Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mazishi yafanyika chini ya ulinzi wa polisi mume, ndugu wakigombea maiti

B Mazishi Yafanyika Mazishi yafanyika chini ya ulinzi wa polisi mume, ndugu wakigombea maiti

Tue, 3 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi limesimamia mazishi ya Christina Chigunda (35) mkazi wa Kata ya Dodoma Makulu jijini hapa umezikwa chini ya ulinzi wa polisi wenye silaha baada ya kutokea mabishano ya pande mbili za wazazi mahali atakapozikwa mwanamke huyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno amesema ulinzi huo ni wa kawaida kwa Jeshi la Polisi kwani na wao ni lazima washiriki kwenye misiba na sherehe za watu.

Otieno amesema polisi ni sehemu ya jamii kwa hiyo ni lazima washirika matukio kwenye jamii iwe ni msiba au sherehe lakini wanaposhiriki haiashirii kuwa kuna tatizo.

Wakati Kamanda wa Polisi akisema hayo, mwenyekiti wa Mtaa wa Msangalalee Magharibi, Leonard Ndama amesema polisi walilazimika kusimamia mazishi ya mwanamke huyo baada ya kutokea mvutano wa pande mbili za wazazi, huku kila mmoja akidai kuwa ana haki ya kumzika mwanamke huyo.

Mazishi hayo yamefanyika jana Jumatatu Oktoba 2, 2023 kwenye makaburi ya Mkalama yaliyopo Kata ya Dodoma Makulu jijini Dodoma ambayo yamesimamiwa na Jeshi la Polisi, Serikali ya Mtaa na viongozi wa dini.

Kwa mujibu wa historia ya marehemu iliyomwa kanisani wakati wa ibada ya mazishi mwanamke huyo amefariki dunia Septemba 29 mwaka huu baada ya kuugua kwa muda mrefu na alipopimwa aligundulika kuwa na uvimbe kwenye titi.

Ndama amesema suala hilo lilipofika kwenye serikali za mitaa waliona hawawezi peke yao na ndiyo maana walilijulisha Jeshi la Polisi kwa kuwa watu walikuwa wameshaanza kutishiana maisha.

Mwenyekiti huyo amesema upande wa mwanaume walikiri kutoshiriki matibabu ya mwanamke huyo lakini walidai mwili wake kwa sababu ni mke wao halali, huku ndugu wa mke walitaka kumzika mtoto wao wao wenyewe baada ya kutelekezwa na familia ya mwanaume tangu aanze kuugua mwaka jana.

Amesema baada ya majadiliano ya muda mrefu kati ya wazazi, Serikali ya Mtaa na polisi ndipo walikubaliana kuwa mwili wa mwanamke huyo utoke chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, uende kanisani na kisha makaburini na baada ya kumzika watu watawanyike warudi makwao ila mwili usiende kwao wala kwa upande wa mwanaume.

Msimamizi wa ndoa na mume wake, Rehema Palanzi amesema wanandoa hao walikuwa na mgogoro uliosababisha kutengana ambapo mwanaume aliondoka na kwenda Dar es Salaam na kumuacha mwanamke huyo na watoto nyumbani. Palanzi amesema baada ya kuona hakuna huduma yoyote kutoka kwa mumewe na hali yake ya kuumwa aliamua kurudi nyumbani kwao kujiuguza ambapo hata baada ya upande wa mwanaume kujulishwa hawakushiriki kumuuguza.

Amesema hata baada ya kutoshiriki matibabu ya mwanamke huyo ndugu hao walivyosikia mwanamke huyo amefariki walienda kudai wakamzike nyumbani kwao kwa sababu wamemlipia mahari na walikuwa hawajaachana kwa talaka.

"Unajua watu wanakiuka kiapo walichoapa madhabahuni wakati wa kufunga ndoa pale wanaposema watakuwa pamoja kwenye shida na raha, kwenye uzima na ugonjwa sasa mtu anaumwa unamtelekeza hawajui kuwa wamekiuka kiapo walichoapa mbele za Mungu," amesema Palanzi.

Akiongoza ibada ya mazishi Kasisi wa Kanisa la Anglikana, Julius Mbumi amesema tukio hilo limeonyesha kuwa upendo kwa waumini umepoa na ndiyo maana hawataki suluhu.

Amesema matukio kama hayo ya kugombania maiti walikuwa wanayasikia huko mbali lakini sasa yamefika mpaka kwao na kuwataka waumini hao kujitafakari.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live