Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbuzi dume kuzikwa hai kaburi lililochimbwa eneo lenye mgogoro

91552 Mbuzi+pic Mbuzi dume kuzikwa hai kaburi lililochimbwa eneo lenye mgogoro

Mon, 13 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serengeti. Matambiko ikiwamo beberu la mbuzi kuzikwa akiwa hai ni mambo yanayotarajiwa kufanyika iwapo utatoka uamuzi wa kutomzika Kitati Nyamsacha (80) mkazi wa Morotonga wilayani Serengeti mkoani Mara ambaye mazishi yake yalisitishwa na polisi kutokana na mgogoro wa ardhi alipotakiwa kuzikwa.

Mazishi hayo yalisitishwa na Kamanda wa polisi wilaya ya Serengeti, Methew Mgema juzi IJuma Januari 9, 2020 wakati wakijiandaa kwa mazishi baada ya kupokea nakala ya uamuzi wa baraza la ardhi na nyumba la Musoma kumpa ushindi Beby Sambagita aliyekuwa anashitakiwa na Nyamsacha (marehemu).

Magori Berabera kijana wa kaka yake na marehemu Nyamsacha leo Jumamosi Januari 11, 2020 nyumbani kwa marehemu amesema kaburi kubaki wazi kwa mila na desturi za kabila la Waikoma ni kitu kisicho cha kawaida hivyo watalazimika kufanya matambiko iwapo hawatamzika hapo.

"Sisi tumeamua kwenda mahakama kuu kitengo cha ardhi kupinga ushindi wa Beby, ikitokea vinginevyo tukaamua asizikwe mwenye kaburi hili lililojengwa kwa umri wake atatafutwa beberu akazikwa mzima kisha matambiko mengine yatafanyika," amesema.

Amesema wasipofanya hivyo vifo katika ukoo wao vitakuwa vya mfululizo na katika mazingira ya utata, hili linajulikana maana kaburi likichimbwa anatakiwa azikwe mtu, hapa kimeshindikana kutokana na mambo ya ajabu tuliyofanyiwa na polisi wakasitisha mazishi dakika ya mwisho," amesema.

Esther Gambahewa (70) shemeji wa marehemu amesema hata kama watazika hapo  lazima kufanyike tambiko kwanza kwa kuwa kaburi limekaa toka Januari 8, 2020 lilipochimbwa na alitakiwa kuzikwa Januari 9,2020.

"Kwa umri wangu wote huu hili ni tukio la kwanza kuona hapa kwetu kuzuia mazishi kwanza limetuingiza katika mazingira ya ajabu, maana uamuzi ulikuwa ya Oktoba 24, 2019 hakuwahi kuleta kwa aliyekuwa anamshitaki ambaye ni marehemu lakini baada ya kufa ndipo wanaleta kuwa ameshinda," amesema.

Nyamsacha alifariki Januari 7,2020 usiku nyumbani kwake, kaburi lilichimbwa na kujengewa Januari 8 kwa ajili ya mazishi Januari 9,2020 siku ambayo polisi walizuia mazishi kwa madai kuwa eneo hilo kisheria si la marehemu bali Beby waliyekuwa wanashitakiana naye.

Kutokana na uamuzi huo mwili ulirudishwa chumba cha kuhifadhia maiti hospitali ya Nyerere huku wakianza taratibu za kutinga Mahakama kuu kitengo cha ardhi Musoma kupinga uamuzi huo ili marehemu azikwe kwenye eneo hilo wanalodai ni lake alilinunua mwaka 1993 kwa baba yake na aliyefungua kesi na kushinda baada ya kusikilizwa upande mmoja.

Chanzo: mwananchi.co.tz