Matukio ya wadau wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, kuvuliwa nguo kwenye upekuzi katika lango la kutokea ndani ya ukuta unayozunguka migodi hiyo yamekomeshwa.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Dkt Suleiman Serera akizungumza mji mdogo wa Mirerani kwenye mdahalo ulioandaliwa na shirika la Civil Social Protect Foundation (CSP) amesema hivi sasa upekuzi ni wastaha.
Dkt Serera amesema matukio hayo yalishamalizika na kutojitokeza tena na hivi sasa wadau wa madini ya Tanzanite wanapekuliwa kistaarabu.
“Pamoja na hayo serikali ipo kwenye mchakato wa kununua mashine ya kupekua ila upekuzi unaofanyika hivi sasa ni wa kistaarabu tofauti na awali,” amesema Dkt Serera.
Katibu wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (Marema) Tawi la Mirerani, Rachel Njau amewataka wanawake wanaoinga ndani ya ukuta huo kuwa na uadilifu ili kuepuka vitendo vya udhalilishaji.
“Hivi sasa upekuzi wa staha unafanyika tofauti na awali ila baadhi ya wanawake wanatorosha madini kwa kuficha kwenye matiti na sehemu za siri ndiyo wanasababisha udhalilishaji,” amesema Njau.
Mwanasheria wa CSP Eliakim Paulo amesema lengo la mradi wao ni kuona changamoto au vikwazo vinavyowakabili wanawake wajasiriamali wa madini ya Tanzanite zinapatiwa ufumbuzi.
“Lengo ni kubaini maazimio tuliyojipangia endapo yamepatiwa ufumbuzi ili tusiibue tatizo juu ya tatizo kwa wanawake wajasiriamali wa madini ya Tanzanite,” amesema Paulo.
Ofisa madini mkazi wa Mirerani mhandisi Menard Msengi amesema serikali imeboresha eneo la upekuzi kwani vyumba vimeongezwa.
Mhandisi Msengi amewataka wadau wa madini ya Tanzanite kutoa ushirikiano na endapo kuna tatizo wapeane taarifa ili waweze kutatua kwa pamoja.