Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbeya kuhimiza wanaume  afya ya uzazi

E16a939d6a6e55ff1c98154cbc45e301 Mbeya kuhimiza wanaume  afya ya uzazi

Sun, 4 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

HALMASHAURI ya jiji la Mbeya imesema imeandaa mpango kamambe wa kuwatumia madiwani,wenyeviti wa mitaa na mabalozi kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa wanaume kushiriki katika ajenda za afya ya uzazi.

Meya wa jiji la Mbeya, Dulmohamed Issa alisema ni jambo linalosikitisha kuona katika karne ya sasa wanaoume hawataki kwenda na wake zao kliniki katika kipindi cha ujauzito na kusema sasa suala hilo litavaliwa njuga ili kuleta mabadiliko.

Alisema hayo baada ya kutembelea vituo vya afya vilivyopo katika kata za Nzovwe na Iyunga na kubaini mwamko mdogo wa wanaume kuongozana na wake zao wajawazito kwenda kliniki.

"Jamani mtoto wa kwetu sote...ule mzigo tukimwachia mama peke yake si sahihi..Wakati wa ujauzito ni wakati wa baba kuwa naye karibu,umwoneshe mapenzi.Katika hili kwa kuwa ninao madiwani wenzangu ambao wana wananchi kwenye kata zao nawatupia mzigo …Wenyeviti wa mitaa na mabalozi nao sasa wasimamie hili,” alisema.

Akiwa katika kituo cha afya Iyunga jijini hapa,Mganga Mfawidhi wa kituo hicho alimwambia wapo wanaume wanaishi maono hafifu kuwa wakiwasindikiza wake zao kliniki watachekwa na kudharaulika katika jamii zao.

"Tukichukulia kwa takwimu za mwezi uliopita ripoti tuliyoandika inaonesha wanawake waliokuja kuanza kliniki wakiwa na ujauzito wa umri wa chini ya wiki kumi na mbili kama inavyoshauriwa walikuwa 12.Lakini kati yao waliokuja na wenzi wao ni walikuwa watatu tu."

Katika Kituo cha afya cha Nzovwe, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho,Dk Leticia Mgeta alisema elimu inahitaji kwa wanaume kutambua umuhimu wa kushiriki kliniki wakati wa ujauzito hadi kujifungua mkewe kwani kwa sasa bado mwamko ni mdogo.

Mganga Mkuu wa Jiji, Dk Jonas Lulandala alikiri kuwa ushiriki wa wanaume katika huduma za afya ya uzazi jijini hapa uko chini na ni tatizo linalohitaji nguvu ya pamoja ya wadau kulishughulikia.

"Tatizo lipo lakini tumejaribu namna ya kuanza kulipunguza ili wanaume waweze kushiriki kwenye masuala ya huduma za uzazi. Kuna umuhimu wake kama baba atashiriki kwenye masuala ya elimu ya uzazi lakini pia akajua huduma ya uzazi inatolewaje,"alisema.

Alisema mwanaume akishiriki suala zima la huduma ya uzazi, atapata elimu, atajua ni lini na idadi ya watoto watazaa na mkewe.

“Wakati wa ujauzito pia atajua aina ya vyakula anavyopaswa kula mkewe na kufanya maandalizi muhimu," alisisitiza.

Chanzo: www.habarileo.co.tz