Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mavunde aagiza uzalishaji miche milioni 20 ya kahawa

Antony Mavunde.jpeg Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde

Sun, 3 Jul 2022 Chanzo: Mwananchi

Naibu waziri wa Kilimo, Antony Mavunde ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Kahawa nchini (TaCRI) kuhakikisha malengo ya Serikali ya uzalishaji wa miche ya kahawa milioni 20 kwa mwaka huu yanafikiwa.

Mavunde ametoa rai hiyo wakati alipotembelea makao makuu ya TaCRI yaliyopo Lyamungo Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, ambapo amesema Serikali ipo katika mkakati wa kuhakikisha inaongeza uzalishaji wa kahawa ili wakulima wa Tanzania waweze kunufaika na zao hilo.

Amesema lengo la Serikali ni kufikia uzalishaji wa miche ya kahawa milioni 20 na kwamba wataifuatilia ili iweze kuongeza uzalishaji na kuleta matokeo chanya katika kilimo cha zao hilo, ambalo ni miongoni mwa mazao matano ya kimkakati nchini.

"Tunataka uzalishaji wa miche ya kahawa milioni 20, tunataka zao hili la kimkakati lirudi lilipokuwa miaka ya awali na vilevile lisaidie kubadilisha maisha ya watu na kukuza uchumi wa Taifa letu"

Ameongeza kuwa "Lakini pia siyo kuzalisha tu miche milioni 20, muweke mfumo wa kuhakikisha inawafikia wakulima na kuleta matokeo, pia mtusaidie kutoa elimu bora kwa wakulima wetu, kwani tunatamani kuona wanalima kwa tija ili kukuza kilimo cha kahawa nchini".

Mkurugenzi mkuu mtendaji wa TaCRI, Dk Deusdedity Kilambo amesema jukumu kubwa la taasisi hiyo ni kufanya utafiti na kusambaza matokeo ya utafiti kwa wadau, ambapo tayari wamefanikiwa kutatua matatizo makubwa ya magonjwa sugu ya kahawa kwa kutoa aina mpya 19 za kahawa aina ya Arabika na nne za Robusta ambazo hazishambuliwi na magonjwa.

"Tumewekewa malengo ya kushiriki katika kukamilisha uzalishaji wa miche milioni 20, lakini kwa mwaka huu tumeongezewa bajeti kutoka Sh300 milioni hadi Sh800 milioni, hivyo ongezeko hilo litatusaidia kwa kiasi kukubwa kufikia malengo hayo ya uzalishaji miche"

Dk Kilambo ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kugharamia mishahara ya wafanyakazi wenye umri chini ya miaka 45 ambao wanafanya kazi katika taasisi hiyo.

Hata hivyo Naibu Waziri aliahidi kulibeba ombi hilo na kueleza kuwa, atalisimamia na kulifikisha Wizarani kuona kama linawezekana ndani ya mfumo wa utumishi ili kuweza kusaidia watafiti wadogo walioko chini ya miaka 45 katika taasisi hiyo.

Chanzo: Mwananchi