Tukio la kufyekewa migomba kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera sio jambo la kawaida. Mara nyingi hubeba ujumbe fulani kwa muhusika tena wahatari na anatakiwa kuchukua hatua haraka iwezekanavyo.
Mara nyingi makazi ya mtu ambaye migomba yake imefyekwa na wananchi huwa sio sehemu salama tena kuishi.
Wakati mwingine matukio ya kufyeka migomba huambatana na kuteketeza nyumba na hata mauaji.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwenye matukio mawili ya ukatili yaliyohusisha kifo cha mwanafunzi na mwanamke.
Namna ilivyokuwa
Mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Ganyamkanda, Kata ya Kishanda wilayani Bukoba, Ismail Hamis (7) baada ya kutoweka wakati akirejea nyumbani Aprili 5, mwaka huu zilipita siku 11 za sintofahamu kwa wananchi wa kijiji cha Ihunga.
Mazingira ya kutoweka kwake yaliibua uvumi wa imanai za kishirikina uliosababisha Polisi kufanya upekuzi kwenye nyumba ya Colleta Francis (65) lakini hawakufanikiwa kumpata Ismail hali iliyoongeza maswali kuhusu tukio hilo.
Baba mzazi wa mwanafunzi huyo Hamis Hamidu anasema siku aliyopotea mtoto wake kama kawaida aliamka asubuhi na kumsalimia kisha kumuaga kuwa anakwenda shuleni na alifanya hivyo pia kwa mama yake mlezi.
‘’Ilikuwa ni Ijumaa asubuhi aliniaga kuwa anakwenda shuleni, baada ya kupotea katika mazingira ya kutatanisha wakati anarudi nyumbani nilitoa taarifa kwa uongozi wa kijiji. Baada ya kupekuliwa nyumbani kwake (Colleta) na mtoto kutoonekana akaniambia nimemdhalilisha,” anasema Hamis.
Wakati ukimya ukiwa umetawala huku wananchi wakiendelea na sintofahamu juu ya kupotea kwa mtoto huyo, siku moja mbwa akaliamsha upya balaa baada ya kubweka mara nyingi huku akifukua ardhini shambani kwa Colleta.
Tukio hilo lilivuta watu waliokusanyika kuona kuna nini. Mbwa huyo aliendelea kufukua sehemu hiyo hadi alipoufikia mwili wa kijana ambapo alianza kuvuta shati nguo inayoelezwa alivaa Ismail siku alipotoweka akitokea shuleni.
Hamidu anasema baada ya mbwa kufichua eneo hilo alipigiwa simu ili kuthibitisha kama ule ulikuwa ni mwili wa mtoto wake na baada ya kuuona hakuwa na shaka nao.
Miongoni mwa mambo yanayoacha maswali mpaka leo ni mwili wa mwanafunzi huyo kuzikwa ukiwa umesimama huku sehemu za siri zikiwa zimeondolewa. Ni tukio la pili katika kijiji cha Ihunga baada ya Laurian Kakoto (83) kuuawa na kuzikwa miezi michache iliyopita kabla ya tukio hilo.
Kikongwe huyo aliuawa na kuzikwa kichwa chini miguu juu huku baadhi ya viungo vya mwili wake zikiwamo korodani zikiwa zimeondolewa. Alitoweka alipokwenda sokoni ambapo hakurejea hadi alipogundulika amezikwa.
Baada ya mwili wa Ismail kugundulika shambani kwa Colleta mita 60 kutoka kwenye makazi yake, wananchi walivamia nyumba yake na kumtoa nje, hapo alianza kushambuliwa kwa silaha za jadi. Walimuua mtuhumiwa, kuteketeza nyumba yake kwa moto na kufyeka migomba kisha kutawanyika huku baadhi yao wakienda kushiriki mazishi ya pili ya mwanafunzi Ismail baada mwili wake kupatikana.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi kuhusu tukio hilo anasema wananchi walimhusisha Colleta na kifo na mazingira ya kupotea kwa Ismail na walimshambulia kwa silaha za jadi hadi kifo chake.
Mazishi ya Colleta pamoja na kukusanya watu kutoka ndani na nje ya Kata ya Kishanda, Polisi walilazimika kuchimba kaburi baada ya wananchi kugoma.
Shuhuda wa tukio hilo, Johakimu Kabikabo anasema pamoja na kushawishiwa kwa ahadi ya fedha ili kuchimba kaburi bado mwitikio haukuwepo hali iliyowafanya polisi kuifnya kazi hiyo.