Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matumizi ya maji Mto Mara  sasa yana mpango rasmi

1292f9128ff9cffed8fa6a65c81f60a3 Matumizi ya maji Mto Mara  sasa yana mpango rasmi

Fri, 21 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAJI ni raslimali muhimu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Maji huhitajika kwa ajili ya shughuli za kilimo, mifugo, uwekezaji wa viwandani, matumizi ya majumbani na pia ni makazi ya viumbe hai.

Hata hivyo, ili jamii iendelee kunufaika na maji ni muhimu kuwe na mipango madhubuti ya matumizi ya raslimali hiyo.

Ni katika muktadha huo, serikali kupitia Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria, hivi karibuni imezindua mpango wa matumizi ya maji ya Mto Mara kwa upande wa Tanzania.

Mpango huo ulizinduliwa hivi karibuni jijini Mwanza na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nadhifa Kemikimba ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Anthony Sanga.

Akizungumza baada ya kuzindua mpango huo, Kemikimba anasema mpango huo wa ugawaji wa maji ya dakio la mto Mara utasaidia katika kuimarisha usimamizi wa raslimali za maji kwa kukomesha migogoro kuhusu matumizi ya maji ya mto huo ikiwemo kukabiliana na tishio la kimazingira linalotokana na ongezeko la idadi ya watu na shughuli za kibinadamu katika bonde hilo.

Kemikamba, licha ya kuwapongeza watalaamu na wadau wote waliowezesha kuzinduliwa kwa mpango huo, anasema mpango huo utasaidia kusimamia matumizi endelevu ya raslimali za maji kwenye bonde hilo, baina ya Tanzania na Kenya.

“Mto huu ni muhimu sana kwa ikolojia katika Bonde la Mto Mara na huchangia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii pamoja na uhifadhi wa uoto wa asili. Niwaagize maafisa wote utekelezaji wa mpango uanze mara moja kwa kuleta matokeo chanya,” anasema.

Mkurugenzi wa Raslimali za Maji kutoka Wizara ya Maji, Dk George Lugomela anaipongeza Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria kwa kuwa bodi ya kwanza kuandaa na kuzindua mpango wa aina hiyo wa matumizi ya maji ambao utakuwa ni kichocheo pia kwa mabonde mengine nchini.

Anasema mpango umeainisha kiasi cha matumizi ya maji yanayohitajika kwa shughuli zote katika eneo la bonde la mto kwa ajili ya matumizi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Dk Lugomela anasema kanuni zote muhimu zinazohusu raslimali ya maji zimezingatiwa kwenye uandaaji wa mpango chini ya mfadhili ambaye ni Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kupitia Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Wanyamapori (WWF).

Ofisa Bonde wa Bodi ya Maji ya Ziwa Victoria, Renatus Shinhu anasema Mto Mara ni chanzo cha maji kinachoanzia kwenye misitu iliyo katika Milima ya Mau nchini Kenya na kupitia katika hifadhi ya Maasai Mara nchini Kenya na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti hapa nchini.

Anasema Bonde la Mto Mara lina ukubwa wa kilomita za mraba 13,325 na urefu wa takribani kilomita 400. Ikolojia muhimu ya bonde hilo huchangia maendeleo endelevu ya kiuchumi, kijamii na uhifadhi wa uoto wa asili kwa nchi hizi mbili.

Anasema mpango wa matumizi ya maji ya mto huo uliandaliwa kwa hatua tano, ya kwanza ikiwa ni tathmini ya raslimali za maji, makubaliano ya pamoja, tathmini ya uhitaji wa maji iliyofanyika 2018 kwa makadirio hadi mwaka 2035 na baadaye kukamilika kwa mpango wa kugawa matumizi ya maji.

Shinhu anasema mpango huo uliandaliwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali; Wizara ya Maji, ofisi za bonde, mtalaamu mshauri, viongozi wa mikoa na wilaya, taasisi za elimu ya juu, Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), ushirikiano wa pamoja wa wadau wa maji (SWP) na WWF na Mgodi wa dhahabu wa North Mara.

Anasema wadau na watalaamu, kabla ya kufikia azma ya kuja na mpango huo walifanya tathmini ya uhitaji wa maji kwenye mto wenyewe na vidakio vyake, kujua raslimali za maji zilizopo, hali ya raslimali hizo katika kila msimu na kila chanzo, kujua kiasi cha maji, kujua mahitaji ya maji kwa sasa na baadae, mahitaji ya maji kwa ajili ya mazingira na kujua ubora wa maji.

Shinhu anachukua hatua kuwapongeza wafadhili watatu; Shirika la Ujerumani la GIZ, SWP na WWF waliofanikisha mpango huo.

