Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalum George Mkuchika amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kuwaita ‘mbumbumbu’ wabunge wa mkoa huu hasa kwenye mitandao ya kijamii huku wakiseme hawasimamii maendeleo ya mkoa huo.
Akizungumza katika hafla fupi ya kuweka mikataba ya ujenzi wa barabara ya Mnivata – Newala – Masasi (km 160) kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa daraja la Mwiti, Mkuchika ambaye pia ni Mbunge Jimbo la Newala Mjini amesema kuwa vijana wamekuwa ‘bize’ na mitandao na kutoa maneno yasiyofaa kwa wabunge wao.
“Vijana wa kwenye mitandao wanasema kuwa wabunge wa Mtwara mbumbumbu baada ya kuona bajeti imepita hatujasema kitu na leo tunaweka sahihi mikataba ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami inawezekanaje uite wabunge mbumbumbu,” amesema na kuongeza;
“Nashangaa kuna watu wanasema kuwa hakuna tunachofanya na tukikamilisha mnapita humo humo mnatafuta nini hauwezi kuongoza nchi kwakusema uongo subiri uchaguzi wa mitaa muone CCM tutakavyowapiga.”
Mkuchika amejitetea kuwa wabunge wa Mtwara wanafanyakazi kama timu ndio maana wanafuatilia mambo kwa faida ya mkoa mzima: "Tunashukuru barabara imekamilika na sasa tupo katika ukarabati wa maji unaendelea wa zaidi ya Sh84 bilioni katika mradi wa makonde.”
Nae Mbunge wa jimbo la Tandahimba Katani Ahamed Katani amesema kuwa wameililia kwa miaka mingi barabara hiyo ambayo inaenda kuboresha uchumi wa wilaya hiyo yenye uzalishaji mkubwa wa korosho.
“Tangia nchi yetu ipate uhuru hatujawahi kuwa na barabara ya lami kukamilika kwa barabara hii kutachochea ukuaji wa Wilaya ya Tandahimba na mkoa kwa ujumla kwakuwa ndio mkoa pekee ambao una uchumi mkubwa wa zao la korosho,” amesema Katani.
Nae Mbunge wa Jimbo la Nanyamba Abdallah Chikota amesema kuwa awali ujenzi ulianza kwa kilomita 50 kutoka Mtwara mjini hadi kijiji cha Mnivata na kubakia kilomita 160 ambayo ndio inaenda kuingia mkataba leo ili ujenzi uweze kuanza.
“Kukamilika kwa barabara hizi kutaongeza chachu ya maendeleo katika maeneo yetu ambapo tunaamini kuwa itaongeza hamasa na kuwa kichocheo cha uchumi katika nchi yetu sasa tunapeleka nguvu katika ujenzi wa reli ya kisasa kutoka mtwara hadi Ruvuma kwenye makaa ya mawe,” amesema.
Mbunge wa Jimbo la Ndanda Cecil Mwambe amesema kuwa kazi ya mama kwenye familia ni pamoja na kuamua ugomvi hasa anapoona watoto wanagombana na alichofanya leo ni kuamua ugomvi kwa wabunge na wananchi kwenye barabara hiyo ambayo ilikuwa ni kero kubwa.
Mbunge wa Mtwara mjini Hassan Mtenga alisema kuwa miradi mingi ya barabara kuna kuwa hakuna uaminifu na hiyo kuomba wilaya zote inapopita barabara hiyo uwepo usimamizi na hivyo kuwawezesha kupata barabara bora yenye viwango vinavyotakiwa.