Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mateso abiria wa treni wakwama siku mbili stesheni

Hali Mbaya Usafiri Wa Treni Mateso abiria wa treni wakwama siku mbili stesheni

Thu, 23 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamia ya abiria waliokuwa wasafiri na treni ya Tazara kwenda mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani ya Zambia, wamekwama kwa siku mbili huku wakiwa hawafahamu hatma yao kutokana na kutopewa taarifa yoyote na mamlaka husika.

Abiria hao walipaswa kuondoka juzi Jumanne Novemba 21, 2023, lakini hadi jana Jumatano Novemba 22, saa tano usiku walikuwa hawajui hatma yao baada ya kufika stesheni na muda wa kuondoka ulipofika hawakuondoka bila kuelezwa chochote.

Wakisimulia mateso wanayoyapitia kutokana na kuahirishwa kwa safari hiyo, abiria hao wamesema wamekuwa wakiuziwa vyakula kwa bei ya juu pamoja kulala kwenye mazingira ya tabu huku baadhi yao wakiwa na watoto wadogo pamoja na wagonjwa.

Scolastika Mapunda, aliyekuwa asafiri kwenda Gwata, amesema ameamua kutumia usafiri wa treni kutokana na barabara kuwa mbovu, lakini cha kusikitisha amekaa siku ya pili bila kuondoka na kuna taarifa yoyote waliyopewa.

“Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mengi mabasi hayafiki, tumeamua kutumia treni lakini mateso tunayopata ni kama haya. Tuliambiwa tutaondoka Jumanne saa tano hadi usiku hatujaambiwa chochote, mbaya zaidi hata wahusika ofisini hawapo,” amesema Mapunda.

Amesema si mara ya kwanza kusitishiwa safari, kwani ratiba zimekuwa zikibadilishwa mara kwa mara na wamekuwa hawapewi taarifa huku wakiuziwa vitu kwa bei ya juu.

Ramadhan Issa aliyekuwa asafiri kwenda Mbeya, amesema treni hiyo imekuwa ikisitisha safari mara kwa mara, mbaya zaidi hakuna taarifa inayotolewa huku baadhi yao wakiwa wanawahi kwenye misiba au wanasafirisha wagonjwa.

“Nimeomba ruhusa ofisini kwa Jumatatu, nikitegemea Jumanne tuondoke ili niwahi kugeuza na treni ya Alhamisi, cha kushangaza hiyo siku hatukuondoka wala kupewa taarifa, tukalala siku iliyofuata tumeshinda bila taarifa yoyote, mbaya zaidi hakuna kiongozi hata mmoja,” amesema.

Neema Mwakipesile aliyekuwa anasafiri kwenda Mbeya akiwa na watoto watatu amesema tatizo sio kusitishwa au kubadilishwa ratiba, wamekuwa wakikaa hapo bila kujua hatma yao na muda wa safari.

Amesema wamekuwa wakiuziwa vyakula bei ya juu, licha ya kutojali abiria anayesafiri ana hali gani au anapokwenda ni nini kinachompeleka.

“Fikiria nina siku mbili haoa, nipo na watoto watatu kikombe cha uji nauziwa Sh 1,500 chakula sahani Sh3,000 hadi Sh4,000 unatoa wapi fedha pengie mtu unakwenda kwenye matatizo,” amehoji Mwakipesile.

Hadi jana saa tano usiku, abiria hao walikuwa hawajaondoka, hata hivyo, jitihada za kuupata uongozi wa Tazara haukuzaa matunda baada ya namba za viongozi kuita bila kupokelewa na ofisi zao kuwa zimefungwa.

Alipotafutwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema kumekuwepo na changamoto ya treni na uchache wa vichwa pamoja na ubovu wa miundombinu.

Amesema katika mkakati wa muda mrefu, Serikali inafikiria kufanya maboresho makubwa kwa kushirikisha nchi ambazo wanashirikiana tangu wakati wanajenga reli hiyo.

“Tunaweza kuja na mpango mkubwa, nadhani kuanzia mwakani wa namna ya kufumua reli hiyo na kuiboresha pamoja na kuweka mfumo mzuri ikiwemo kuongeza mabehewa kupitia uwekezaji,” amesema Kihenzile.

Amebainisha kuwa hali ya treni zote ikiwemo Shirika la Reli Tanzania (TRC), miundombinu yake ni mibovu wakati mwingine abiria wanachukua muda mrefu kufika wanapokwenda kutokana na uchache wa vichwa na ubovu wa miundombinu.

“Serikali imejipanga kuja na muarobaini wa namna ya kumaliza tatizo na kupata ufumbuzi wa kudumu, kwa tatizo liliotokea siwezi kuwa na majibu ya moja kwa moja kwanza sijapata taarifa kwa hiyo sitakuwa kwenye nafasi nzuri ya ulizungumzia,” amesema

Miongoni mwa abiria hao walikuwa wakisafiri kwenda maeneo mbalimbali ikiwemo Mlimba Morogoro, Njombe, Iringa, Tunduma na nchi jirani ya Zambia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live