Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mazishi ya maiti iliyosuswa Mbeya bado kizungumkuti

14414 Pic+mazishi TanzaniaWeb

Wed, 29 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Uongozi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya umesema haujapokea maelekezo kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kuhusu mwili wa Frank Kapange uliohifadhiwa hospitalini hapo tangu Juni 4.

Mwili wa Frank upo mochwari kwa siku 86 sasa na kwa mujibu wa taarifa za uongozi wa hospitali hiyo, ulipelekwa na polisi.

Ndugu wamesusa kuchukua mwili wakidai Frank aliyekuwa mfanyabiashara wa nguo za mitumba sokoni Sido jijini Mbeya alifariki dunia akiwa mikononi mwa askari, wakiwatuhumu polisi kuhusika na kifo chake.

Familia ya Frank ilifungua kufungua maombi Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya ikiomba mahakama kutoa amri ufanyike uchunguzi wa kina kubaini sababu za kifo cha kijana huyo.

Agosti 24, Mahakama iliamuru mwili wa Frank uchukuliwe mochwari na ndugu kwa ajili ya mazishi baada ya kutupilia mbali maombi ya familia.

Uamuzi huo ulitolewa na Mahakama baada ya kusikiliza pingamizi zilizowasilishwa na mawakili wa Serikali.

Pia ilitoa amri kwa mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kutoa mwili na kuwakabidhi ndugu wa marehemu wakazike kama zilivyo tamaduni za Kiafrika badala ya kuendelea kuuacha mochwari.

Mahakama ilielekeza endapo ndugu watagoma kwenda kuuchukua mwili, uongozi wa hospitali kwa kushirikiana na kitengo cha afya cha Jiji la Mbeya kifanye utaratibu wa kwenda kuuzika.

Uongozi wa hospitali

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dk Godlove Mbwanji akizungumza na Mwananchi jana alisema mwili huo bado unahifadhiwa mochwari na hakuna mtu aliyekwenda kuuchukua.

“Ofisi yangu haijapokea taarifa yoyote kwamba Mahakama ilitoa amri kuhusu mwili wa ndugu huyo, hivyo ninachoweza kusema ni kwamba, bado tunaendelea kuuhifadhi mwili hadi pale tutakapopata taarifa rasmi kutoka mamlaka husika kwa kuwa mwili uliletwa hapa na Polisi na ndugu walikuja kumtambua siku tatu baadaye,” alisema.

Harakati za rufaa

Familia kwa upande wake imesema inaendelea na jitihada za kukata rufaa kuhusu uamuzi wa Mahakama ulioamuru wakauzike mwili wa Frank.

Mlezi wa familia hiyo, Julius Kapange alisema jana kuwa hawakuridhika na uamuzi wa Mahakama hivyo wanaendelea na utaratibu wa kisheria wa kutakaa rufaa. “Tupo mahakamani tunashughulikia rufaa, mwanasheria ameshaandika rufaa yenyewe. Hatukuridhika na uamuzi uliotolewa na hakimu, hivyo hatupo tayari kuuchukua mwili wa kijana wetu na kwenda kuuzika hadi pale haki itakapopatikana,” alisema Julius.

Soma zaidi: Kifo cha Kapange kinavyoitesa familia yake, siku 82 zatimia yagoma kumzika

Chanzo: mwananchi.co.tz