Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matukio manne yatikisa Mbeya

33696 Mbeya+pic Tanzania Web Photo

Thu, 27 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Kuna matukio mengi yaliyotokea mwaka 2018 mkoani hapa, lakini manne ndiyo yaliyoonekana kulitikisa zaidi jiji la Mbeya na kuwagusa watu wengi.

Miongoni mwa matukio hayo ni lile la Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga kushtakiwa kisha kufungwa miezi mitano jela, jingine ni mfululizo wa ajali zilizosababisha vifo vya watu na wengine kupata ulemavu wa kudumu, polisi kutuhumiwa kuua raia na kifo cha aliyekuwa Askofu wa Jimbo la Mbeya (kwa sasa Jimbo Kuu la Mbeya), Mhashamu Evarist Chengula.

Sugu na Masonga kwenda jela

Tukio la Sugu na Masonga ambalo lilivuta hisia kubwa ndani na nje ya Jiji la Mbeya ndiyo la kwanza mkoani hapa, ambapo safari ya wanasiasa hao kwenda jela ilianza Januari 2, mwaka huu Sugu na mwenzake walipoitwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya (RCO) na walihojiwa kwa takribani saa nane kabla ya kuachiwa kwa dhamana.

Januari 16, Sugu na Masonga walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi-Mbeya kwa mara ya kwanza na kusomewa shtaka la kutumia lugha ya kumfedhehesha Rais John Magufuli waliodaiwa kuitoa Desemba 31, 2017 wakati wakihutubia kwenye mkutano wa hadhara jijini Mbeya.

Baada ya kufikishwa mahakamani na kusomewa kosa lao Sugu na Masonga walikana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Michael Mteite alizuia dhamana yao hivyo walikaa mahabusu katika Gereza Kuu la Ruanda kwa siku 24 kabla ya kuachiwa kwa kujidhamini wenyewe kwa maneno. Februari 26 Sugu na Masonga walihukumiwa kwenda jela miezi mitano kila mmoja baada ya kukutwa na hatia ya kutumia lugha ya kumfedhehesha Rais Magufuli.

Lakini Sugu na Masonga walitumikia kifungo hicho kwa siku 73 kabla ya kuachiwa huru Mei 10 mwaka huu kwa msamaha wa Rais siku ya sherehe za Muungano.

Vifo ajali za barabarani

Kuanzia Aprili hadi Septemba Jiji la Mbeya lilikumbwa na simanzi nzito kutokana na mfululizo wa ajali za barabarani zilizosababisha vifo vya watu 61 na wengine kupata ulemavu wa kudumu.

Ajali hizo zilitokea kwa nyakati tofauti ambapo Aprili 9, watu wanane walifariki papo hapo baada ya gari dogo aina ya Noah kugongana uso kwa uso na basi kubwa la abiria eneo la Igodima kata ya Iganjo na mmoja alijeruhiwa.

Juni 14, watu 13 wakiwamo vijana 10 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Ofisa wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) mmoja, dereva na kondakta wake walikufa na vijana wengine wa JKT 48 kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Tabora kwenda Kambi ya JKT-Itende kikosi cha 844KJ-Itende kwa mafunzo ya vitendo kupinduka eneo la mteremko wa Mwasekwa Jijini Mbeya barabara ya Mbeya Mjini-Chunya.

Julai 1, watu 20 walifariki papo hapo na wengine 45 kujeruhiwa baada ya lori kugonga mabasi madogo ‘Daladala’ na magari mengine matatu ya abiria kwenye mteremko wa Mlima Iwambi-Mbalizi wilaya ya Mbeya katika barabara kuu ya Tanzania-Zambia.

Lakini kabla tukio hilo halijasahaulika, siku tano baadaye (Julai 5) watu watano walifariki papo hapo na mmoja kujeruhiwa. Ajali hiyo ilihusisha lori la mizigo lililofeli breki likiwa kwenye mteremko mkali wa Igawilo jijini hapa barabara kuu ya Tanzania –Malawi kisha likaparamia magari mengine matatu kabla ya kupinduka na kulalia gari dogo aina ya Noah na kusababisha vifo hivyo.

