Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbeya waonja adha mgomo wa daladala

Wed, 20 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya.Wananchi katika Jiji la Mbeya jana walikumbana na adha ya usafiri kufuatia mgomo wa daladala uliosababishwa na madereva daladala kulalamikia bajaj kuendelea kubeba abiria kwenye barabara kuu, hivyo mgomo huo ni jitihada za kushinikiza Bajaj kuondolewa kwenye njia hizo.

Mgomo huo ulianza saa 12 alfajili, huku njia zilizoathirika na mgomo huo ikiwa ni Nsalaga-stendi kuu, Igawilo-stendi kuu,Must-Mwanjelwa,Mbalizi-Mwanjelwa,Igawilo-Mbalizi na Nsalaga-Mbalizi.

Kutokana mgomo huo gharama za usafiri zilipanda mara dufu ukilingamisha na zile za kila siku, ambapo Bajaj,magari aina ya Noah na gari za kubebea mizigo maarufu kirikuu zilikuwa zikibeba abiria kwa kiasi cha Sh.1000 kutoka kituo kimoja kwenda kingine na bodaboda wakitoza kiasi cha Sh.5000 kutoka Uyole hadi Kabwe tofauti na siku zingine ambapo hutoza Sh. 3000.

James Mwaipokela Dereva wa daladala ya Mwanjelwa-Must,alisema hawatorejesha huduma za usafiri barabarani mpaka pale Serikali ya mkoa itakapoondoa bajaj  kwenye barabara kuu.

Mwaipokela, alisema ‘Hawa madereva bajaji wamekuwa wakichukua sehemu yoyote abiria bila kufuata utaratibu uliyowekwa na Serikali wa kuchukua abairia kwenye vituo vilivyopangwa na hawachukuliwi hatua,daladala ikichukua abiria nje na kituo tunakamatwamatokeo yake abiria wameacha kupanda daladala zetu kisa bajaji  hivyo tumeamua kufanya hivyo ili wahusika wasikie kilio chetu’.

Naye Amani Khamis dereva daladala za Igawilo-Stendi kuu, alisema kilicho wafanya wagome ni fujo wanazofanyiwa na madereva bajaji wanavyokuwa barabarani na kupelekea ajali za mara kwa mara.

Khamisi, alisema bajaji zilipangiwa kufanya shughuli zake nje ya barabara kuu na ‘ruti’ zake zinajulikana hali ambayo imekuwa tofauti badala  yake wanabeba abiria kutoka stendi kuu hadi uyole matokeo yake daladala zinakosa abiria.

Timoth Sebastian ambaye ni dereva bajaj, alisema haoni sababu ya madereva daladala kugoma kutoa huduma kwa sababu wote wanatafuta riziki cha msingi walitakiwa wakae wazungumze namna ya kutatua changamoto iliyopo.

“Sioni sababu za kugoma hapa cha msingi walitakiwa watuite sisi madereva bajaji ili kutafuta suluhisho la tatizo lilipo kwani hata sisi hatupendi kusuguana kila siku barabarani, kwani barabara ambazo zilipangwa kwa ajili ya matumizi ya bajaji ni mbovu na hazijaengwa kwa kiwango kinachotakiwa na nje mji hakuna abiria”, alisema Sebastian.

Mkazi wa Nsalaga Atuganile Julius,alisema kutokana na mgomo huo umemuathiri sehemu kubwa kuendesha shughuli zake za kiuchumi ambazo anazifanya kwenye soko la Mwanjelwa.

“Mimi ni mfanyabiashara bidhaa la urembo kwenye soko la mwanjelwa huwa nafungua duka langu saa moja kamili kwa ajili ya kuwajumlishia wamachinga wadogo,sasa leo nimekaa stendi hadi saa tatu tayali nimepishana wateja wangu”, alisema Atuganile.                

Wafunzi wakosa mtihani

Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya Sekondari Maziwa iliyopo jijini hapa kutokana na mgomo huo wameshindwa kufika shule hivyo kukosa mtihani ambao hufanyika kila mwezi shuleni hapo.

Mwanafunzi wa Shule hiyo Hawa Mwaijenda alisema, siku ya jana ilikuwa siku ya kuanza mitihani ya kujipima ambayo inafanyika kila mwezi.

“Nimefika kituo cha daladala Kabwe tangu saa 12 alfajili, lakini sikuona gari yoyote ambayo inaelekea barabara ya shuleni kwetu na sijui kama walimu watatulewa tukuwaeleza kwamba tumeshindwa kufanya mtihani kisa kukosa usafiri”, alisema Hawa.

Naye Paul Haule alisema,’Hapa tulipo hatuelewi tufanye nini maana hawa madereva bajaji na noah wanasema nauli ni Sh.1000 na sisi nyumbani tumepewa Sh.1000 na wazazi wetu kwa ajili ya nauli  ya kwenda na kurudi pamoja na mutumizi mengine’.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Ulrich Matei alisema mgomo huo umetokana mvutano wa masuala ya kibiashara kati ya bajaji na daladala.

“Kitu ambacho tunatakiwa kuelewana ni kwamba ushindani ulipo kwenye biasahara usafiri kwa sasa umetokana na utandawazi kwani kwa sasa kuna bajaji na kuna bodaboda hivyo kimsingi biashara ya magari itapungua, hivyo wajue kwamba biashara ya usafiri ni huria kwa kipindi hiki na madereva daladala waboreshe huduma zao watapata abiria siyo kulalamika kila siku”, alisema Matei.

Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra) Kanda ya Nyanda za Juu kusini Denis Daud alipotafutwa kwa njia simu haikopokelewa na badala yake alimtaka mwandishi amwandikie ujumbe mfupi kwani alikiuwa kwenye kikao.



Chanzo: mwananchi.co.tz