Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mauaji ya watoto yasababisha kura kupigwa Simiyu Tanzania

41718 Simiyupic Mauaji ya watoto yasababisha kura kupigwa Simiyu Tanzania

Fri, 15 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bariadi. Mbivu na mbichi kuhusu watuhumiwa wanaodaiwa kuhusika na matukio ya mauaji ya watoto wa kike eneo la Lamadi, wilaya ya Busega mkoani Simiyu itajulikana leo wakati wakazi wa eneo hilo watakapopiga kura za siri kufichua wahusika.

Miongoni mwa wanaoweza kujikuta matatani ni polisi wa kituo cha Lamadi ambao wananchi wanawatuhumu kuwakingia kifua wanaodaiwa wa matukio hayo, kwa kuwatia mbaroni na kuwaachia.

Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka ndiye anatarajiwa kuongoza upigani kura hizo baada ya kukubaliana na ombi la wananchi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika eneo hilo Februari 11.

Wakizungumza wakati wa mkutano huo, baadhi ya wananchi waliwanyooshea vidole polisi kwa kushindwa kuchunguza kwa kina matukio ya mauaji ya watoto watatu wa kike yaliyofanyika kati ya Oktoba 10, 2018 na Februari 8.

Mtoto Susan Shija (9), mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mwabasabi ndiye alikuwa wa kwanza kuuawa Oktoba 10, 2018 na maiti kutelekezwa ndani ya nyumba ambayo ujenzi wake haujakamilika.

Desemba 13 mwaka ja mwili wa mtoto mwingine, Milembe Maduhu (12) uliktwa akiwa ameuawa na kutelekezwa nyumba ya aina hiyo eneo la Lamadi kabla ya tukio lingine la karibuni la Februari 8 la mwili wa mtoto Joyce Joseph (8), mwanafunzi wa darasa la pili Shule ya Msingi Lukungu kukutwa ameuawa.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Emmanuel Gundu aliyehudhuria mkutano huo pia aliunga mkono wazo la kura ya maoni kubaini wanatuhumiwa.

Akizungumzia mauaji hayo, Mtaka alisema Serikali itachunguza kwa kina na kubaini kiini na wahusika wa matukio hayo huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi leo kupiga kura za siri kutaja wanaotuhumiwa.

“Wananchi wawe huru kuwataja wahusika wa matukio hayo kwa sababu wanaishi nao mitaani na wanawafahamu. Muhimu ni kutotumia fursa hiyo kuonea mtu yeyote,” alisema Mtaka.

Kuhusu tuhuma dhidi ya askari, mkuu huyo wa mkoa alisema hakuna aliyezembea katika majukumu yake atakayesalimika baada ya uchunguzi kukamilika.

“Inasikitisha polisi kuhangaika kuwakamata waendesha bodaboda huku wakishindwa kushughulikia masuala ya msingi ya kulinda usalama na maisha ya wananchi. Kama (polisi) mnashindwa kuchunguza mauaji (ya watoto), mnafanya kazi gani? alihoji Mtaka.

Kamanda wa polisi mkoani Simiyu, Deustedith Nsimeki alisema tayari watu wanne wanashikiliwa kwa mahojiano.



Chanzo: mwananchi.co.tz