Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maumivu mgawo wa umeme wahamia kwenye maji

Maji Mwanza Mwanza Maumivu mgawo wa umeme wahamia kwenye maji

Wed, 27 Sep 2023 Chanzo: mwanachidigital

Wakati maumivu ya mgawo wa umeme yakiendelea nchini, wananchi wameingia kwenye maumivu mengine ya ukosefu wa maji na kutofuatwa kwa ratiba kwa maeneo yenye mgawo.

Ukosefu huo wa maji umeelezwa na baadhi ya mameneja wa mamlaka za maji kwenye baadhi ya maeneo, kwamba unasababishwa na tatizo la kukatika umeme, miradi inayoendelea na sehemu zinazotumia mitambo ya nishati ya jua, kukumbwa na tatizo la ukosefu wa mwanga wa kutosha wa jua.

Gazeti hili siku chache zilizopita liliandika habari kuhusiana na maumivu ya mgawo wa umeme uliopewa jina la ratiba ya umeme nchini, namna unavyoumiza wananchi majumbani na sehemu za biashara na kazi.

Hali hiyo inaendelea kwani Shirika la Umeme Tanzania (Tanseco) lilitoa taarifa kwa umma iliyosema:

“Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linawatangazia wananchi kwamba umeme utakuwa wa ratiba. Kutakuwa na ratiba maalumu ya upatikanaji wa umeme hapa nchini. Hakutakuwepo tena mgawo wa umeme bali kutakuwa na ratiba ya upatikanaji wa umeme.”

Ratiba za umeme pia zimekuwa zikisababisha ukosefu wa maji kwenye maeneo mengi, ambayo mitambo ya kusukuma maji inategemea nguvu ya umeme hivyo kuongeza maumivu kwa wananchi.

Ratiba ya upatikanaji wa umeme imeendelea kutolewa licha ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko kusema suala hilo linafanyiwa kazi kupata ufumbuzi wa kudumu.

Akizungumza mwishoni mwa wiki akiwa mkoani Geita, Dk Biteko alisema katika siku za karibuni, Tanesco yenye Mkurugenzi mpya, Gisima Nyamo-Hanga itaeleza jinsi ya kumaliza tatizo hilo.

Naye Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi, alipoulizwa kuhusu uhaba huo wa maji nchini, alisema wizara inaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa maji yanapatikana.

Hali ya maji mikoani

Zikiwa zimepita siku chache baada ya gazeti hili kuelezea maumivu ya mgawo wa umeme, jana baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Arusha, waliandamana hadi ofisi za Mkuu wa Mkoa, wakilalamika ukosefu wa maji kwa muda mrefu.

Maandamano Arusha yalilisukuma gazeti hili kuangalia upatikanaji wa maji katika maeneo mengine ya nchi.

Kilichobainika ni kuwa ratiba za mgawo wa maji zipo siku nyingi kwa mujibu wa mamlaka za maji kwenye baadhi ya maeneo.

Kwa mfano, jijini Dodoma baadhi ya maeneo yana ratiba, lakini malalamiko ni kwamba ratiba yake haifuatwi.

Gazeti hili lilifanya uchunguzi katika maeneo kadhaa ya nchi na kubaini kuna kilio cha uhaba wa maji kwenye maeneo mengi, huku wananchi wakilalamikia kutofuata kwa ratiba ya mgawo wa maji na sehemu nyingine maji kutoka kwa muda mfupi wa saa mbili au tatu pekee.

Si hivyo tu, maeneo mengine ambayo Mwananchi iliyachunguza hayakuwa na maji hata ya mgawo

Maandamano Arusha

Maandamano hayo jijini Arusha yalikwenda sambamba na kuhoji zilipo Sh520 bilioni zilizotolewa na Serikali tangu mwaka 2021 kukabiliana na tatizo la maji mkoani humo.

Abraham Mollel ambaye ni balozi wa CCM katika shina namba 18, kitongoji cha Mbuni, alisema wameamua kuandamana kwenda kumuona Mkuu wa mkoa Arusha, John Mongella kumwelezea kero ya maji.

“Tumekuja hapa kuonana na mkuu wa mkoa kumweleza kero zetu za maji na kuelekezewa mitaro ya maji, lakini hatujafanikiwa kuzungumza naye kwani katibu wake ametuomba tukaonane na mkuu wa Wilaya ya Arumeru na kama akishindwa kutusaidia turudi kwake,” alisema.

Mollel alisema ndoo ya maji katika eneo hilo imefikia Sh1,000 kama huna usafiri na ambao wana usafiri wanaofuata kwenye visima, ndoo wanauziwa Sh300.

Sio Mushono pekee, bali maeneo mengi ya Jiji la Arusha na wilaya ya Arumeru, kama maeneo ya Sakina, Kiranyi, Makao Mapya, Ngarenaro , Unga Ltd na Daraja mbili, nayo yanapitia changamoto hiyo kwa sasa.