Anasema lengo la kuwa na mpango huo wa matumizi wa maji, ni takwa la sheria la usimamizi wa raslimali za maji Na. 11 ya mwaka 2009, kifungu cha 98 ambacho kinampa Waziri mwenye dhamana ya maji katika kuandaa sera, miongozo na mikakati ya kuhakikisha maji yanatumika kwa uwiano unaokubalika, uendelevu na usimamizi bora wa maji shirikishi.

Anasema lengo jingine la mpango huo ni kutokana na kuwepo kwa makubaliano ya pamoja kati ya Tanzania na Kenya kuhusu utunzaji na uendelezaji wa maji shirikishi ya Bonde la mto Mara ili kuhakikisha usimamizi thabiti wa mto huo.

“Nchi hizi zilikubaliana kuandaa mpango huu ambao tayari umezinduliwa hapa nchini ili kupata majawabu ya kiasi cha maji kinachotumika na kinachohitajika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii, ikiwemo kutatua changamoto za kimazingira na migogoro ya matumizi ya maji,” anasema.

Tayari Kenya ilishaandaa mpango wao wa aina hiyo na Tanzania ilikuwa ikisubiriwa ili kuona kila nchi inahitaji maji kiasi gani na matumizi yake.

Anasema kwa kawaida wastani wa mtiririko wa maji katika mto Mara ni lita 126,300 kwa mwaka lakini wakati wa masika huwa lita 256,600, vuli lita 75,200 na kiangazi wastani mtiririko huwa lita 45,800 kwa siku.

“Mpango huu utasaidia usimamizi mzuri wa raslimali maji na bioanuai na kuendeleza sekta muhimu za kiuchumi, utalii, kilimo, ufugaji na madini,” anasema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Maji, Bonde la Ziwa Victoria, Boniventure Baya anasena uandaaji wa mpango huo wa matumizi ya maji umezingatia makubaliano ya pamoja ya nchi za Kenya na Tanzania kuhusu utunzaji na uendelezaji wa maji ya bonde hilo.

Anasema ingawa bonde lina mito mikubwa mingine tisa vikiwemo vyanzo vingine vya maji, Bodi ilianza kutekeleza takwa hilo la kisheria kwa Mto Mara kwa sababu ni mto shirikishi na kwamba unahitaji mpango wa pamoja wa usimamizi wa matumizi ya maji.

Aidha anasema changamoto za kimazingira zinazotokana na shughuli za kibinadamu ndani ya bonde (kilimo, ufugaji, uchenjuaji wa madini) na uwepo kwa hifadhi za Taifa za Serengeti na Masai Mara ndani ya bonde hilo zinahitaji mpango mahususi ili kulinda maji ya bonde hilo.

“Ongezeko la idadi ya watu kutoka 340,500 kwa mwaka 2012 hadi 460,000 wanaoishi kuzunguka bonde ni sababu nyingine ya kuwa na mpango wa matumizi ya maji ya mto,” anasema Baya.

MWISHO

MAELEZO YA PICHA MBILI ZA MAKALA HAYA

Picha-1-

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nadhifa Kemikimba akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mpango wa matumizi ya maji ya Mto Mara. Aliyeshikilia kipaza sauti ni Ofisa Bonde, Bodi ya Maji ya ziwa Victoria Renatus Shinhu na kushoto kwa Katibu Mkuu ni Mkurugenzi wa Raslimali za Maji kutoka Wizara ya Maji, Dk George Lugomela na kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Maji, Bonde la Ziwa Victoria, Boniventure Baya.

Picha-2- Naibu Katibu Mkuu, Mkuu Wizara ya Maji, Nadhifa Kemikimba akitoa hotuba kwenye hafla ya uzinduzi wa mpango wa matumizi ya maji ya Mto Mara.

Picha-3- Wadau waliohudhuria mkutano wa uzinduzi wa mpango wa matumizi ya maji ya Mto Mara hivi karibuni jijini Mwanza.

Picha-DSC0020-

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nadhifa Kemikimba (Wa pili kutoka kushoto) akipiga makofi baada ya kuzindua mpango wa kugawa maji ya Mto Mara hivi karibuni jijini Mwanza. Kushoto kwa Naibu Katibu Mkuu (aliyeshika nakala ya mpango) ni Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na uzalishaji) kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Emil Kasagara na wa kwanza kutoka kulia (aliyeshikilia pia nakala ya mpango huo) ni Mwenyekiti wa Bodi ya Maji, Bonde la ziwa Victoria, Boniventure Baya. Wa pili kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Raslimali za Maji kutoka Wizara ya Maji, Dk George Lugomela.

Chanzo: www.habarileo.co.tz