Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa vivuko vitano vinavyojengwa na Serikali kupitia Kampuni ya Songoro Marine Transport Limited umefikia kati ya asilimia 35 hadi 72.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa wanafunzi na viongozi 15 wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (NDC), Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine, Meja Songoro amesema ujenzi wa vivuko unagharimu Sh18.7 bilioni.
Songoro amesema ujenzi wa Kivuko cha Bwiro-Bukondo ambacho kinagharimu Sh601 milioni, umefikia asilimia 72 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 29, 2024.
Kuhusu ujenzi wa kivuko kitakachofanya safari kati ya Kisiwa cha Rugezi na Kisorya wilayani Bunda Mkoa wa Mara kinachogharimu Sh892 milioni umefikia asilimia 71 huku kikitarajiwa kukamilika Aprili 29, 2024.
Songoro amesema kivuko kitakachotoa huduma kati ya Kisiwa cha Ijinga na Kahangala wilayani Magu Mkoa wa Mwanza kinachogharimu Sh5.2 bilioni, ujenzi wake umefikia asilimia 70 na kitakamilika Machi 29, mwaka huu.
“Kupitia mradi huu tumetoa ajira kwa vijana wazawa zaidi ya 100 miongoni mwao ni waliohitimu katika vyuo vya ufundi stadi. Pia, tutaendelea kutoa ajira kwa vijana wengi zaidi,” amesema Songoro.
Katika hatua nyingine, Kivuko cha Nyakalilo-Kome wilayani Sengerema mkoani humo kinachogharimu Sh8 bilioni, kimefikia asilimia 55.5 na kitakamilika Aprili 29 mwaka huu huku kivuko cha Buyagu-Mbalika ambacho kinagharimu Sh3.8 bilioni ujenzi wake umefikia asilimia 35 na kitakamilika Februari 23, mwaka huu.
Akizungumzia mradi huo, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (NDC), Meja Jenerali, Wilbert Ibuge amesema kupitia ziara hiyo wanafunzi na uongozi wa NDC umejifunza kuhusiana na ushirikishwaji wa sekta binafsi na sera za Serikali.
“NDC ilianza mwaka 2012 na sasa tuko na kozi ya 12 inayoshirikisha viongozi waandamizi wa kijeshi na vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi maofisa wakuu waandamizi kutoka taasisi za kiraia. Katika kushiriki kozi hizo tunaanza na nadharia kisha vitendo ndiyo maana leo tumekuja kwenye vitendo,” amesema Meja Jenerali Ibuge.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amemtaka Kaimu Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), Vitalis Bilauri kuhakikisha anafuatilia kwa kina ujenzi wa vivuko hivyo huku akimtaka Songoro Marine kukamilisha mradi huo kwa muda uliopangwa.
“Vivuko hivi vikikamilika vitarahisisha usafiri ziwani kuwa na usafiri wa uhakiki, wananchi hawa kwa muda mrefu na mara kwa mara wamekuwa wakitumia vivuko na mitumbwi kwa hiyo ni uwekezaji mkubwa katika sekta ya usafirishaji,” amesema Makalla.
Joyce Mbunju ambaye ni miongoni mwa washiriki wa ziara hiyo kutoka NDC amesema mradi huo siyo tu utaboresha miundombinu ya usafirishaji mkoani Mwanza, pia utaongeza ujuzi kwa vijana jambo linaloifanya Serikali ijitengenezee watalaamu wa ndani wa ujenzi wa ndani.
“Tumepita eneo la mradi na kukutana na vijana wengi wa Tanzania ndiyo wanaojenga hivi vivuko, hii ni ishara kwamba ujuzi wa ujenzi huu unazidi kusambaa kwa watanzania wengi zaidi. Serikali iendelee kutoa miradi kwa wawekezaji wazawa kuongeza ujuzi wa watanzania,” amesema Mbunju.
Meja Songoro ni miongoni mwa Watanzania, wanaomiliki kampuni za ujenzi wa meli, mbali na ujenzi wa vivuko hivyo, kampuni yake imetanuka na kupewa mikataba ya ujenzi wa meli na vivuko katika Bandari ya Hindi na nchini Uganda.