Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watu saba kwa tuhuma za wizi na uharibifu wa miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Juni 17, 2023, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Wilbroad Mutafungwa amesema watuhumiwa hao wamekamatwa baada ya msako uliofanywa na jeshi hilo kwa kushirikiana na Tanesco.
“Juni 5, 2023 usiku eneo la Sagani Wilaya ya Magu mjini zilipatikana taarifa kwamba wahalifu wameshusha transfoma, Askari walifika eneo la tukio na kufanikiwa kumkamata, Karoli Clement (26) mkulima na mkazi wa Kisesa akiwa na pikipiki ambayo walikuwa wakiitumia kwa usafiri baada ya wenzake kutoroka,” amesema Kamanda Mutafungwa
Mutafungwa amesema baada ya kufanya uchunguzi wamefanikiwa kuwakamata wengine sita wanaojihusisha na ununuzi wa vyuma chakavu wakiwa na nyaya ambazo zinadaiwa kuwa na mfanano na nyaya za Tanesco.
“Watuhumiwa waliokamatwa katika msako huo ni Daniel Magege (43) mkazi wa Igudija Kisesa, John Nyangaka (37) mfanyabiashara na mkazi wa Nyamnhongolo, Bahati Stanley (39) mkazi wa Igoma, Marwa Dismas (30) mkazi wa Kangaye, Wilson Joseph (32) mkazi wa Meco, na Ally Tarimo (52) mkazi wa Kilimahewa. Watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika,” amesema Mutafungwa
Hata hivyo Kamanda Mutafungwa ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuliamini Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uharifu na waharifu wote ili hatua za kisheria ziendelee kuchukuliwa dhidi yao.