Mvutano wa kugombea eneo la kujenga kituo cha afya kati ya kijiji cha Njinjo na Kipindimbi wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi umechukua sura mpya baada ya mbunge wa Kilwa Kusini, Francis Ndulane na diwani wa Njinjo, Nurudini Abdallah kurushiana maneno.
Abdallah amesema alipigiwa simu na mbunge huyo akitaka kujua msimamo wake kuhusu ujenzi wa eneo hilo na kumjibu kuwa ni Njinjo akisisitiza kuwa ni msimamo wa kikao cha kamati ya maendeleo ya kata.
"Baada ya majibu hayo mbunge alisema kama ndiyo wanatofautiana wenyewe kwa wenyewe basi ataona kama mwaka 2025 atashinda udiwani kwamba atahakikisha uchaguzi ujao sipati ushindi."
"Mimi nilichaguliwa na wananchi na yeye alichaguliwa na tusubiri uchaguzi ujao utaeleza," amesema.
Kwa upande wake Ndulane amesema ujenzi wa kituo hauna mjadala utafanyika kijiji cha Kipindimbi na tayari barua ya maelekezo kutoka wizarani imeletwa inayobadili ujenzi wa kituo hicho kutoka kijiji cha Njinjo kwenda kijiji cha Kipindimbi .
"Mimi kwa sasa sina muda wakuongelea haya mambo nimebanwa nina mambo mengine naenda kushughulikia hoja za wananchi kata ya Somanga, nimepanga siku rasmi kuzungumzia mambo hayo, nitafanya kikao na waandishi wa habari mkoani," amesema Ndulane.
Advertisement Musa Mohamedi mkazi wa Kipindimbi amesema kitendo cha viongozi kutofautiana kwenye suala lenye maelekezo ya Serikali linaweza kuwagawa wananchi.