Rehema Msangi mkazi wa Sakina alisema wanashangazwa, kwani Serikali ya awamu ya tano, ilitoa fedha Sh520 bilioni kutatua tatizo la maji Arusha.

Mradi huo maji wa sh 520 bilioni, ulitarajiwa ifikapo desemba mwaka 2022 uwe unazalisha lita milioni 22 za maji kwa siku.

“Sasa tunaomba Serikali ichunguze tatizo lipo wapi kama fedha zimeliwa tuelezwe,” alisema.

Neema Mollel mkazi wa Kiranyi alisema maji yanatoka usiku wa manane na hayana nguvu hata kupanda kwenye matanki, hivyo wanalazimika kubeba kwa ndoo.

Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo hivi karibuni pia alitaka kumalizwa kwa kero ya maji, badala ya Mamlaka ya maji safi na Taka Arusha (AUWSA) kufikiria kuongeza gharama za ankara za maji.

Mkurugenzi AUWSA, Justine Rujumba akizungumza hivi karibuni alikiri uwepo na tatizo la upungufu wa maji na kuahidi kuwa kama mradi mkubwa wa maji utakamilika, kero hiyo itabaki kuwa historia.

“Kwa Siku Arusha inahitaji zaidi ya lita 90 milioni lakini ambazo zinapatikana ni chini kwa sasa, hivyo mradi ukikamilika shida ya maji Arusha na wilaya za jirani itabaki ni historia”alisema

Rujomba alisema mradi huo wa maji safi unakwenda sambamba na mradi wa mabwawa ya majitaka ambao utagharimu zaidi ya Sh15 bilioni na una uwezo wa kutibu majitaka lita milioni 22 kwa siku ndani ya miaka 20, huku mtandao wa maji taka ukiwa ni kilometa 268.

Dodoma

Mkoani Dodoma, baadhi ya wakazi walisema pamoja na kuwepo ratiba ya mgawo wa maji ambao unawawezesha kupata maji mara mbili kwa wiki, ratiba haufuatwi kwani kila siku wanabadilishiwa siku za kupata maji hayo.

Neema Niko mkazi wa Mtaa wa Oysterbay Kata ya Dodoma Makulu, alisema mtaa huo huwa unapata maji mara mbili kwa wiki, Jumatano na Jumamosi, lakini ratiba hiyo huwa inabadilika kila mara.

Alisema kwa wiki tatu mfululizo wamebadilishiwa siku za kupata maji, kwani badala ya maji kutoka Jumatano siku hizi yanatoka Alhamisi na badala ya kutoka Jumamosi yanatoka Jumapili jioni.

“Hata saa za kutoka maji zimebadilika zamani yalikuwa yanatoka mchana kutwa, lakini sasa hivi yanaweza kutoka saa kati ya tano hadi nane tu kisha yanakatika,” alisema.

Happiness Tito kutoka kata ya Ntyuka alisema eneo hilo lina siku mbili za kupata maji kwa wiki, lakini hata yanapotoka huwa hayana kasi kubwa na hutoka kwa saa chache na kisha hukatika.

Wakazi wa eneo la Kikuyu walisema ratiba ya maji kutoka ni Alhamisi na Jumapili, lakini kwa siku za hivi karibuni maji yamekuwa yakitoka kwa kusuasua na wakati mwingine kutotoka kabisa.

Maji kwenye visima vya mitaani pamoja na matanki hununuliwa kwa kati ya Sh500 hadi Sh1,000 kwa dumu la lita 20 kulingana na umbali mtu anapotaka kufikishiwa maji kutoka kisimani.

Hali ilivyo Dar es Salaam

Jijini Dar es Salaam, baadhi ya wakazi walisema kuna tatizo la ratiba na sehemu nyingine hayatoki kabisa.

Mkazi wa Mbezi kwa Msuguli, Adelina Twalibu alisema maji yanatoka mara moja kwa wiki jambo ambalo limekuwa ni kero kwao.

“Kibaya zaidi wiki hii yote hayajatoka na jana (juzi) Jumapili yalitoka kama nusu saa tu kisha yakakatika,” alisema Adelina.

Jumanne Athumani ambaye ni mkazi wa Kimara, alisema kwa eneo hilo kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji ambapo yanatoka mara moja moja na si mara zote kama zamani.

Wakati Athumani akiyaelezea hayo pia, Amina Abdallah mkazi wa Kimara Golani anasema katika eneo hilo wamekosa huduma ya maji kwa takribani wiki tatu mfululizo, hivyo kuwalazimu kununua maji katika visima kila ndoo moja Sh200 hadi Sh300.

“Huku Tabata maeneo ya hapa St Mary tuna siku ya tatu maji hayajatoka. Tunatumia maji ya kisima na wakati mwingine inabidi watu kununua kwa watu wa mikokoteni ambayo wanauza dumu Sh700 kutokana na umbali wa sehemu,” alisema Juliana Kibona mkazi wa Tabata akielezea machungu anayokumbana nayo.

