Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mazoezi ya polisi yazua taharuki benki

19109 Taharuki+pic TanzaniaWeb

Tue, 25 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Taharuki ilitanda leo Jumatatu Septemba 24, 2018 katika mtaa wa One way jijini Dodoma baada ya askari wa Jeshi la Polisi na wale wa  Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ‘kuvamia’  Benki ya NMB tawi la Dodoma kwa ving’ora.

Magari matano yenye askari wenye silaha za moto na vifaa vya kujihami walifika katika benki hiyo wakiwa sambamba na askari kanzu waliokuwa wamevalia kininja.

Hali hiyo ilizua taharuki na kuwafanya baadhi ya wafanyabiashara kutimua mbio na kuacha bidhaa zao, huku wateja waliokuwa ndani ya benki hiyo wakitimua mbio kutoka nje.

Staili ya kushuka ya askari hao katika magari na jinsi walivyokuwa wakiingia na kutoka ndani ya jengo la benki hilo huku wakifunga njia za kuingia katika benki hiyo iliyopo katika jengo la CCM katikati ya jiji hilo, ilikuwa kama filamu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto aliamua kuwatoa wasiwasi wananchi baada ya kutumia kipaza sauti na kusema askari hao walikuwa katika zoezi la utayari.

“Sisi na wenzetu wa benki tulikuja kufanya zoezi la utayari hivyo msiwe na wasiwasi kila kitu kipo salama na hakuna kilichoharibika, hapa tulitaka kuwaonyesha kuwa yakitokea matatizo jeshi lenu lipo imara,” amesema Muroto.

Meneja wa NMB tawi la Dodoma, Harold Lambileki amesema benki hiyo iliamua kufanya zoezi hilo ili kuwapa taarifa wateja wao kuwa wako imara wakati wowote na miamala yao haiwezi kupotea kwani wana ushirikiano mzuri na vyombo vya ulinzi na usalama.

Mmoja wa wateja wa benki hiyo, James Luwaha (74) amesema kitendo walichokifanya kimewaumiza zaidi kwani walikuwa katika foleni lakini ghafla wakaambiwa kuwa moto unawaka ndani na walipoanza kutoka wakakutana na vikosi vya askari wenye silaha.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz