Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbopo na maajabu ya kutoka shule ya mwisho hadi ya 859

42594 Pic+mbopo Mbopo na maajabu ya kutoka shule ya mwisho hadi ya 859

Tue, 19 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukistaajabu matokeo ya Shule ya St Francis, utayaona ya Shule ya Sekondari Mbopo.

Achana na matokeo ya kipekee na pengine ya kushangaza ya shule ya St Francis iliyoongoza katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyotangazwa mwishoni mwa Januari.

Matokeo hayo yana sura nyingine ya kipekee.

Unakumbuka katika matokeo ya mwaka 2017 Mkoa wa Dar es ulipoongoza kwa kutoa shule sita zilizoshika mkia katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka 2016?

Katika orodha ya shule hizo sita, ilikuwamo Shule ya Sekondari Mbopo. Kati ya wahitimu 71 hakuna aliyepata daraja la kwanza, la pili wala la tatu. Ni watahiniwa 16 pekee waliopata daraja la nne, huku waliosalia 55 wakifeli kabisa kwa kupata sifuri.

Miaka miwili baadaye shule hiyo iliyopo Kinondoni mkoani Dar es Salaam, imefanya maajabu kwa kushika nafasi ya 859 kati ya shule 3488, huku ikifuta daraja sifuri.

Kwa mujibu wa Necta, shule hiyo iliyokuwa na watahiniwa 70, imepata wastani wa ufaulu wa pointi (GPA) 3.7578, ikiwa na wanafunzi wawili waliopata daraja la kwanza, wanafunzi saba daraja la pili na watahiniwa tisa wakipata daraja la tatu.

Daraja la nne ni wanafunzi 51 na mtahiniwa mmoja pekee aliyepata daraja sifuri.

Mabadiliko ya shule yalianza tangu mtihani wa mwaka 2017 ilipojitutumua na kuwa ya 2298 kati ya shule 3039. Mwaka uliofuata Mbopo ikafanya muujiza kwa kuruka viunzi zaidi ya 2000 na kushika nafasi katika orodha ya shule 1000 bora.

Nini kimetokea?

Aliyekuwa Mkuu wa shule ambaye sasa amepata uhamisho, Hamis Malela anasema baada ya kujiunga na shule hiyo mwishoni mwa 2016 na kubaini changamoto tete ikiwamo ya utovu wa nidhamu, alilazimika kuandaa mkakati uliohusisha kubadili safu ya uongozi wa shule.

“Tukatengeneza mkakati ulioitwa tokomeza sifuri uliokuwa wa miaka mitatu. Mkakati huu uliwahusu wanaoingia kidato cha nne mwaka 2017 hadi wale 2019 kuhakikisha hawapati daraja sifuri,’’ anasema na kuongeza:

“Ndani ya mkakati huu kulikuwa na sera ya kulindana kwa wanafunzi wenyewe kwa wenyewe ambapo tuliwagawa wawili wawili yaani kila mwanafunzi anakuwa mlinzi wa mwenzake. Hali hii ilisaidia kuwarudisha watoto kutoka vichakani.’’

Akiwa na matumaini kuwa kama shule imekuwa ya mwisho, inaweza pia ikawa ya kwanza, uongozi wake uliandaa mkakati mwingine waliouita ‘Nipige tafu’

“Hapa mwalimu mmoja akipata dharura, kipindi chake hakipotei badala yake kinashikwa na mwalimu mwingine. Ikiwa mada fulani mwalimu hana utashi nayo, basi anasaidiwa na mwingine kwenye idara husika,’’ anasema.

Kwa sasa Malela anasema wana mkakati wanaouita: ‘ Towards Universities’ (Kuelekea vyuo vikuu) wenye dhamira ya kukuza ufaulu kwa wanafunzi walio kidato cha pili mwaka 2021. Na wale watakaofanya vibaya anasema angalau wawe na alama C katika masomo matatu yatayaowafanya wasome kidato cha tano na sita na hatimaye kuingia vyuo vikuu.

Wataalamu wa Hisabati walivyoinusuru

Matokeo mabaya ya shule hiyo mwaka 2016 yaliwagusa wadau wengi, kikiwamo Chama cha Hisabati Tanzania (Mat/ Chahita ),ambapo wanachama wake waliamua kujitolea kufundisha somo hilo.

Mwenyekiti wa Mat/Chahita, Dk Saidi Sima anasema, walilazimika kuomba kibali kuztembelea shule zilizofanya vibaya ikiwamo Mbopo kwa minajili ya kujua kilichozisibu shule hizo.

“Tulienda na tuligundua changamoto mbalimbali ikiwamo uhaba wa walimu wa hesabu. Tulikubaliana na wenzangu tutumie maadhimisho ya wiki ya hesabu kufundisha na tulianzia shule ya Mbopo,”anasema.

Dk Sima anasema walifundisha kuanzia kidato cha pili hadi cha nne na kila mwalimu alifanikiwa kumaliza mada moja ndani ya muda huo sanjari na kuwapa moyo wa kusoma kwa bidii wanafunzi ili wafanye vizuri katika mitihani.

“Matunda yameanza kuonekana ikiwemo wanafunzi wa 14 wa Mbopo waliofanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha nne kwa kupata alama B wakati awali walikuwa wakipata F,’’anasema.



Chanzo: mwananchi.co.tz