Siku moja tangu Manispaa ya Ubungo, ianze utaratibu mpya wa kuingia na kadi katika stendi ya ya mabasi ya Magufuli ili kudhibiti upotevu wa mapato, mawakala wa mabasi wamelalamikia utaratibu huo huku wakiomba wapewe vitambulisho maalum vitakavyowaruhusu kulipia mara moja.
Hatua ya matumizi ya N- Card yalianza Jumatatu Februari 20, 2023 ili kupunguza changamoto ya foleni hasa wakati asubuhi ambapo kuna kuwa abiria na wasindikizaji wengi katika eneo hilo.
Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Februari 21, 2023 baadhi ya mawakala wamedai mfumo huo unawalazimu kulipa kila wanapoingia na kusababisha kutumia fedha nyingi kwa siku.
"Tunaomba halmashauri ya ubungo na uongozi wa stendi utufikirie angalau tuwe tunalipa kama mwanzo ukilipa tiketi moja unaitumia hadi jioni lakini mfumo huu unatulazimu kulipa kila unapoingia na kusababisha kutumia fedha nyingi kwa siku," amesema Fatma ambaye ni Wakala.
Innocent Shirima ambaye ni wakala amesema mfumo huo unawakosesha riziki kwa kuwa wanatafuta mahitaji ya watoto kitendo cha kulipa Sh300 kila wanapoingia na kutoka inawasababisha wasipate chochote.
"Mfumo huu unasababisha mtu kama ni kukaa ndani ninndani tu, kama ni nje ni nje tu kwa kuwa hakuna mwenye uwezo wabkulipa kila wakati suala hili Serikali inapaswa kutufikiria angalau tuwe na vitambulisho maalumbtulipe mara moja," amesema Shirima.
Meneja wa stendi hiyo, Isihaka Waziri alisema, mfumo huo unalenga kuwadhibiti mawakala wasumbufu kwa abiria na kudhibiti mapato.
"Kuna hawa mawakala wamekuwa ni wasumbufu kwa abiria, walikuwa wanawafwata nje na kuwasindikiza hadi ndani kupitia mfumo huu labda awe na uwezo wa kulipa kila akiingia na kutoka," amesema Waziri.
Amesema utaratibu huo una kadi za aina mbili, ikiwemo ya muda mrefu, ambayo ama abiria akitaka kumiliki kadi yake atainunua kwa Sh 1000 na kuweka salio kupitia kwa mtoa huduma yoyote ya kitedha na ya pili ni ya kulipia Sh300 ambayo hubaki baada ya mhusika kuingia ndani ya stendi.