Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge Abood aeleza jinsi ya kutangaza utalii Morogoro

86050 Pic+abood Mbunge Abood aeleza jinsi ya kutangaza utalii Morogoro

Thu, 28 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Mbunge wa Morogoro Mjini (CCM), Abdul-Aziz Abood amewataka wananchi kuwatumia wanasoka na wanamuziki wakongwe kutangaza utalii mkoani Morogoro.

Akizungumza leo Jumanne Novemba 26, 2019 katika kampeni ya wiki ya kuhamasisha utalii Morogoro iliyoandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Abood amesema utalii unatakiwa kuendelezwa kwa kutangaza vivutio.

“Serikali imefanya juhudi kukuza na kuendeleza utalii, sisi tunatakiwa kuonyesha kwa vitendo kuutangaza utalii uliopo kwetu,” amesema mbunge huyo.

Amesema kuboreshwa kwa sheria mbalimbali za kulinda wanyamapori na mapori ya Hifadhi ni kiashiria kikubwa cha Serikali kutaka kukuza utalii.

Akizungumzia namna ya kuwatumia wanasanii na wanamichezo kutangaza utalii wa Mkoa huo, amesema kuna makaburi ya mwanasoka Gibson Sembuli; wanamuziki, Salum Abdallah na Mbaraka Mwishehe, kwamba yakitumika vyema yanaweza kuwa kivutio cha utalii.

Amesema makaburi hayo yanaweza kutembelewa na wanasoka wa sasa pamoja na wanamuziki, kutaka yaboreshwe.

Awali mkurugenzi wa taasisi ya RTCN, Eda Kapinga amesema pamoja na Morogoro kuwa na vivutio vingi vya utalii, vinavyofahamika ni vichache.

“Tumeamua kufanya uhamasishaji wa kutangaza vivutio vyote hasa vilivyopo maeneo ya milimani ambavyo mara nyingi vinasahaulika.”

“Jamii inatakiwa kutambua na kuhamasika kwa sababu wao ndio walengwa, kama taasisi tunachofanya ni kuwaelimisha watoto wa shule za msingi na sekondari waweze kufahamu mapema faida za utalii kupitia matamasha,” amesema Kapinga.

Ofisa Maliasili Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa ameeleza kuwa katika kuendeleza utalii wanatafuta mwekezaji katika uwanja wa maonyesho ya Nanenane atakayeweka wanyama uwanjani hapo ili wananchi waweze kutembelea muda wote, si kusubiri wakati wa maonyesho.

Chanzo: mwananchi.co.tz