Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbeya ilivyoanza kuchakata ahadi ya JPM kuigawa wilaya

Cf9f818dec31d97fd4e89da3fe9136f8 Mbeya ilivyoanza kuchakata ahadi ya JPM kuigawa wilaya

Wed, 17 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

UGAWAJI wa maeneo ya kiutawala si jambo geni hapa nchini. Ni mpango wenye kulenga kuongeza maeneo ya kutolea huduma muhimu zikiwemo za kiserikali na hivyo kuwarahisishia wananchi kuzipata kwa ukaribu zaidi.

Hiyo ndiyo sababu kumekuwa na utaratibu wa mara kwa mara wa kugawa mikoa, wilaya, tarafa, kata na vijiji kila Serikali inapojiridhisha juu ya uhitaji wa jambo hilo.

Akiwa katika ziara ya kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana, Rais John Magufuli, wakati huo akiwa mgombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliahidi kuwaondolea wananchi adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma muhimu za kiserikali kwa kuigawa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ili zipatikane mbili sambamba na kuigawa wilaya pia.

Ilikuwa ni mwaka 1984 wakati Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ilipoanzishwa kama halmashauri ya wilaya. Hii ni baada ya kuanza kufanya kazi kwa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Na. 7 (1982).

Mkurugenzi wa kwanza kuitumikia halmashauri hii alikuwa John Matata aliyehudumu kuanzia mwaka 1984 hadi 1990. Huyu alifuatiwa na wakurugenzi watendaji wengine hadi aliyepo hivi sasa, Stephen Katemba.

Halmashauri hii ni moja kati ya saba zinazounda Mkoa wa Mbeya. Nyingine ni Mbarali, Chunya, Kyela, Rungwe, Busokelo na Jiji la Mbeya.

Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya inapakana na Wilaya za Mbarali na Makete kwa upande wa Mashariki, Rungwe na Ileje upande wa Kusini, Magharibi imepakana na Mbozi na Momba mkoani Songwe na Kaskazini Magharibi inapakana na wilaya ya Songwe mkoani Songwe wakati upande wa Kaskazini inapaka na wilaya ya Chunya.

Inaundwa na tarafa tatu za Tembela, Isangati na Usongwe.

Baada ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi mwaka 2014, halmashauri hii ina jumla ya kata 28, vijiji 140 na vitongoji 931 vyenye jumla ya kaya 74,468 ambazo kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 ilikuwa na jumla ya wakazi 305,319, kati yao wanaume wakiwa 143,779 na wanawake ni 161,540, ikiwa na ongezeko la asilimia 2.5 la watu kwa mwaka.

Kwa mujibu wa tovuti ya halmashauri hiyo, ina ukubwa wa kilometa za mraba 2,432 ambazo ni sawa na hekta 243,200 huku eneo linalofaa kwa kilimo katika halmashauri hiyo likiwa hekta 216,400.

Shughuli kubwa za wakazi wa halmashauri hii ni kilimo hasa katika mazao ya kahawa, pareto, viazi mviringo, mahindi na miti kwa ajili ya mbao.

Kutokana na ahadi ya Rais, mwishoni mwa Januari mwaka huu, kikao cha baraza la madiwani kiliridhia mapendekezo ya kuanzishwa kwa wilaya mpya ya Mbalizi sambamba na uanzishwaji wa halmashauri mpya mbili za Mbalizi yenye makao yake makuu katika mji mdogo wa Mbalizi na Isangati yenye makao yake makuu katika kata ya Ilembo.

Kadhalika baraza hilo lilitupilia mbali mapendekezo ya makao makuu ya wilaya mpya ya Mbeya itakayoundwa kuwekwa katika kata ya Inyala zilipo ofisi za muda za halmashauri hiyo kwa sasa na badala yake wakapendekeza makao makuu hayo yapelekwe eneo la Simambwe, yalipo makao makuu ya Tarafa ya Tembela kwa sasa.

Katika kujadili hoja hiyo madiwani kwa kauli moja pasipo uwepo wa hata mmoja kupinga, walionya kutopewa fursa kwa mawazo ya mtu mmoja au kikundi cha watu wachache wanaolazimisha makao makuu kuachwa Inyala kwa maslahi yao binafsi waliyosema hayatakuwa na msaada kwa wananchi kwa kuwa wengi watabaki kuwa mbali na yalipo makao makuu katika kupata huduma muhimu za kiserikali.

Diwani wa kata ya Ulenje, Boniface Njombe, mbali na kupongeza jitihada zilizofanywa na wataalamu wa halmashauri katika kutekeleza agizo la Rais za kuigawa wilaya hiyo na kuanzisha pia halmashauri mpya alisema hana shaka na kuanzishwa kwa halmashauri mbili zilizopendekezwa.

Hata hivyo, alisema hakubaliani na mapendekezo ya makao makuu ya halmashauri itakayobaki kuwekwa Inyala, na badala yake akapendekeza yapelekwe Simambwe.

