ngoja kiongozi afike ndio utajua kuna wananchi wana shida kubwa vijijini.

Kiongozi mwenyewe unapoona uhalisia wa tukio ndio unaweza kuchukua hatua, lakini hujaona… unaandikiwa barua na kuamini bila kujiridhisha lazima utakwamishwa tu. Nani uzoefu katika hili wakati nikiwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara na nikiwa mkuu wa mkuu wa mkoa, tulilekeza kila kijiji mtu alime kiasi fulani ili kunusuru baa la njaa.

Nikapanga ziara kuanza kuzunguka kukagua utekelezaji wake, nikafika kijiji kimoja haya mwenyekiti soma taarifa nikaelezwa kijiji lina shamba kiasi Fulani, nikasema sawa twende tukaone hilo shamba, nikaanza kupigwa Kiswahili mara oooh, ni mbali kidogo… nikasema gari ninalo twendeni tu aah, huko gari halifiki….

Nikasema mabwana shamba na maofisa watendaji kata tumewapa pikipiki, wakaanza aah, mzee shamba lingine lipo kulee mbali kidogo hutaweza kufika. Nikawauliza kwani nimekuja kufanya nini? Si nimekuja kufanya kazi? Jibu ndiyo.

Nikawauliza kwani nyie mlikwenda kulima kwa namna gani? Wakasema aaah! Tulikwenda kwa baiskeli mara kwa miguu, nikawaambia ofisa kilimo, mtendaji kata wote mna pikipiki hapa, haya wengine wote tuachane hapa, mimi utanibeba ofisa tarafa na wengine wekeni mshikaki hukuna trafiki huku twendeni.

Anasema kufika eneo la tukio hakuna cha shamba wala mfano wake, na hapo ndipo alipogundua kwamba siku zote huwa anapelekewa na kusomewa taarifa za uongo ofisini kwake na kumbe kwenda moja kwa moja eneo la tukio na kujionea ukweli ndio unajiridhisha uhalisia wake.



Chanzo: mwananchi.co.tz