Alisema, ana ndugu zake eneo la Kinyerezi ambapo wakiongea wanasema maji yanatoka wiki hadi wiki wakati mwingine yanapitiliza hata wiki mbili na kuwalazimu kununua maji ya kwenye magari ambayo yanauzwa Sh15, 000 kwa lita 1,000.

“Kwa kipindi hiki ambapo kuna mgawo wa umeme, upatikanaji wa maji umekuwa mgumu na kusababisha uhaba ambapo maji yanaenda kutafutwa sehemu nyingine ikiwemo Kipawa na tunanunua kwenye madumu ya lita 20 kwa Sh500,” alisema Steven Charles mkazi wa Vingunguti.

…Mwanza

Jijini Mwanza mahitaji ya maji kwa siku ni lita milioni 160, huku uzalishaji ukiwa ni lita milioni 90 kwa siku kupitia chanzo cha maji cha Capripoint, hivyo kufanya jiji hilo kuwa na upungufu wa lita za maji milioni 70.

Matarajio na matumaini ya wananchi jijini humo yapo katika mradi wa maji wa Butimba unaogharimu Sh69 bilioni ambapo ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha maji kwa siku lita milioni 48 huku ukitarajia kuwanufaisha watu 450,000.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Mwauwasa, Mohamed Saif, alisema kuna wakati mamlaka inalazimika kutoa huduma kwa mgawo kutokana na upungufu wa maji unaochangiwa na uwezo mdogo wa uzalishaji maji katika chanzo cha capripoint, kwa sababu ya kukosekana kwa umeme.

Bukoba

Wilayani Bukoba Mkoa wa Kagera baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Maruku Halmashauri ya Bukoba Vijijini wanalazimika kununua ndoo ya lita 20 kwa Sh500.

"Mwezi Julai mwaka huu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alifika hapa kukagua utekelezaji wa mradi wa maji na walimwonyesha mradi ulioonekana unatekelezwa, lakini hakuna kilichofanyika tena baada ya ziara hiyo. Kifupi walimdanganya Waziri kwa kumwonyesha mradi kiini macho," alisema Husna Abdallah, mkazi wa Maruku

Mkoani Mtwara

Mkoani Mtwara, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mchanje, Ismail Mussa Mpokotela alisema shida ya maji inasababisha wananchi kutembea zaidi ya kilomita tatu kufata maji Mto Ruvuma, huku Mbunge wa Jimbo la Nanyamba Abdallah Chikota, akisema maji yanakosekana kwa sababu ya uhafifu wa jua kwa kuwa mitambo ya kusukuma maji inatumia nguvu ya jua.

“Lakini, kwa sasa tuna mikakati ya kuhakikisha kuwa miradi yote ya maji inayotumia jua inabadilishwa na kuanza kutumia umeme ili kuepuka changamoto za maji zilizopo katika maeneo yetu ambazo ni kubwa” alisema Chikota.

Meneja wa Mamlaka ya maji Mjini na Vijijini (Ruwasa) Mhandisi, Hamis Mashindike alisema mpaka sasa upatikanaji wa maji katika mji wa Nanyamba ni asilimia 58 ambapo katika Kijiji cha Kitaya kuna mradi ambao utatekelezwa kutoka katika Kijiji cha Ngoja kwenda Kitaya ambapo utanufaika vijiji vitatu vya Kitaya, Kihamba na Dindwa.

Alisema pia upo pia mradi unaotoka katika Kijiji cha Njengwa ambao utanufaisha vijiji vitatu vya Jengwa, Njengwa sokoni na Majengo ambapo kwa sasa umeshafikia asilimia 80.

Moshi

Imebainika kuwa Mji wa Moshi hukosa maji pale umeme unapokosekana huku ratiba ikiathiri upatikanaji wa maji.

Mathalani, jana saa 7:29 asubuhi katika kundi la Whatsapp la ‘Tanesco Huduma Moshi’ kulitolewa taarifa ya umeme kukatika katika visima vya Muwsa vilivyopo Longuo, KCMC, Mawenzi B na KCMC B na kusababisha pampu kutofanya kazi.

Hii ilisababisha maeneo kadhaa kukosa huduma ya maji hususan KCMC, Kitandu, Kiborlon Juu, Shah Tours, Mdawi, Sango na Korini Kusini na umeme ulirudi saa 3:30 asubuhi na pampu kuendelea kufanya kazi lakini ukakatika tena saa 4:34.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa Muwsa, Innocent Lugodisha, alisema hakuna changamoto ya upatikanaji wa maji, isipokuwa hujitokeza kwa wateja wachache wanaohudumiwa kupitia visima vinavyotumia pampu za umeme.

“Changamoto ni umeme, lakini kuna hatua kama mamlaka imeshazichukua na tumeagiza jenereta kwa ajili ya kusaidia pale umeme unapokosekana. Kwetu itatuongezea gharama lakini wateja wetu ni muhimu zaidi,” alisema.

Chanzo: mwanachidigital