Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbeya kukosa umeme leo kwa saa 5

Kampuni Ya Kenya Power Kuanza Kutoa Umeme Kwa Mgao Giza

Sat, 6 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkoa wa Mbeya leo utakosa huduma ya umeme kwa saa tano ili kuwezesha kuhamishwa kwa miundombinu ya nishati hiyo kupisha ujenzi wa njia tano za barabara inayoekea nchini Zambia.

Miongoni mwa huduma zitakazoathirika ni afya ambapo hospitali ikiwemo ya rufaa mkoani humo itakosa huduma hiyo.

Taarifa hiyo imetolewa jana Ijumaa Januari 5, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, baada ya kuhojiwa na Mwananchi kuhusiana na barua aliyowekwa kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram ikionyesha kukosekana kwa huduma hiyo kutokana na  kuwepo kwa uhamishaji wa miundombinu ya umeme.

“Nimepata hiyo barua kama ilivyoeleza Jumamosi, Januari 6, 2024 laini namba moja itazimwa ili kumruhusu mkandarasi kuhamisha miundombinu ya umeme eneo la Esso mpaka Mataa, hivyo kuathiri upatikanaji wa umeme kwa saa tano kwenye hospitali ya mkoa na chanzo cha maji Nzovwe.

“Niwaondoe hofu wananchi ndani ya saa tano huduma zitarejea, lengo ni kuharakisha utekelezaji wa mradi wa barabara njia nne kutoka Uyole mpaka Ifisi ambayo ikikamilika itachochea shughuli za kiuchumi,” amesema Homera.

Amesema lengo la Serikali ni kuona miradi mkubwa ya mikakati inatekelezwa kwa wakati, ili Watanzania wanufaike na matunda ya Serikali yao.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu hosptali ya mkoa kukosa umeme kwa saa tano, ofisa uhusiano na mawasiliano wa hospitali hiyo, Agrey Mwaijande amesema wameshafanya maandalizi ya kuwasha  jenereta, hivyo huduma zitaendelea kama kawaida.

“Siku zote tuna jenereta ambalo ikitokea umeme umekatika linajiwasha, kwani limewekwa kwenye mfumo rasmi hivyo hakuna athari zitakazokuwepo katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa,” amesema Mwaijande.

Amesema changamoto kubwa ni gharama za mafuta, kwani kwa saa moja jenereta hilo wanatumilia lita 25 mpaka 30, hivyo lazima wajipange kuhakikisha hakuna huduma itakayokwama.

Akizungumza na Mwananchi mfanyabiashara wa kuchomelea vyuma Mtaa wa Esso jijini hapa, Yohana Yohana amesema kwa muda huo uliotangazwa utawasababishia hasara kwa kupoteza wateja muhimu wakiwepo wa bajaji na magari yanayohitaji huduma hizo nyakati za asubuhi.

“Tumshukuru mkuu wa mkoa kwa uzalendo wake wa kutumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii kutoa taarifa, vinginevyo tungekuta huduma imesitishwa bila taarifa kama ilivyozoeleka,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live