Chato. Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mtemi Msafiri ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani humo kumkamata ofisa ununuzi wa halmashauri, Salum Madunda na mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mganza, Daudi Mazoya kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa kituo hicho.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja tangu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika kulieleza Bunge kuwa wakuu wa mikoa (RC) na wilaya (DC) watakaowaweka watu ndani kinyume cha sheria watashtakiwa wao binafsi.
Kutokana na agizo hilo la Msafiri, Mwananchi jana lilimtafuta Waziri Mkuchika kutaka kujua agizo hilo la mkuu wa wilaya ambapo alisema watafutwe viongozi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambao alisema inaweza kulizungumza kwa kina lakini nao walilirudisha kwa Mkuchika.
Alipotafutwa kutolea ufafanuzi jambo hilo, Naibu Waziri Tamisemi, Mwita Waitara alijibu kuwa wanaopaswa kulizungumzia ni Utumishi na Utawala Bora.
Alipoelezwa kuwa Utumishi na Utawala Bora wameeleza kuwa wanaopaswa kutolea ufafanuzi suala hilo ni Tamisemi, Waitara alisema hawezi kuzungumza zaidi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo hakupatikana kuzungumzia suala hilo kwani simu yake iliita bila kupokewa.
Agizo la mkuu huyo wa wilaya kukamatwa kwa watumishi hao linakuja ikiwa siku chache baada ya mkuu wa mkoa wa Geita, Robert Gabriel kukataa kukagua kituo hicho kinachojengwa kwa zaidi ya Sh500 milioni baada ya kutoridhishwa na utekelezaji wake.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara, mkuu huyo wa wilaya alisema utaratibu wa ujenzi wa vituo vya afya na zahanati umeelezwa wazi kutumia vikundi lakini katika Kata ya Mganza umetumika udanganyifu na kutumia fundi.
“Ubebaji wa mchanga hapa kwa gari ni 25,000 lakini hawa wametoa tenda kwa mtu anabeba kwa Sh35,000 na kwa sababu hiyo Sh27 milioni zimetumika, hili halivumiliki,” alisema Msafiri.
Kituo cha Afya Mganza kilianza kwa nguvu za wananchi mwaka 2009 kwa kuanza na jengo la wagonjwa wa nje kutokana na kata hiyo yenye vijiji tisa na vitongoji zaidi ya 40 kutokuwa na zahanati wala kituo cha afya na kusababisha wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya afya.
Aprili 9 alipokitembelea, Gabriel alisema hajaridhishwa na ujenzi huo kwa kuwa wananchi wameweka nguvu kubwa kwenye majengo hayo lakini kasi ya ujenzi haionekani huku taarifa ya fedha ikionyesha haitakamilika kwa fedha hizo.
“Sioni sababu ya kuleta milioni 100, nilitegemea nikute jengo hili limekamilika kwa kuwa lilijengwa na wananchi na bado mmepewa milioni 400 bado haijakamilika. Hili jengo limechangiwa na viongozi mbalimbali chunguzeni muone hapa, nataka nione chenji kwa kuwa mnatumia force account,” alisema mkuu huyo wa mkoa.
Ofisa Mtendaji Kata ya Mganza, James Kongwa alisema kituo hicho kilichoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi, kinajengwa kwa zaidi ya Sh500 milioni na Sh400 milioni zilitolewa na Serikali, Sh100 milioni zilitolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na Rais John Magufuli pia amewahi kukichangia kituo hicho Sh10 milioni.