Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge awatuliza walioathirika na tope mgodi Mwadui

Waathirikapiicnhnhn Mbunge awatuliza walioathirika na tope mgodi Mwadui

Thu, 17 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mbunge wa Kishapu Boniphace Butondo, amewataka wananchi walioathirika na maji tope kuwa na utulivu na imani kwamba mgodi wa Williamson Diaond Ltd (WDL) utaendelea kuwapa zote zinazotakiwa kuwalipa haki zao zinazotakiwa.

Wito huo ameutoa leo, Novemba 17, 2022 alipowatembelea wananchi hao walioathirika na majitope yaliyotokana na kupasuka kwa bwawa la kuhifadhia majitope linalomilikiwa na mgodi huo.

Butondo amesema Serikali inawajali wananchi wake hivyo itahakikisha inasimamia kikamilifu ili wapate sitahiki zao ikiwemo kujengewa nyumba za kuishi zenye ubora zitakatosha kwa familia walizonazo.

"Licha ya kujengewa nyumba pia mtalipwa sitahiki zenu zote na sasa mgodi unaendelea kufanya taratibu za kutafuta nyumba za kupangisha zinazozunguka mgodi huu kwa wale watakaotaka kwenda kuishi huko mtahudumiwa kama kawaida huku taratibu za ujenzi zikiendelea na kutafutiwa eneo kwa ajili ya kulima kwa sababu maeneo yenu mliyokuwa mnalima yamevamiwa na tope ambalo mpaka sasa hivi bado bichi,"amesema Butondo.

"Nilipokuja awamu ya kwanza niliwaahidi kuwa nitakuja tena kuwaona mnaendeleaje ndiyo maana nimekuja, nilisisitiza mpatiwe huduma nzuri na salama, ninaamini mnatendewa haki na mnapata chakula vizuri na sisi ndiyo tunataka mpate chakula kizuri ili muendelee kupata amani kama watu wengine,"amesema Butondo.

Mbunge huyo pia aliushukuru uongozi wa mgodi huo kwa kuendelea kuwahudumia wananchi hao na kuwapeleka na kuwarudisha shule wanafunzi walioathirika na majitope.

"Serikali ipo pamoja nanyi inawapa pole sana, kwa kupatwa na ajali hii, siyo kwamba mnapenda kukaa hapa bali ni kwa sababu ya shida tu, hapa mnakaa kama vile mpo kifungoni hamfurahi sana ,hivyo tunaomba taratibu hizi zifanyike kwa haraka ili muende kwenye nyumba zenu ambazo zitajengwa na kukamilika ndani ya miezi minne hadi mitano” amesema

Ofisa Uhusiano wa mgodi huo, Benard Mihayo amesema wananchi hao wapo 131 kutoka kaya 32 na wametoka katika kijiji cha Kabondo Kata ya Mwadui Lohumbo na wanawahudumia kulingana na mahitaji ya kibinadamu.

"Hakuna atakayedhulumiwa chochote kwani kutakuwa na timu ya kijiji na ya Serikali ili kuhakikisha mwananchi anachokiongea ni sahihi, tathimini ndiyo itatuongoza ili kuhakikikisha mwananchi anapata stahiki zake hivyo nawaomba muendelee na uvumilivu, sisi tutahakikisha mnapata huduma zote mnazositahili” amesema

Mihayo amesema kwa sasa hawaendelei na uzalishaji mpaka pale Serikali itakapomaliza uchunguzi wake ndipo wataanza.

Meneja wa mgodi huo Ayoub Mwenda, amesema wananchi hao watalipwa mara baada ya watu wa tathimini kukamilisha kazi yao lakini pia mgodi utaliboresha eneo hilo.

"Tutaongea na viongozi wa kijiji wa wilaya ili mpate maeneo ya karibu mnayoyazoea na kuhakikisha watoto wanaenda shule,tunatakiwa tupate idadi ya watu wote, hii ni ajali ambayo hakuna aliyekusudia mpaka sasa hivi hakuna anayejua kuwa chanzo ni nini, hivyo uchunguzi unaendelea ili kujua chanzo ni nini tuwe na uvumilivu, tupo pamoja nanyi bega kwa bega,"amesema Mwenda.

Hata hivyo baadhi ya walioathirika na kupasuka kwa bwawa hilo wamegawanyika pande mbili juu ya mpango wa kujengewa nyumba ambapo moja inataka walipwe fedha na nyingine zijengwe nyumba

Robert Gibe amesema kutokana na mgawanyiko huo wanahitaji kukaa kwenye meza ya mazungumzo ili kufikia mwafaka wa jambo hilo ili kila mmoja apate anachostahili.

Familia zilizoathirika na majitope mpaka sasa zinaendelea kuhudumiwa na mgodi huo na waliolazwa hospitali wameruhusiwa na waliopoteza mawasiliano wamenunuliwa simu.

Baadhi ya viongozi walioambatana mbunge Butondo kwenye ziara hiyo ni viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga, Edward Ngelela

Chanzo: www.tanzaniaweb.live