“Kwa sababu tunawakilisha wananchi na kwa kulinda maslahi ya wananchi na hasa wanaotoka kwenye tarafa hii ya Tembela. Mwenyekiti naomba makao makuu ya halmashauri hii ya Mbeya inayopendekezwa yawe sehemu ambayo makao makuu ya tarafa yapo sasa hivi na hili ni eneo la Simambwe au pale Tembela,” alisema Njombe.

Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Iwiji, Anderson Kabenga lakini akafariki siku chache baada ya kikao hicho, alisema: “Halmashauri hii ya Wilaya ya Mbeya wote tunaijua jiografia yake na yawezekana tunalaumu maendeleo hayaji kutokana na ukubwa uliopo. Mimi pia niungane na mapendekezo ya wataalamu kwamba kuwe na halmashauri ya Isangati makao makuu yawe Ilembo, sina matatizo nawapongeza sana na halmashauri ya Mbalizi makao makuu yawe Utengule. Lakini kwa hoja ya Halmashauri ya Mbeya makao makuu yawe Simambwe.”

Awali Kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya, Nicodemas Tindwa, alivitaja vigezo vilivyotolewa na Tamisemi mwaka 2014 juu ya ugawaji wa maeneo ya kiutawala kuwa ni pamoja na jiografia nzuri ya sehemu yanakopelekwa kuwa makao makuu kuwa sehemu inayofikika kwa urahisi ili kuwapunguzia adha wananchi.

“Kigezo kingine ni uwezo wa miundombinu kama vile majengo ya utawala ili kuweza kutoa huduma, uwepo wa huduma za uhakika za barabara, maduka na pia uwezo wa halmashauri kuweza kujiendesha kimapato angalau kwa asilimia 20, utayari wa wananchi kukubali kuchangia uanzishwaji wa eneo la halmashauri na uwezo wa Serikali wa kuanzisha utawala,” alisema na kuongeza kwamba lingine ni idadi ya watu wasiopungua laki mbili na nusu kwa halmashauri.

“Lakini hivi vigezo vilivyowekwa haimaanishi kwamba lazima vyote vifikiwe, hapana. Unaweza ukawa na vigezo viwili vitatu vilivyofikiwa na vingine vinne vitano visifikiwe lakini bado mamlaka hiyo ikaanzishwa kisheria. Hivyo tusifuatilie vyoote vikamilike.”

Baada ya majadiliano hayo yaliyoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ezekia Shitindi, kaimu mkurugenzi huyo pia aliwataka madiwani kutambua kuwa maamuzi ya kikao hicho si ya mwisho kwa kuwa mapendekezo yaliyofikiwa lazima yapelekwe kwenye ngazi za juu vikiwemo vikao vya ushauri vya wilaya (DCC) na mkoa (RCC) na kisha Tamisemi.

Lakini wakati madiwani wakijadili haya Serikali ngazi ya wilaya nayo ikawa na mapendekezo yake ili kufikia azma ya Rais ya kuwapunguzia adha wananchi.

Katika kutoa salamu za Serikali, Katibu tawala wilaya ya Mbeya, Saitoti Zelothe alishauri halmashauri hiyo na halmashauri ya jiji la Mbeya kuwa na mikakati shirikishi katika uainishaji wa mapendekezo ya kuyagawa maeneo ya kiutawala kwa kuwa upo uwezekano mkubwa wa baadhi ya maeneo kutakiwa kuhamishwa kutoka eneo moja la kiutawala kwenda jingine kutoka yaliyopo hivi sasa kabla ya kuanzisha maeneo mapya.

Zelothe alisema kwa kuwa lengo la Rais ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki za kiutawala kwa urahisi ni muhimu jiografia rafiki ikazingatiwa wakati wa ugawaji wa maeneo ya kiutawala ili matokeo ya mgawanyo huo yawe yenye tija na si yenye kuzua malumbano wala malalamiko ndani ya jamii.

Alishauari kwenye mchakato wa aina hiyo ni vizuri halmashauri zetu zote mbili zikakaa kwa pamoja zikaona ni namna gani nzuri ya kufanya ugawaji wa maeneo.

“Mnaweza mkakuta kwamba kuna baadhi ya kata zinakuwa na tija zaidi kwa wananchi kama zitakwenda kwenye halmashauri ya jiji la Mbeya. Na kuna baadhi ya kata mkaona zinaweza kuwa na tija zaidi zikitoka jijini kuja halmashauri ya wilaya ya Mbeya,” alisisitiza Zelothe.

Anasema kufuatia hali hiyo ni vizuri wataalamu wa pande zote mbili kwa kushirikiana na ofisi yake ya katibu tawala wakakutana kwa pamoja huku akisema kwa upande wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya amesikia tayari kuna mazungumzo yameanza wakitaka kuchukua baadhi ya kata kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kuzipeleka jiji.

Anasema ni vyema vitu kama hivyo vikafanyika kwa ushirikiano wa pamoja ili isitokee baadaye mapendekezo yakafanyika na kupelekwa mbele yakakwama kwa sababu hapakuwa na mbinu zenye kuonesha manufaa ya pande zote kwa maslahi ya wananchi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz