Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matumizi ya kemikali chanzo cha upotevu mazao ya samaki

Kemikali.jpeg Mwenyekiti wa Taasisi ya Muungano wa Wavuvi nchini (Fuo), Jevenary Matagili akitoa elimu kwa wavuvi

Sun, 11 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Imeelezwa kuadimika kwa samaki aina ya Sangara kunaweza kusababishwa na uvuvi haramu ukiwemo wa matumizi ya nyavu na taa zisizotakiwa wakati wa uvuaji wa samaki na dagaa.

Imeelezwa kuwa bei ya samaki imepanda masokoni ambapo samaki sangara wa vipande vitatu inauzwa kati ya 5,000 wakati awali aliuzwa kati ya Sh1,000 hadi 3,000 kulingana na ukubwa.

Akitoa elimu juu ya matumizi ya taa za sola katika uvuvi wa dagaa eneo la Kayenze Ndogo leo Jumamosi Desemba 10, 2022, Katibu wa Taasisi ya Muungano wa Wavuvi nchini (Fuo), Demai John amesema betri za nje (zinazoonganishwa na balbu wakati wa kwenda kuvua) zina madhara wakati wa uvuvi kutokana na kemikali zilizopo kwenye betri hizo.

“Sasa hivi sangara wamekuwa ni adimu sana, mnakumbuka miaka ya tisini katika uvuvi ndani ya Ziwa Victoria sangara ndio walikuwa wanaongoza lakini sasa hivi dagaa ndio wanaongoza, kama hawa dagaa tusipowatunza tutawambia nini watoto wa watoto wetu? Watakuja kusema baba zetu ndio walivuruga hili ziwa kwa kuvua kwa kutumia kemikali leo hii samaki hakuna.

“Ninyi wote ni mashahidi hapa kuna samaki walikuwa wanaitwa gogo, kuna samaki walikuwa wanaitwa nembe na aina nyingine sasa hivi hazipatikani ni kwa sababu ya madhara kama haya inawezekana kuna vitu vilifanyika huko nyuma leo ndio tunaona madhara ya samaki hawa kutoweka,”amesema

Katibu Mkuu wa Chama cha Wavuvi Tanzania (Tafu), Jephta Machandalo amesema taa za sola zinazotumika ambazo zimeidhinishwa kisheria ni karibu asilimia 10 huku asilimia 90 zinazotumika ni taa haramu na kudai kwa matumizi ya taa hizo haramu samaki wachanga hasa sangara wanachotwa kwa wingi na kupelekea kuwa adimu.

“Ilifikia hatua labda kutokana na hili turudi kwenye karabai lakini ikaonekana kwamba tayari utafiti ulikuwa umeshafanyika kwa aina za taa ya sola pamoja na za betri na kuonekana taa za sola hazina madhara lakini za betri zikaonekana zina madhara.

“Tathimini ikifanyika sasa hivi utakuta wengi wetu tunatumia taa ambazo hazijaidhinishwa na zina mwanga mkali zaidi ya ule unaotakiwa. Kwa nje mtu akiangalia ziwani anaona ni taa za sola lakini kumbe hizo sio sola ni taa za betri ambazo ni matumizi ya majumbani,”amesema

Mwenyekiti wa Fuo, Juvenary Matagili amewataka wavuvi kutumia taa zilizoidhinishwa na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri) ambazo ni Simusolar, Wassha na Sagar Energy Solutions ili kuendeleza rasilimali za uvuvi kwa kizazi cha sasa na cha baadaye.

Naye Kaimu Ofisa Mfawidhi Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Kanda ya Ziwa, Laurent Mbujiro amesema kuna vitendo vya baadhi ya wavuvi kutumia taa za sola zilizoonganishwa na betri kisha kuwekwa chini ya maji kisha mvuvi kuanza kuvua.

“Sasahivi umekuja mtindo wa kuchukua taa hizo zinadumbukizwa chini kabisa, huo ni uvuvi haramu, mnazamisha taa mnavua na vile visivyotakiwa kuvuliwa, wewe umepewa leseni ya kwenda kuvua dagaa kavue dagaa,”

“Tumekubaliana sheria inatukataza tusivue wakati wa mbaramwezi tuziachie nafasi zile dagaa au samaki zetu zipumue, zizaane ndani ya siku 10 baadaye mnarudi mnaendelea ndo utaratibu unasema hivyo, lakini sasa hivi watu mnavua kipindi chote ni hatari, hakutakuwa na uendelevu wa rasilimali za uvuvi,”amesema

Kwa mujibu wa sheria ya uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2019, kifungu namba 66, kifungu kidogo cha (ii) kina sema mtu haruhusiwi kutumia au kusababisha mtu mwingine kutumia taa za sola katika Ziwa Victoria zenye nguvu zaidi ya wax 10 na jumla ya taa za sola katika mtumbwi mmoja zisizidi taa tisa.

Chanzo: Mwananchi