Septemba 7, watu 15 walipoteza maisha na wengine 15 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari matano, manne yakiwa malori na moja la abiria (Hiace) eneo la Mlima Igawilo jijini Mbeya.

Polisi kutuhumiwa kuua raia

Tukio lingine lililovuta hisia kwa wakazi wa Jiji la Mbeya ni kuhusiana na vifo vya vijana wawili ambavyo vilitokea Machi na Juni, huku polisi wakituhumiwa kuhusika kuwaua kwa nyakati tofauti.

Mkazi wa Iyela II, Jijini Mbeya, Alen Mapunda (20) ambaye alikuwa mfanyabiashara wa machungwa Soko la Sido jijini hapa, alifariki dunia huku kifo chake kikigubikwa na utata na ndugu wa kijana huyo wakiwatuhumu polisi kwamba walihusika kumuua baada ya kumkamata mtaa wa Maendeleo.

Tukio hilo lilitokea saa 4 usiku Machi 24 ambapo ilidaiwa kijana huyo alikamatwa na polisi akiwa eneo la kuchezea ‘pool table’ kisha akapelekwa kituo kikuu cha polisi na alikaa mahabusu siku moja kabla ya kudhaminiwa na ndugu zake, lakini kutokana na majereha aliyokuwa nayo kichwani, mikononi na miguuni walimpeleka Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya ambako alifariki.

Kifo kingine ni cha Frank Kapange (21) ambaye hadi sasa mwili wake umefikisha siku ya 206 ukiwa mochwari baada ya ndugu zake kugoma kuuchukua wakidai kijana wao alifariki akiwa mikononi mwa polisi.

Frank alifariki Juni 4 mwaka huu huku kifo chake kikigubikwa na utata kutokana na mazingira yake baada ya ndugu kudai kijana wao ambaye alikuwa mfanyabiashara wa mitumba Soko la Sido alifariki kwa kipigo akiwa mikononi mwa polisi hivyo waligoma kuchukua mwili na hadi sasa upo mochwari huku polisi wakituhumiwa kuhusika.

Ndugu waligoma kuuchukua na kuuzika mwili wa kijana wao kisha wakakimbilia mahakamani kufungua shauri la kuiomba itoe amri ya kufanyika kwa uchunguzi rasmi wa kifo cha kijana wao, lakini Mahakama ya Hakimu Mkazi-Mbeya ilitupilia mbali shauri hilo na kuamuru mwili huo kuzikwa na ndugu wanahitajika kubeba gharama zote za mazishi.

Hata hivyo, ndugu hao walidai kutoridhika na uamuzi huo, wakaamua kukata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ambayo nayo ilitoa uamuzi wa kuifuta kesi hiyo baada ya kujiridhisha kwamba mlalamikaji hakufuata taratibu zilizopaswa wakati wa kufungua kesi hiyo.

Hadi sasa mwili wa Frank haujazikwa huku wakili wa familia hiyo, Moris Mwamwenda akitoa msimamo kwamba ameweka kusudio la kukataa rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi Mahakama Kuu.

Kifo cha Askofu Chengula

Kifo cha aliyekuwa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya, Mhashamu Evarist Chengula kilishtua na kuwagusa watu wengi ndani na nje ya Mbeya.

Askofu Chengula alifariki dunia Novemba 21 wakati akipatiwa matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete-Muhimbili Jijini Dar es Salaam na mazishi yake yalifanyika Novemba 27 ndani ya Kanisa la Kiuaskofu la Mtakatifu Antony wa Padua Jijini Mbeya.

Askofu Chengula alipendwa na watu wengi hususan waumini wa kanisa hilo kutokana na misimamo yake aliyoisimamia na kuwa tayari kukemea na kusema bila kuogopa chochote.



Chanzo: mwananchi.co.tz