Musoma. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde ameliagiza Shirika la Taifa la Hifadhi za Jamii (NSSF) kuifikisha mahakamani kampuni ya uchimbaji madini ya MMG kwa tuhuma za kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wake katika mfuko huo.
Pia, ameitoza kampuni hiyo faini ya Sh3.6 milioni kwa madai ya wafanyakazi wake kufanya kazi bila kuwa na mavazi ya kinga na usalama mahala pa kazi.
Akizungumza baada ya kufanya mkutano na wafanyakazi wa mgodi huo, Mavunde amesema licha ya uongozi wa mgodi huo kukata makato kwa ajili ya mfuko huo lakini fedha hizo hazipelekwi.
“Uongozi wa NSSF umeomba orodha ya watumishi wenu ili waweze kuweka mahesabu sawa, wajue kwa idadi hiyo wanatakiwa kupokea kiasi gani kutoka kwenu lakini kwa makusudi kabisa mmegoma kuwasilisha orodha hiyo,” amesema Mavunde.
Meneja wa mgodi huo, Esther Kijonga amesema mgodi huo unajitahidi kupeleka michango hiyo kwa wakati isipokuwa kuanzia Mei, 2019 hadi sasa ndio hawajawasilisha michango hiyo.
Mavunde amesema mbali na kutokupeleka michango hiyo kwa zaidi ya mwaka mmoja, mgodi huo ulikataa kupeleka orodha ya watumishi wake kama ilivyotakiwa na NSSF ili mfuko huo uweze kuwa na idadi na kiasi cha fedha kinachotakiwa kupelekwa.
Pia Soma
- Benki Kuu Tanzania yaanzisha mfumo kuwatambua wasiorejesha mkopo
- Waliomuua mtoto kwa kumchoma moto kunyongwa
- Wakuu wa vituo vya polisi Kijitonyama, Oysterbay waitwa mahakamani